31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

EU yatoa tamko zito kwa Tanzania

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

UMOJA wa Ulaya (EU) umetoa taarifa rasmi inayoeleza kwa kina sababu za kuitwa kwa balozi wake mjini Brussels nchini Ubelgiji.

Umesema ni hatua muhimu ya kuangalia upya uhusiano wake na Tanzania kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Taarifa yake iliyotolewa na kuwekwa rasmi katika tovuti ya umoja huo nchini, inaeleza kuondoka kwa balozi huyo, Roeland Van De Geer mwishoni mwa wiki iliyopita ni hatua muhimu katika kuangalia upya uhusiano huo.

“Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya Tanzania, Balozi Roeland Van de Geer ameitwa mjini Brussels kwa ajili ya majadiliano ya kina.

“Kwa sasa naibu wake, Charles Stuart ataendelea kushika nafasi ya msimamizi wa masuala yote ya umoja huo kwa kipindi hiki.

“Umoja wa Ulaya kwa sasa unasikitishwa na hali ya ukandamizwaji wa haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania, na kwamba kwa sasa uongozi unazungumza na balozi huyo mjini Brussels kufanya mapitio ya tathmini kwa kina kuhusu uhusiano wa nchi wanachama wa umoja huu na Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa taarifa hiyo kuwekwa rasmi katika mtandao wa umoja huo tangu zilipoanza kuibuka taarifa kuhusu balozi huyo kufukuzwa nchini Novemba 2, mwaka huu zikieleza kuwa hakutakiwa kuendelea kuwepo katika ardhi ya Tanzania baada ya Novemba 3, mwaka huu.

Taarifa hiyo ilisahihishwa na ofisa mawasiliano wa umoja huo kupitia tovuti hiyo, akieleza usahihi ni kwamba ameitwa mjini Brussels kwa majadiliano kuhusu hali ya baadaye ya uhusiano wa umoja huo na Tanzania.

Umoja wa Ulaya kwa sasa unajumuisha nchi wanachama 28 ambazo zimekuwa zikiwakilishwa na mabalozi walioko chini ya umoja huo sehemu mbalimbali duniani, na zimekuwa sehemu ya wadau wanaochangia maendeleo katika nchi masikini na zinazoinuka kiuchumi.

Taarifa hiyo ya msimamo wa EU imetolewa siku chache baada ya kusambaa kwa taarifa kwamba balozi huyo alitakiwa kuondoka nchini kufikia Jumamosi Novemba 3 kwa amri ya Serikali.

Taarifa za awali zilieleza kutokana na amri hiyo, balozi huyo aliondoka Novemba 3 saa 5:55 usiku kwa ndege ya Shirika la KLM kupitia Amsterdam, Uholanzi.

Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, ilisisitiza haikumfukuza balozi huyo na kwamba hatua hiyo ilichukuliwa baada ya majadiliano ya pamoja na mamlaka kutoka pande zote mbili.

Balozi Mahiga alikaririwa akisema mjumbe huyo aliitwa makao makuu ya EU na kwamba Serikali ilijadili suala hilo.

Kwamba huenda amepangiwa kazi nyingine au majukumu mengine kwa ajili yake na kwamba hakufukuzwa.

KUKOSOA SERA NA MWENENDO WA SERIKALI

Kabla ya taarifa hizo, Balozi Roeland amekuwa akitajwa kuwa mtu ambaye amekuwa akieleza wazi misimamo yake.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, amekuwa mstari wa mbele katika kukosoa sera na mwenendo wa Serikali ya Rais John Magufuli hasa kuhusu suala la uhuru na haki za raia.

Februari mwaka huu, Umoja wa Ulaya ulijitokeza hadharani na kutoa msimamo wao katika kile walichokiita ‘tishio la misingi ya demokrasia na haki za binadamu kwa Watanzania’ baada ya kupigwa risasi na kuuawa kwa mwanafunzi Aqwilina Aqwilin aliyekuwa akisoma katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),  Dar es Salaam.

Umoja huo pia uliwahi kutoa tamko la kulaani suala la kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alipokuwa akitokea bungeni mwaka mmoja iliopita na hatua ya kupotea kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi aliyekuwa Kibiti, Azory Gwanda.

KAMPENI YA KUWASAKA MASHOGA

Hata hivyo, hatua ya sasa ya kuondoka kwake nchini inahusishwa pia na kampeni kuhusu operesheni ya kuwasaka na kuwachukulia hatua wapenzi wa jinsia moja iliyoidhinishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, iliyokuwa imetarajiwa kuanza rasmi juzi.

Katika kampeni hiyo, Makonda aliunda kamati maalumu ya watu 17 inayohakikisha watu wanaofanya biashara chafu za ngono na mapenzi ya jinsia moja kwa wanaume, yaani ushoga wanachukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo siku moja kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa kampeni hiyo na siku moja baada ya kuondoka kwa Balozi Roeland nchini, Serikali ilisema itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa inayohusu haki za binadamu ambayo imeisaini na kuiridhia.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa Novemba 4, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilieleza kuwa imejitenga na kampeni hiyo ya kuwakamata na kushtaki mashoga inayoongozwa na Makonda.

Taarifa hiyo ilidai kampeni hiyo ni mawazo binafsi ya Makonda na si msimamo rasmi wa Serikali.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na itaendelea kuheshimu na kulinda haki hizo kama zilivyo katika katiba,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kufuatia tangazo la Makonda, taarifa zilieleza pia kuwa Serikali ya Marekani iliwaonya raia wake wanaoishi nchini ikiwataka wajihadhari kwa kuondoa au kuficha picha na lugha ambayo huenda zikakiuka sheria za Tanzania kuhusu mapenzi ya jinsia moja na kuonesha wazi picha za ngono.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles