Na, ALOYCE NDELEIO
SERIKALI ya Awamu ya Tano ilipoibua suala la makinikia na kuzibana kampuni zilizokuwa zinamiliki makinikia hivyo wakiwa ni wawekezaji katika baadhi ya migodi zimekuwapo hoja nyingi lakini hitimisho likaelezwa kuwa wawekezaji hao wamekubali kulipa kasoro walizozisababisha.
Hali hiyo kwa wanajamii wengine ambao hawapo katika mazingira yaliyo na rasilimali hizo si ajabu kwamba ilikuwa inawakanganya kwa kuibuka baadhi ya maswali yanayohitaji majibu.
Baadhi ya maswali; Ni kitu gani muhimu kuhusu shughuli za madini? Na ni kitu gani nchi inayotegemea sekta ya madini inanufaika nacho katika kukua kwa uchumi?
Majibu yake ni kwamba sekta hai ya madini kama ilivyo sekta nyingine ile inatakiwa kutoa fursa muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi. Hata hivyo kuna mambo mengine yanayotofautisha madini na sekta nyingine za uzalishaji chini ya ardhi kama mafuta au gesi au sekta nyingine za uzalishaji viwandani au utalii.
Kile ambacho kinapatikana chini ya ardhi ni amana ya Taifa. Kwa miaka mingi uzalishaji wa maliasili umekuwa ukichukuliwa tofauti kulingana na makundi yanayounda zawadi asilia.
Nchi nyingi zinachukulia chuma na madini kuwa ni amana zilizo mikononi mwa umma kwa ujumla. Hali hiyo imesababisha ama Serikali kumiliki                                                                                                                       kampuni za madini au katika mazingira ambayo ni zaidi ya kawaida kujumuishwa katika leseni zinazotolewa kwa kampuni za madini, sekta za usimamizi na masuala ya fedha, ikiwamo kodi, ada na uwekezaji katika kusaidia miundombinu.
Kwa uhalisia wake sekta ya madini kama zilivyo sekta za mafuta na gesi zinakuwa ni alama inayoweza kuleta matokeo katika mazingira, jamii na uchumi.
Hata hivyo uasilia huo unapotumika katika eneo au kanda matokeo au usimamizi mbovu katika mazingira au mambo yanayohusiana na jamiii kunaweza kuleta madhara hasi kiuchumi kwa eneo kubwa la nchi.
Hivyo unakuwapo umuhimu wa kuzipima faida dhidi ya athari na gharama zinazozunguka uendeshaji wa sekta na kudhibiti madhara yoyote ambayo ni hasi.
Madini ni sekta ambayo ni kipaumbele kwa uwekezaji kutoka nje. Nchi nyingi zinazoendelea hupata athari kubwa kutoka kwa wawekezaji wa nje.
Uendeshaji wa madini katika nchi hizi ambako kunakuwapo uuzaji wa nje na malipo ya mapato yakiwa katika dola ndio za kwanza kuwasilisha madai ya athari zinazopata kutokana na kanuni za wawekezaji.
Katika hatua za mwanzo Serikali hujikuta zenyewe hazijajitayarisha wakati wa kujadiliana mikataba na wawekezaji wa madini.
Matokeo yake wawekezaji wanaweza kujikuta wao wenyewe wakikabiliana na matatizo maalumu katika kushirikiana na mawakala wa Serikali na washirika wengine wa ndani.
Madini ni chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali. Sekta hii muhimu huwa inazalisha mapato makubwa ya fedha zinazotumiwa na sekta nyingine.
Kwa kuwa miongoni mwa nchi nyingi zinazoendelea sehemu kubwa za mapato ya fedha yanatokana na mauzo ya nje, sekta za kuuza madini nje inatoa sehemu kubwa zaidi ya mapato ya Serikali.
Katika baadhi ya nchi zilizo na madini asilimia 25 au 30 ya mapato yake ya fedha yanategemea moja kwa moja sekta ya madini.
Kuhusu iwapo uchimbaji wa madini unaweza kuinufaisha au kuikwamisha nchi inayoendelea katika kiu yake ya kukua kwa uchumi na ustawi, hilo limekuwa likisababisha kuibuka kwa tafiti nyingi.
Baadhi ya wachambuzi wanapendelea nchi kutumia sekta ya madini kuboresha ukuaji wake wa uchumi na hivyo kuona uchimbaji wa madini ni mzuri.  Kimsingi walio wengi wanaangalia upande ambako nchi zimekuwa zikinufaika na hakuna migogoro ambayo chimbuko lake linakuwa ni madini.
Wengine wanapigia debe kuachana na uchimbaji wa madini wakiwa na dhana kuwa uchimbaji wa madini ni mbaya. Hawa wanaangalia upande wa nchi au maeneo ambayo yamekumbana na tatizo la  migogoro, ikiwamo vita vya wenyewe kwa wenyewe na madini yakiwa yametumika kupata fedha zinazochochea migogoro ya aina hiyo.
Mifano ya hali hiyo ni katika nchi za Sierra Leone na Angola ambako kwa kuangalia madhara waliyokumbana nayo raia, thamani ya madini kuwapo katika nchi hizo kuligeuka kuwa laana badala ya neema.
Katika mazingira hayo ni dhahiri pale ambapo zinafanyika jitihada za kuwa na mikataba sahihi kunamaanisha kuepusha taswira hasi na kuiongezea thamani sekta ya madini.