24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kilimo cha umwagiliaji kunufaisha kaya maskini Uyui

Na Allan Vicent, Uyui

Kaya maskini zinazonufaika na mpango wa serikali wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) katika kijiji cha Kigwa B kata ya Kigwa wilayani Uyui Mkoani Tabora zimejiunga katika vikundi na kuchimba bwawa litakalowasaidia kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa mwaka mzima.

Akizungumza na vyombo vya habari vilivyotembelea kata hiyo jana kujionea maendeleo ya miradi iliyoanzishwa na kaya hizo, Kaimu Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kigwa B Ngassa Joseph alisema kuwa bwawa hilo litakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wao.

Alisema bwawa hilo lililochimbwa kupitia mradi wa TASAF wa ajira za muda mfupi (PWP) katika kitongoji cha Majengo kijiji cha Kigwa B ndani ya kata hiyo litavinufaisha jumla ya vikundi 10 vya walengwa wa mpango huo.

Alitaja shughuli zitakazofanyika kuwa ni kulima bustani za mboga mboga, nyanya na ufugaji samaki ikiwemo kilimo cha mpunga, mahindi, maharage na karanga ambapo wahusika watalima mazao hayo kwa kipindi chote cha mwaka mzima.

Mratibu Msaidizi wa TASAF wilayani humo, Humphrey Kilua alieleza kuwa bwawa hilo ni muhimu sana katika kuinua uchumi wa kaya maskini na jamii kwa ujumla, aliahidi kuwa serikali ya kijiji itaendelea kuwapa ushirikiano wote.

“Kilimo cha umwagiliaji ni mhimili mkubwa wa uchumi endelevu kwani kitawezesha wananchi kulima wakati wote pasipo kujali msimu wa masika au kiangazi, hivyo kuwa na uhakika wa chakula na kukimbia umaskini,” alisema.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji hicho, Charles Simwanza, alipongeza serikali kwa kuanzisha mpango huo wa kunusuru kaya maskini kwani umewezesha jumla ya kaya maskini 135 kunufaika.

Alibainisha kuwa anajisikia faraja sana kutokuwa na wananchi ombaomba katika kijiji chake, alizitaka kaya zote zilizoingizwa katika mpango huo kutumia vizuri fedha wanazopewa na kujikita zaidi katika kilimo cha umwagiliaji.

Baadhi ya wanavikundi wanaowezeshwa na TASAF katika kijiji hicho Joha Ngayaula (68) na Esta Luhende (53) wakazi wa kitongoji cha Magiri Juu walisema kuwa maisha yao sasa yamebadilika tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Walibainisha kuwa fedha kidogo wanayopewa wataitumia kuboresha miradi yao ya kuku, mbuzi, ng’ombe na kilimo ikiwemo kulima bustani za mboga mboga na nyanya.    

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles