23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

MIMBA TATIZO KWA MTOTO WA KIKE

Na ASHA BANI-NANYUMBU

MATATIZO ya mimba za utotoni kwa wanafunzi wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara yameshika kasi.

MTANZANIA iliyokuwa wilayani humo, ilishuhudia kundi la wanafunzi walioambatana wakitoka shule ya Sekondari Sengenya kuelekea Zahanati ya Sengenya, kwa ajili ya kupima mimba, jambo linalotoa taswira ya ukubwa wa tatizo  hilo.

Kwa mujibu wa mlezi ‘Matron’ wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Mwanaid Simba, aliliambia gazeti hili kuwa anawapeleka wanafunzi hao kupimwa mimba na huo ni utaratibu  wa mara kwa mara kutokana na ukubwa wa tatizo lenyewe.

Baadhi ya wanafunzi walipohojiwa, walisema wengi wanapata mimba kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na kufanya kushindwa kutimiza ndoto zao.

 Wanafunzi waeleza sababu

Riziki Hokororo mwanafunzi wa kidato cha nne, amesema moja ya sababu ni tamaa, umasikini, vishawishi vya hapa na pale pamoja na utandawazi.

Alisema wao wameanza kuishi shuleni wakiwa kidato cha nne, lakini huko nyuma walikuwa wakiishi nyumbani kwao ambapo ni umbali mrefu hadi kufika shuleni.

Alisema umbali mrefu wa takribani km nane  kutoka Mangaka hadi Sengenya, njiani wanakutana na vishawishi vingi ikiwa ni pamoja na kuomba  lifti za bodaboda na kupakiwa na kisha kudanganywa kwa kuwa wanapata tabu ni rahisi kukubali kufanya mapenzi na madereva wa bodaboda.

Husna Hamis mwanafunzi wa kidato cha nne , anasema unyago unachangia kuwaingiza katika vishawishi vya ngono licha ya kwamba wanachezwa wakiwa na umri mdogo.

Alisema mara nyingi wanapofanyiwa unyago, huwa wanafundishwa jinsi ya kumtunza mume na ‘kukatika viuno’, hivyo wanaamua kutumia mafunzo hayo kwa kuyafanya kwa vitendo pia.

“Sisi katika unyago tunafundishwa jinsi ya kulea na kutunza familia hata ‘kukatikakatika’ basi tunapotoka kwenye mafunzo hayo, tunayafanya kwa vitendo kwa hivyo ni rahisi kupata mimba na mafunzo yake hayatoki kichwani, mimi hadi leo nakumbuka nilifundishwa kitu gani,” alisema Husna.

Mwanafunzi wa kidato cha pili, Siza Halifa, kutoka Shule ya Sekondari Likokona ambaye Aprili mwaka huu alibainika kuwa ameshika mimba, alisema imesababishwa na umasikini wa familia yake.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa huyo lakini binti alikana kupewa mimba na kijana huyo na hatimaye kuachiwa.

Takwimu zinaonyesha kuwa wanafunzi 23 wa shule za sekondari wamekatisha masomo kutokana na sababu za kupata mimba wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

Ofisa Elimu wa Sekondari wa Wilaya hiyo, Lwoga Musijaki, aliliambia gazeti hili kuwa wanafunzi hao ni wa kutoka shule mbalimbali, wamekatisha masomo kutokana na sababu za kupata mimba wakiwa shuleni.

Alisema kwa mwaka 2016, jumla ya wanafunzi 17 na mwaka 2017 hadi kufikia jana, jumla ya wanafunzi sita wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kupata mimba.

Alizitaja baadhi ya shule walizotoka wanafunzi hao kwa mwaka 2016 na 2017,  kuwa ni pamoja na shule ya Chipuputa (1), Mangaka (4), Michiga (1), Mikangaula (1)Nandete (1). Shule nyingine ni pamoja na Nangomba (2), Napacho (4) na Sengenya (3).

Musijaki alisema kuna sababu mbalimbali zinazomfanya mwanafunzi  kupata mimba, ikiwa ni pamoja na tamaa ya mwanafunzi mwenyewe, baadhi ya wazazi kutokuwajibika kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi na changamoto ya miundombinu ambayo si rafiki kwao.

“Hili pia linakuwa ni tatizo, utakuta mwanafunzi anakaa mbali na maeneo ya shule hivyo huwalazimu wazazi kuwapangia watoto wao nyumba maeneo ya karibu na shule, lakini wanashindwa kufuatilia mienendo ya watoto hao, hatimaye kujiingiza katika makundi ya wahuni na hata kupata mimba wakiwa shuleni na kukatisha ndoto zao,” alisema Musijaki.

Akizungumzia kuhusu mila hizo ambazo baadhi ya wanafunzi wameeleza kuchangia kwao kujiingiza katika vitendo vya ngono, Ofisa Utamaduni wa Wilaya, Ahamad Tabia, alisema unyago upo toka vizazi na vizazi lakini tofauti iliyopo ni katika umri.

Alisema zamani walikuwa wakifundishwa wakiwa wanajitambua na wakifundishwa jinsi ya kumtunza mume, akitoka anaolewa moja kwa moja kwa kuwa hata umri wake unamruhusu kufanya hivyo. Lakini unyago wa sasa wanafundishwa wakiwa katika umri mdogo ni tatizo.

“Unyago wa sasa mambo yaleyale wanayofundishwa wakubwa na wakitoka wanarudia kufanya ndio hayo hayo wanafundishwa watoto, hii ndio changamoto iliyopo kwa sasa ni tatizo kweli,” alisema Tabia.

Aliongeza kuwa Serikali kwa sasa wamekuwa wakali kwa maana hata yeye anatoa vibali kulingana na mwezi ambao pia wanafunzi wanakuwa likizo, ingawa alisisitiza ni vigumu kulizuia kwa asilimia kubwa suala hilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hamis Dambaya, alisema wanaendelea na kupambana na changamoto mbalimbali zinazomfanya mtoto wa kike ashindwe kusoma.

Alisema kwa Nanyumbu, Serikali katika usimamizi wake na viongozi wengine wamejitahidi kuhakikisha wanajenga mabweni ili kuepuka mwanafunzi kutembea umbali mrefu na vishawishi wanavyoweza kuvipata wakiwa njiani.

“Tatizo pia umbali wa wanafunzi na  maeneo ya shule ambapo wazazi wanawapangia nyumba karibu na shule, lakini hawana usimamizi wanakuwa huru kufanya kitu chochote, hilo nalo linachangia mimba.

“Rais Magufuli ameshasema mtoto akipata mimba atakaa nyumbani aendelee kunyonyesha mtoto wake na hapa  ni hivyo hivyo kama kaona kujiingiza katika vitendo hivyo ni bora zaidi, basi akae nyumbani alee mtoto wake lakini lengo la Serikali wasome,” alisema Dambaya.

Kauli ya Mbunge

Kwa upande wake Mbunge wa Nanyumbu, Dua Nkurua (CCM), aliliambia gazeti hili kuwa matatizo ya watoto wa kike yanachangiwa na wazazi kutokuwajibika na kuona kama kawaida.

Mapema mwaka huu baadhi ya wabunge walitoa maoni yao tofauti tofauti kuhusiana na hatua ya Serikali kuweka sheria ya kuwafukuza shule wanafunzi wanaopewa mimba na kutaka Serikali ibadili kifungu hicho cha sheria.

Katika Bunge la Februari mwaka huu, Mbunge wa Urambo, Margareth Sitta (CCM), aliuliza swali la nyongeza kuhusu mimba za utotoni akikazia swali kama hilo lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Vullu.

Alisema wanaopata mimba waendelee na masomo yao, kwani wanajisikia vibaya kama wanawake kukatazwa wanafunzi kuendelea na shule pindi wanapojifungua.

Alisema: “Tanzania Bara pekee ndio ambayo hairuhusu hilo, kwani Zanzibar mtoto akipata ujauzito wanaruhusu kuendelea na masomo, nchi ya Zambia, Kenya na kwanini isiwe Tanzania na imebaki peke yake,” alihoji mbunge huyo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya, alisema suala hilo linatakiwa kuangalia na kutekelezwa kwa pamoja na ndio maana wameamua kuwashirikisha na wabunge.

Suala hilo lilikuwa na mjadala mpana katika mkutano wa saba wa Bunge la 11 wakati wa kupitisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha wa 2017 -2018.

Hata hivyo, Sheria ya mwaka 1971 ambayo pia inawazuia watoto wasifanye mapenzi wakiwa katika umri mdogo, waliieleza kuhitajika kufanyiwa pia marekebisho kwa kuwa inamnyima haki mtoto wa kike kurudi shule.

Asasi mbalimbali zisizo za Kiserikali ikiwemo Hakielimu, Mtandao wa Elimu nchini (TENMET) na nyinginezo tayari zimejitokeza kuonesha nia ya dhati kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki sawa, ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali kuliangalia kwa ukaribu njia mbadala itakayoweza kumsaidia mtoto wa kike aweze kusoma na kutimiza ndoto zake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles