Na Allan Vicent, TaboraÂ
Mpango wa Serikali kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya 3, umeleta neema kubwa kwa wakazi wa kijiji cha Chang’ombe kata ya Ndevelwa wilaya ya Tabora baada ya miradi ya kilimo na ufugaji iliyoanzishwa na kaya hizo kuanza kuwainua kimaisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari waliotembelea kijijini hapo jana baadhi ya wanufaika hao walisema kuwa mradi huo umebadilisha maisha yao kwa kiasi kikubwa.
Asha Yusuph (65) mkazi wa kitongoji wa Ntukila alisema kuwa fedha za TASAF anazopewa zimemsaidia kuanzisha kilimo cha mahindi na mboga mboga na kila mwaka anavuna magunia kuanzia 5 ya mahindi kwa ajili ya kuuza na kula.
Aliongeza kuwa pia alianzisha mradi wa ufugaji kuku ambao unamwezesha kupata kitoweo au fedha pale anapokuwa na uhitaji ikiwemo kununua mahitaji ya watoto wake wanaosoma shule.
‘Ninamshukuru sana Rais Magufuli kwa kutuletea mradi wa TASAF, umeniinua kimaisha, nimeweza kusomesha watoto wangu wote na mmoja yuko Chuo Kikuu cha Dar es salaam sasa hivi’, alisema Ashura.
Ilawa Ally (40) mkazi wa kitongoji cha Mabatini katika kijiji hicho alisema kuwa sh 80,000 anayopata kutoka TASAF imemsaidia kulima mahindi, maharage na karanga na kununua kuku 2 ambao wameongezeka hadi kufikia 10.
Alibainisha kuwa sehemu ya fedha anayowezeshwa huitumia kununulia mbolea kwa ajili ya shamba lake la mahindi kitu ambacho kimemwezesha kuvuna magunia 5 hadi 10 kila mwaka kutegemeana na wingi wa mvua.
“Sasa hivi watoto wangu wanakula milo 3 kwa siku, nawasomesha na kuwanunulia mahitaji mengine, TASAF imenisaidia sana kimaisha, sasa hivi nimenunua hata godoro la kulalia, nimeweka umeme wa jua katika nyumba yangu na kuanzisha mradi wa duka,” alisema.
Kwa upande wake, Khadija Ramadhani (47) mkazi wa kitongoji cha Magereza alisema kuwa fedha kidogo anazopata zimemwezesha kulima mahindi na karanga na kufuga mbuzi ambapo alianza na mbuzi 2 sasa wameongezeka hadi kufikia 9.
‘Sasa hivi nalima na nimefuga mbuzi na kuku, kwa kweli ninaishukuru sana serikali kwa kutujali sisi wanyonge na kutuwezesha kimaisha’, alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho Kidumla Mtandi alikiri kuwa miradi ya kilimo na ufugaji iliyoanzishwa na wanufaika wa TASAF kijijini hapo imewanufaisha sana kwani wana uhakika wa maisha tofauti na huko nyuma.
Alibainisha kuwa wamekuwa karibu zaidi na kaya hizo na kila wanapowezeshwa wamekuwa wakiwapa ushauri ili watumie fedha kidogo wanazopewa kwa kuanzisha miradi itakayowasaidi kujikamua kimaisha, hili limewasaidia sana.