24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

WATANZANIA WASHAURIWA KUBORESHA AFYA ZAO

Na BENJAMIN MASESE – MISUNGWI

WATANZANIA wameshauriwa kujenga utamaduni wa kula mlo kamili bila kusahau mayai ili kuondokana na ukosefu wa virutubisho mwilini.

Ushauri huo umetolewa juzi na Ofisa Mradi wa shamba la ufugaji wa kuku la Prime Farm Ltd, Florian Kivamba, mbele ya Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour, alipotembelea eneo la mradi wa uwekezaji Idetemya.

Kivamba alimweleza Amour kwamba mradi huo ulianzishwa mwaka jana na mwekezaji Nishat Alibhai Mulji, chini ya usimamizi wa wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi baada ya kuwapo na changamoto ya upatikanaji wa mayai kwa wananchi.

Alisema Watanzania, hususan wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, hawana budi kuzingatia kula mayai ambayo awali upatikanaji wake ulikuwa mgumu, huku akisisitiza kwamba mwili wa binadamu unahitaji virutubisho vya aina nyingi ili kuwa na afya.

Kivamba alisema mwili wa binadamu unapokosa madini fulani na virutubisho, unakosa nguvu ya kujikinga na maradhi mbalimbali na aliwaomba kuzingatia mlo kamili ili kuokoa gharama za matibabu.

“Wazo la ufugaji wa kuku wa mayai ya kisasa lilitokana na changamoto zilizopo za upatikanaji wa mayai ikiwa ni sehemu ya kuwapatia urahisi wananchi kula mayai ili kupata virutubisho vya protini.

“Kwa siku moja tunazalisha mayai 1,500 sawa na ‘trei’ 500 ambazo zinaingia sokoni, tumetoa ajira kwa vijana 15 ambao wanashughulika na masuala yote kuanzia kiwandani hadi kusambaza bidhaa sokoni.

“Hadi sasa mradi umegharimu Sh milioni 400, ikiwa ni gharama za kununua ardhi, ujenzi wa mabanda, usimikaji wa mashine za kusaga na kuchanganya chakula, uchimbaji wa visima, dawa na fedha za uendeshaji wa mradi,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuanzishwa kwa uwekezaji wa shamba hilo la kuku kutakuza uchumi wa wakazi wa Mkoa wa Mwanza na kuongeza soko la ajira kwa vijana na biashara.

Kwa upande wake, Amour, alisema Serikali ya awamu ya tano ni ya viwanda, hivyo kuanzishwa kwa shamba hilo ni sehemu ya kutimiza sera ya Tanzania ya viwanda.

Aliwataka vijana walioajiriwa hapo kuwa waaminifu na kutanguliza uzalendo kwanza badala ya masilahi binafsi.

Pia aliushauri uongozi wa shamba hilo kuendeleza  uwekezaji huo katika maeneo mengine ya mkoa ili kurahisisha upatikani wa mayai hayo.

Wakati huo huo, aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kufanikisha kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 16 kwa kiwango cha changarawe, ambayo imeunganisha mawasiliano kati ya vijiji vya Mondo, Mwaniko, Ndinga, Lubuga na vijiji jirani vilivyopo kati ya Mkoa wa Mwanza na Shinyanga.

Kaimu Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Jacob Uswege, alimweleza Amour kwamba barabara hiyo imetengenezwa kwa gharama ya Sh milioni 91.97 ambazo zimetokana na Mfuko wa Barabara na kuongeza wanafikiria kujenga kwa kiwango cha lami.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles