MOHAMED KASSSARA-DAR ES SALAAM
KOCHA Fred Minziro amefichua sababu zilizomfanya kutoonekana kwenye benchi la timu ya Singida United, katika michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ambayo yote ilichezea vichapo.
Singida ilianza kuchapwa bao 1-0 na Mwadui FC, katika mchezo wa kwanza kabla ya juzi kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Namungo, mchezo uliochezwa Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
Matokeo hayo yaliibuka maswali wapi alipo Minziro ambaye alikabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita.
Akizungumza na MTANZANIA jana , Minziro alisema ameamua kujiweka kando baada ya uongozi wa klabu hiyo kutojali mambo ya msingi, ikiwamo kumzungusha kuhusu mkataba wa kazi.
“Baada ya kunizungusha kwa muda mrefu waliniletea mkataba lakini haukuwa maslahi mazuri hivyo nikaamua kujiweka kando.
“Nilipousoma niliona hauna faida kwangu kwani hauna bonsai(marupurupu), kifupi ni mkataba wa kisela, hivyo nikaona hakuna sababu ya kuusaini.
“Kwa sasa siko na timu hiyo hivyo siwezi kuzungumzia kilichotokea kwenye michezo hiyo miwili, uongozi hawakuthamini mchango wangu,”alisema Minziro
Minziro alifichua sababu nyingine ilimfanya kujiengua kwenye timu hiyo ni kitendo cha uongozi kujichukulia uamuzi wa kufanya usajili wa wachezaji bila kumshirikisha.