26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

CHADEMA YAMKANA MGOMBEA UBUNGE

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limemkana mgombea ubunge katika Jimbo la Singida Kaskazini, ambaye ametangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Jana, NEC ilitoa orodha ya wanachama 15 wa vyama vya siasa walioteuliwa kugombea ubunge katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido.

Katika orodha ya walioteuliwa na NEC kugombea ubunge katika Jimbo la Singida Kaskazini, limo jina la David Djumbe aliyetajwa kupitia Chadema.

Lakini chama hicho jana kilitoa taarifa kwa umma kuwa hakijateua mgombea yeyote kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo hilo.

Uchaguzi wa jimbo hilo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wake, Lazaro Nyalandu kutangaza kujivua uanachama wa CCM Oktoba 30 na kujiunga na Chadema.

Wagombea wengine walioteuliwa na NEC kugombea jimbo hilo vyama vyao kwenye mabano ni Omari Sombi (AFP), Dalphina Mlelwa (CUF), Monko Joseph (CCM), Aloyce Nduguta (ADA- TADEA) na Mchungaji Yohana Labisu (CCK).

Walioteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Longido ni Kisiongo Mayasek Olokuya (CUF), Francis Ringo (CCK), Dk. Steven Kiruswa (CCM), Mgina Mustafa (AFP), Godwin Sarakikya (ADA TADEA), Feruziy Furuziyson (NRA), Ngilisho Paul (Demokrasia Makini), Simon Bayo (SAU) na Robert Lukumy (TLP).

 

TAARIFA YA CHADEMA

Chadema kupitia Msemaji wake, Tumaini Makene jana ilitoa taarifa kwa umma kuwa hawajamteua mgombea kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo la Singida Kaskazini licha ya NEC kutangaza kumteua mgombea wa chama hicho.

“Mkurugenzi wa NEC (Ramadhani Kailima) amesikika asubuhi (jana) wakati akihojiwa na Radio Clouds kwenye kipindi cha Power Breakfast, akisema Chadema kimechukua fomu za kugombea ubunge katika uchaguzi wa marudio Jimbo la Singida Kaskazini.

“Kupitia taarifa hii ya awali, tungependa vyombo vya habari na umma kwa ujumla ujue kuwa Chadema hakijateua mgombea kuwania nafasi ya ubunge katika uchaguzi huo wa marudio.

“Mkurugenzi wa NEC atambue kuwa suala la kugombea nafasi ya ubunge kwa mchakato wa ndani ya Chadema linasimamiwa na Kamati Kuu ya chama, hivyo yeye hana mamlaka wala hawezi kuwa msemaji wa suala hilo katika hatua ya sasa.

“Tunafuatilia kupata taarifa za kina kuhusu msingi wa kauli ya Kailima, kisha tutatoa taarifa kamili katika hatua ya baadaye,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), aliandika katika mitandao ya kijamii kuwa chama hicho hakijamsimamisha mgombea mahali popote katika uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Januari 13, mwakani.

“CCM wanajaribu kutafuta uhalali katika uchaguzi huu ambao upinzani umeususia, hizi ni fujo zenye mwelekeo mbaya wa siasa nchini,” alisema Lema.

 

MSIMAMO WA CUF

Kwa upande wa chama cha CUF upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ambacho ni sehemu ya Ukawa, kimesema msimamo wake uko palepale wa kutoshiriki uchaguzi huo mdogo.

Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande, aliliambia MTANZANIA kuwa kamwe hawawezi kusimamisha mgombea hadi pale NEC itakapoondoa kasoro zilizopo.

Akizungumzia kuhusu kusimamishwa mgombea wa Ukawa kwenye baadhi ya majimbo ya uchaguzi, alisema ni hujuma za baadhi ya wana CCM.

“Msimamo wetu upo palepale hatuna mpango wa kusimamisha mgombea na kama yupo, huyo wanamfahamu wao wenyewe, sisi hatumjui.

“Inawezekana kabisa CCM wametumia fursa hiyo kusimamisha mgombea ili kutuvuruga wakati sisi hatuna mpango huo hadi kieleweke.

“Kinachoshangaza mgombea anateuliwa na kamati kuu ya chama, sasa iweje chama kisimfahamu kama hakuna mchezo mchafu,” alisema Maharagande.

Kwa upande wake Abdul Kambaya ambaye ni Mkurugenzi wa Habari wa CUF upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kila jimbo wanasimamisha wagombea na kwamba wana uhakika wa kushinda.

“Kama kuna uchaguzi halafu wapinzani mnagoma kusimamisha wagombea, basi mnataka kuingia msituni. Sisi hatushirikiani na Ukawa, lakini tutahakikisha tunashiriki uchaguzi kama ulivyopangwa na tunatarajia kushinda,” alisema Kambaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles