Na Safina Sarwatt, Moshi
MISITU ya asili nchini ipo hatarini kutoweka kutokana na uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu na kuongezeka kwa joto.
Kutokana na hali hiyo imeelezwa kuwa kuna ya kuibuka kwa kasi magonjwa ya milipuko yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Balozi wa Mabadiliko ya Tabianchi nchini, Mchungaji Profesa Aidani Msafiri alikuwa akizungumza katika kongamano la vijana na viongozi wa dini mjini Moshi.
Alisema kuwa uoto wa asili nchini umetoweka kwa asilimia 60 kutokana na uharibifu wa mazingira.
Profesa Msafiri alisema jambo hilo limesababisha kukauka vyanzo vya maji, kuongezeka joto kali na kushuka kiwango cha uzalishaji wa mazao ya chakula.
“Tanzania kwa sasa imebakia kama jangwa wengine wanaona suala hilo kama mzaha lakini hali ilivyo kwa sasa siyo nzuri.
“Asilimia 40 tu ya miti ya asili ndiyo imebaki,” alisema Profesa Msafiri.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga, alisema hali ya joto kwa mkoa huo imezidi kuwa mbali kuwa na hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
Alisema utafiti unaonyesha baada ya miaka 20 Mkoa wa Kilimanjaro utakuwa kame zaidi kuliko Mkoa wa Dodoma.