27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mishahara mipya yakwamisha bajeti

Na FREDY AZZAH -DODOMA

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2017/18 ni pamoja na kupunguzwa kazi kwa wafanyakazi wa migodi na kutoongezeka mishahara kwa wafanyakazi kama ilivyotarajiwa.

Dk. Mpango aliyasema hayo jana bungeni jijini hapa, alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa na mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya mwaka 2019/20.

“Changamoto kubwa zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2017/18 ni pamoja na ugumu wa kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara waliopo kwenye sekta isiyo rasmi, kwa kuwa hawana sehemu rasmi na za kudumu za kufanyia biashara na hawatunzi kumbukumbu.

“Sababu nyingine ni kutofikiwa kwa lengo la kodi zitokanazo na ajira kwa maana ya ‘payee’ kulikosababishwa na kutofikiwa kwa malengo ya ajira mpya na kutoongezeka kwa mishahara kwa wafanyakazi kama ilivyokuwa imetarajiwa.

“Vilevile kodi hizi zimeathirika kutokana na kupunguzwa kazi kwa wafanyakazi kwenye migodi ya madini kufuatia kupungua kwa shughuli za uchimbaji madini kwa baadhi ya migodi.

“Sababu ya tatu ni kushuka kwa biashara za kimataifa kulikosababisha kutofikia malengo ya uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kama ilivyokuwa imetarajiwa.

“Sababu nyingine ni upungufu wa wafanyakazi na vitendea kazi ndani ya Mamlaka ya Mapato nchini kulikopunguza ufanisi wa utendaji kazi wa mamlaka hiyo na sababu nyingine ni kupungua kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo,” alisema Dk. Mpango.

Katika hatua nyingine, Dk. Mpango alisema mapato ya ndani yanakadiriwa kuongezeka hadi Sh trilioni 23.20 mwaka 2019/20, kutoka Sh trilioni 20.89 mwaka 2018/19.

Alisema misaada na mikopo nafuu, inatarajiwa kupungua kutoka Sh trilioni 3.38 kwa mwaka 2019/20, hadi Sh trilioni 3.28 mwaka 2021/22.

“Mikopo kutoka nje na ndani inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 6.93 mwaka 2019/20 na shilingi trilioni 6.76 mwaka 2021/22,” alisema Dk. Mpango.

Kuhusu matumizi ya Serikali, Dk. Mpango alisema yanakadiriwa kukua hadi Sh trilioni 33.50 mwaka 2019/20 kutoka Sh trilioni 32.47 mwaka 2018/19.

“Kwa mwaka 2019/20 mishahara inakadiriwa kuwa shilingi trilioni 7.55 na inakadiriwa kuongezeka hadi Sh trilioni 8.42 mwaka 2021/22.

“Malipo ya riba na mtaji kwa deni la ndani na nje yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 8.62 mwaka 2019/20 na kuongezeka hadi shilingi trilioni 8.62 mwaka 2021/22,” alisema Dk. Mpango.

Alisema kiasi cha kulipia bidhaa, huduma na ruzuku kinakadiriwa kuwa Sh trilioni 4.93 mwaka 2019/20 na kuongezeka hadi Sh trilioni 5.16 mwaka 2021/22.

“Matumizi ya maendeleo yanakadiriwa kuwa Sh trilioni 12.38 mwaka 2019/20 na kuongezeka hadi Sh trilioni 13.55 mwaka 2021/22/,” alisema Dk. Mpango.

VIPAUMBELE

Miongoni mwa maeneo ya vipaumbele ya mpango huo, alisema ni ujenzi wa viwanja vya kukuza uchumi, ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji na kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

Akielezea dira ya mpango huo, Dk. Mpango alisema maeneo hayo yamezingatia mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016/17-2020/21.

Alisema ujenzi wa viwanda ni pamoja na uanzishwaji wa kanda maalumu za kiuchumi za Ruvuma, Mtwara, Kigoma na Bagamoyo na kukuza kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi.

Maeneo mengine yaliyotajwa na waziri huyo ni maliasili na madini, misitu na wanyamapori, utalii, biashara na masoko.

“Aidha kwa kuzingatia umuhimu wa pekee wa sekta ya kilimo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na ustawi wa wananchi, Serikali itaweka msukumo zaidi katika uendelezaji wa sekta hii, uboreshaji wa masoko ya bidhaa za kilimo na uimarishaji wa bei za mazao,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji, Dk. Mpango alisema kipaumbele kitatolewa kwa miradi ya nishati kama ujenzi wa mtambo wa kufua umeme katika Mto Rufiji, ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge na usafiri wa anga.

“Aidha maeneo mengine yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara, madaraja, bandari, usafiri wa majini, teknolojia ya habari na mawasiliano, ardhi na maeneo ya uwekezaji, biashara, huduma za fedha, ushirikiano wa kikanda na kimataifa,” alisema.

Wakati huo huo, Dk. Mpango alisema hadi kufikia Juni mwaka huu deni la taifa lilikuwa limefikia Dola za Marekani bilioni 27.77  ikilinganishwa na dola bilioni 25.35 kwa kipindi kama hicho mwaka 2017.

“Kwahiyo, matokeo ya deni hilo yameonesha lipo chini ya kiwango cha hatari na bado ni himilivu.

“Kuhusu akiba ya fedha za kigeni, zimefikia Dola za Marekani bilioni 5.48 mwishoni mwa Juni na kuhusu mfumuko wa bei, unaendelea kushuka na kufikia asilimia 5,” alisema.

KAMATI YA BUNGE

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene alisema kamati yake inaishauri Serikali kupunguza kukopa kwenye vyanzo vya ndani na vyanzo vya biashara.

Simbachawene aliyasema hayo wakati akisoma maoni ya kamati yake bungeni jana kuhusu mpango huo wa maendeleo ya taifa na mwongozo wa kutayarisha mpango wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/20.

“Kamati inaendelea kuishauri Serikali ipunguze kukopa kwenye mikopo ya masharti ya kibiashara ambayo ina riba kubwa na kwenye vyanzo vya ndani.

“Hatua hii itasaidia kupunguza mzigo wa ugharamiaji wa mikopo hiyo kupitia ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kudumaza ushindani na ukopeshaji kwa sekta binafsi,” alisema Simbachawene.

KAMBI YA UPINZANI

Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee, alisema Serikali inatakiwa kutoa maelezo juu ya zinapotoka fedha za kugharamia mradi wa reli ya standard gauge.

“Septemba 20, Jarida la Expogroup liliripoti kuwa Tanzania imepata mkopo wa Dola za Marekani bilioni 14 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 3 kutoka Benki ya Standard Charterd kwa ajili ya kugharamia kipande cha reli kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora Dodoma.

“Habari hiyo ni tofauti na maelezo ya rais kuwa tunajenga reli ya kati kwa fedha zetu wenyewe ila kwa kuwa jarida hilo limemnukuu Waziri wa Fedha, ni vema akaeleza Bunge ugharamiaji wa mradi huo ukoje,” alisema Mdee.

Pia Mdee alihoji ni kwanini reli hiyo inaanza kwenda Mwanza hadi Rusumo badala ya kwenda Tabora hadi DRC ambako kuna fursa za kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles