31 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Misoji Nkwabi Anakuja upya, Hapendi ujinga…

img-20160929-wa0034

Na JOHANES RESPICHIUS,

SHINDANO la kumsaka staa wa Bongo, linalokwenda kwa jina la Bongo Star Search (BSS) limekuwa likiibua wasanii mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya vyema katika gemu la muziki wa Bongo Flava.

Baadhi ya wasanii wanaofanya vizuri kwenye gemu ambao walitokea BSS ni pamoja na Peter Msechu, Kala Jeremiah, Kayumba Juma, Misoji Nkwabi na wengine wengi.

Lakini leo Swaggaz limepiga stori na mshindi wa shindano hilo, mwaka 2008, Misoji Nkwabi, ambapo amezungumzia mambo mengi kuhusu safari yake katika sanaa.

Misoji ameweka wazi kilichomfanya awe kimya kwa muda mrefu ambapo amesema kuwa alikuwa akifanya kazi ya uelimishaji wa masuala ya ukatili wa kijinsia.

Akizungumzia kuhusu wasanii wanaotokana na BSS kutofanya vizuri anasema: “Suala hilo naweza kuliongelea kwa upande wangu maana sijui wenzangu wako vipi, binafsi sijawahi kupotea kwenye gemu sema nilikuwa nikifanya kazi na mashirika mbalimbali kutokana na nyimbo zangu ambazo nimekuwa nikiimba.

“Wimbo wangu ya Ukimwi ulinifanya niweze kuzunguka nchi nzima nikiwa na Shirika la Healthy Family International kwahiyo nikawa mtu wa kutembea mikoani,” anasema Misoji.

KUREJEA SHULE
Anasema sababu nyingine iliyompoteza kwenye game kwa muda ni kuendelea na masomo, maana wakati akishiriki fainali ya BSS, alihairisha kufanya mitihani yake ya kidato cha sita.
“Kabla ya kwenda BSS nilikuwa nimeruka mitihani yangu ya kidato cha sita hivyo mashindano yalipomalizika nilirudi kufanya, nashukuru nilifaulu kwenda chuo.

“Baada ya hapo nilipata safari ya kwenda Ujerumani, nikawa siyo mtu wa kutulia kufanya muziki na sasa nimetulia naanza kazi.
“Katika kuwadhihirishia hilo, wiki ijayo natarajia kuachia vibao vyangu vipya viwili; ‘Nampenda’ na ‘Usawa’, mashabiki wakae mkao wa kula, mambo mazuri yanakuja. Nipo tayari sasa kuwashika. Narudi kwa kasi,” anasema Misoji.

MAPENZI SIYO DILI
“Mapenzi ni maisha ya kila siku na kila sehemu yapo lakini mbali na mapenzi kuna mambo mengi yanaendelea nchini kama ukatili, mauaji ya Albino, magonjwa, mazingira, siasa na mengineyo mengi.
“Mimi ni mwanamke na nimekutana na mambo ya kunyanyasika kijinsia ingawa siyo kwamba nimefanyiwa kitu kikubwa sana lakini hata kudharauliwa ni moja ya unyanyasaji.
“Mfano shuleni kama msichana unafanya vizuri katika masomo wapo vijana ambao hudiriki kusema kuwa hawawezi kuongozwa na msichana kwamba ‘demu demu tu atanipitaje?’.
“Hilo na mengine mengi, yamenifanya niimbe zaidi kuhusu harakati kuliko mambo ya mapenzi. Kila msanii anaimba mapenzi, jamii ina matatizo mengi zaidi ya mapenzi,” anasema Misoji.
Kutokana na matukio hayo, kwa kushirikiana na Mtandao wa Kijinsia aliamua kutunga wimbo wa ‘Usawa’ wenye kuhamasisha usawa na haki kati ya mwanamke na mwanaume.

ANAMILIKI BENDI
“Nashukuru kwa sasa nina bendi yangu inaitwa Afrijamu Band, nalipa mishahara wafanyakazi wangu na kutumia sanaa kutatua matatizo mbalimbali yaliyopo katika jamii inayotuzunguka.

“Nyimbo zangu nyingi hulenga katika kuelimisha jamii hasa kwa upande wa masuala ya kijinsia ambapo nimeona kuna tatizo sana, mfano katika mikoa ya Mara, wilaya za Musoma na Tarime ambako kumekuwa kukitokea matukio mbalimbali ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Hivyo basi kutokana na hali hiyo niliamua kutatua tatizo hilo kwa kutumia sanaa yangu kuelimisha jamii, wanaume kwa wanawake. Kila wimbo wangu lazima uwe na maneno yenye ujumbe,” anasema Misoji.

Anasema aliamua kuanzisha Afrijamu Bandi kutokana na hulka yake ya kutopenda kutumbuiza majukwaani kwa kutumia ‘background’ za nyimbo.
“Huwa sipendi kupigiwa ‘background’ nikiwa jukwaani natumbuiza, napenda sana kufanya muziki live, hicho ndicho kilinipelekea kuunda bendi.

“Mwanzo kabla ya BSS nilikuwa naimba ila kuna kipindi niliamua kukusanya watu ili tuweze kushirikiana kufanya muziki na bahati nzuri wasanii wa Bagamoyo huwa wako tofauti,”anasema Misoji.

Anasema watu ambao hawaijui bendi yake wajitayarishe kuijua zaidi kwani mpango wake ni kuendelea kutoa kazi nyingi pamoja na kufanya maonyesho katika maeneo mbalimbali ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles