29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mishahara ya vigogo yaanza kufyekwa

B-3*Waziri Kairuki aeleza namna bodi inavyochambua

* Kambi ya upinzani yaja juu, watumishi hewa 4,317 wabainika

FLORIAN MASINDE NA JOHANES RESPICHIUS, DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kutoa agizo la kupunguza mishahara mikubwa ya watendaji wa mashirika ya umma, hatimaye Serikali kupitia Bodi ya Mishahara imeanza kazi ya kufanya marekebisho hayo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Magufuli, kuagiza kushushwa kwa viwango vya mishahara ya viongozi wa mashirika ya umma ambapo wengine hulipwa Sh milioni 36 hadi milioni 40 kwa mwezi.

Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema katika kipindi cha miezi 15 kuanzia sasa mishahara ya watumishi hao itapunguzwa na kuwa yenye uwiyano.

“Katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa tunayo Bodi ya Mishahara ambayo ilianzishwa katika Serikali ya awamu ya nne na jukumu lake kubwa ni kufanya mapitio ya mishahara mbalimbali na kuhakikisha mishahara ya watumishi wa umma haipishani sana.

“Hatua ambazo tumeanza kuzitekeleza, tayari mamlaka zetu zimeanza kukutana kupitia Utumishi, Hazina na Msajili wa Hazina ili kuangalia namna ya kulitekeleza agizo hilo,” alisema Waziri Kairuki.

Alisema kutokana na hali hiyo mamlaka hizo hivi sasa zinaangalia mishahara ya taasisi mbalimbali na watumishi ili kuweza kubaini wale wanaolipwa zaidi ya Sh milioni 15 ni wangapi na itakatwa vipi.

Akizungumzia taasisi zinazozalisha kwa kiwango kikubwa na kuwa na uwezo wa kujiendesha, Waziri Kairuki, alisema Bodi ya Mishahara hivi sasa ina jukumu la kuangalia uwiano baina ya mtumishi wa umma na mashirika ya Serikali.

“Unakuta mtumishi wa taasisi X kiwango chake cha elimu, uzoefu, ujuzi, muda wa kuingia kazini pamoja na kazi anayoifanya ni sawa na ya mtumishi wa taasisi Y lakini unakuta mtumishi X analipwa mshahara mkubwa zaidi ya mara tano ya mtumishi Y jambo ambalo si haki katika utumishi,” alisema.

Kauli ya Magufuli

Machi 30, mwaka huu akiwa wilayani Chato, Mkuu huyo wa nchi, alisema kuna watu wanalipwa kiwango kikubwa cha mishahara na wamekuwa wakiishi kuliko hata malaika na sasa ni lazima washushwe ili waishi kama shetani.

Hatua ya Rais Magufuli, kupitisha panga na kuweka uwiyano wa mishahara kwa watendaji wa taasisi hizo unaelezwa kuwa utaisaidia uwajibikaji na usawa kwa watendaji.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli, alishangazwa na baadhi ya bodi za wakurugenzi kushindwa kufanyakazi zao kwa mujibu wa sheria na badala yake wamekuwa na kazi ya kupandisha mishahara kwa watendaji.

Alisema anashangazwa na bodi hizo, kwani kila kukicha zimekuwa zikifanya kazi ya kupandisha mishahara pamoja na kufanya vikao nje ya nchi.

Alisema hivi sasa ameunda timu ya wataalamu ambayo imeanza kufanya kazi ya upunguzaji mishahara mikubwa kwa watendaji wakuu wa mashirika ya umma.

“Tena hawa wakurugenzi ndio wanaongoza kwa kulipwa fedha nyingi na hata kwenda kufanya vikao ulaya. Ninasema hapa kwamba suala hili litaanza kushughulikiwa katika bajeti hivi karibuni,” alisema Rais Magufuli.

Alisema tayari ameunda timu ya wataalamu ambayo inafanya kazi ya kupunguza mishahara hiyo na kufikia Sh milioni 15 kwa mwezi ili asipatikane Mtanzania anayelipwa zaidi ya kiwango hicho.

“Kuna watu wanaishi kuliko hata malaika lazima tuwashushe waishi kama shetani,” alisema Rais Magufuli.

Mishahara hewa

Katika hatua nyingine Waziri Kairuki alisema kuwa Serikali imeokoa Sh bilioni 3.95 katika kipindi cha kuanzia Machi Mosi hadi April 4 mwaka huu ambazo zingetumika kulipa mishahara ya watumishi hewa 4,317 nchini kote.

Alisema baada ya kupokea taarifa za awali za watumishi hewa kutoka kwa wakuu wa mikoa wamebaini kuwepo kwa upungufu katika taarifa hizo.

Alitaja upungufu huo kuwa ni pamoja na taarifa hizo kutokuwa na majina ya watumishi hao na waliotolewa kwenye malipo, sababu za kuondolewa pamoja na utambulisho.

Kutokana na dosari hizo wizara yake imewaagiza waajiri wote wawe wamewasilisha taarifa zao wiki hii ili kuwezesha kujua kwa usahihi wa watumishi ambao ni hewa na hatua ambazo zinachukuliwa.

Kambi ya upinzani yachambua

Kwa upande wake Waziri Kivuli na Msemaji Mkuu wa Kambi ya upinzani bungeni, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ruth Mollel,  alisema kuna tatizo ambalo linachangia kuwepo na kukua kwa tatizo la watumishi hewa katika utumishi wa umma.

Alisema tatizo hilo ni udhaifu mkubwa wa Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ndio Tume Rekebu yenye jukumu la kuhakiki raslimali watu katika utumishi wote wa umma.

“Kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizotolewa na Tume hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa hivi karibuni, Tume hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa yanayokwamisha utendaji kazi wake.

“Kwa mfano, Tume hiyo haina watumishi wa kada mbali mbali, vitendea kazi vya aina mbali mbali kama vile magari, kompyuta na vifaa vingine vya ofisi.

“Na katika mwaka huu wa fedha, Tume ya Utumishi wa Umma imepatiwa aslimia 9.3 ya fedha iliyotengwa kwenye bajeti kwa ajili yake.

“Katika mazingira haya, Tume hiyo imeshindwa kabisa kutekeleza majukumu ya kuhakiki watumishi wa umma katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu.

“…tatizo lingine ambalo limechangia kuwepo au kuongezeka kwa watumishi hewa ni kutokuwepo kwa mfumo mmoja wa rasilmali watu unaojumuisha na kuunganisha mifumo mingine yote.

“Kwa mfano, kwa utaratibu wa sasa, mfumo wa kusajili uzazi na vifo uliopo chini ya RITA haujaunganishwa na mfumo wa utumishi wa umma wala na mifumo ya hifadhi ya jamii kama vile NSSF, LAPF, PSPF,” alisema.

Mollel, alisema si mara ya kwanza kwa Serikali kufanya uhakiki wa watumishi wa umma ili kuondoa watumishi hewa.

Alisema mwaka 1993 Serikali ilisimamisha kwa muda utaratibu wa kulipa mishahara ya watumishi wa umma kwa kuipitishia kwenye akaunti zao benki na badala yake Serikali ilihakiki kwa kuwalipa mishahara kupitia dirishani.

“Yaani malipo ya moja kwa moja kwa watumishi husika. Watumishi ambao hawakujitokeza kuchukua mishahara yao dirishani walihesabika kuwa ni ‘watumishi hewa’ na majina yao yaliondolewa katika ‘payroll.’ Hata hivyo uhakiki huo ulishindwa kuondoa tatizo la ‘watumishi hewa’ ambalo liliendelea kuwa sugu katika utumishi wa umma nchini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles