Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Hospitali ya Miracolo iliyopo Tabata Sanene inasherehekea Sikukuu ya Wapendanao kwa kutoa huduma ya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno bure.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk. Anna – pendo Deogratias, amesema huduma hizo zilizoanza kutolewa Februari Mosi zitaendelea hadi Februari 28 na kuwataka wananchi wajitokeze kuchangamkia fursa hiyo.
Dk. Anna amesema mwitikio ni mkubwa na kwamba wamebaini watu wengi wana matatizo ya kinywa na meno lakini hawajui.
“Wengi wanakimbilia kung’oa kumbe meno mengine sio ya kung’oa, yanaweza yakatibiwa yakazibwa,” amesema Dk. Anna.
Katika hatua nyingine hospitali hiyo pia imetoa msaada wa vifaa mbalimbali katika Gereza la Segerea kama sehemu ya kusherehekea Sikukuu ya Wapendanao.
Msaada huo ni pamoja na magodoro, sabuni na pampasi ambapo Dk. Anna amesema waliamua kuwasaidia watu walioko kwenye mazingira magumu kwa kuwasambazia upendo.
“Kuna watu wako kwenye mazingira magumu kama walioko gerezani wanatamani kupendwa, mbali ya kuwa na mpendwa wako uliyenaye karibu jaribu kufikiria na jamii nyingine…tuwasaidie wenzetu walioko kwenye mazingira magumu kwa kuwasambazia upendo,” amesema.
Amesema hospitali hiyo pia inatoa huduma mbalimbali za madaktari bingwa kama vile wa watoto, magonjwa ya ndani kama vile moyo, kisukari, presha, mfumo mzima wa chakula, magonjwa ya kina mama na vipimo vyote vya maabara.