28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mikakati nane kutekeleza bajeti

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amewasilisha bajeti ya wizara yake akiomba Bunge kuidhinisha matumizi ya Sh trilioni 11.94, huku akija na mikakati nane ya kutatua changamoto za utekelezaji wa bajeti.

Akisoma hotuba yake bungeni jana, Dk. Mpango alisema katika mwaka wa fedha wa 2018/19, walikumbana na changamoto tatu kwenye kutekeleza bajeti hiyo.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni masharti yasiyo rafiki ya mikopo katika masoko ya fedha duniani, kupungua na kutopatikana kwa wakati kwa fedha za washirika wa maendeleo katika kugharamia miradi ya maendeleo na mwamko mdogo wa kulipa kodi kwa hiari, kudai au kutoa risiti za kielektroniki.

Dk. Mpango alisema ili kukabili changamoto hizo, wizara yake itahakikisha wizara na taasisi zote za umma zinatumia mfumo wa Serikali wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato (GePG) na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kupunguza utegemezi.

Hatua nyingine ni kuboresha mfumo wa usimamizi wa mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs) ili ziweze kutumika kwa kila muamala unaofanywa.

“Uboreshaji huu utaondoa uwezekano wa kughushi risiti na kupunguza mianya ya ukwepaji wa kodi,” alisema Dk. Mpango.

Mkakati mwingine ni kudhibiti biashara ya magendo kupitia bahari, maziwa, mipaka, na njia zisizo rasmi kwa kushirikiana na taasisi za Serikali kama Wakala wa Barabara (Tanroads), Mamlaka ya Bandari (TPA), Jeshi la Polisi, Jeshi la Wanamaji na Usalama wa Taifa.

Alisema pia wataongeza jitihada za ukusanyaji wa kodi za majengo kwa kushirikisha Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Mkakati mwingine uliotajwa na Dk. Mpango ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015, kuendelea kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo kwa kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano (DCF) ili kuhakikisha fedha zilizoahidiwa zinatolewa kwa wakati.

Alisema pia wizara yake itaendelea na majadiliano na taasisi za fedha za kimataifa ili kuhakikisha fedha zinazotokana na mikopo ya kibiashara zinapatikana kwa kipindi kilichobaki. 

FEDHA ZILIZOOMBWA

Akiomba Bunge kuidhinisha fedha, Dk. Mpango alisema wizara yake na taasisi zake pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, inakadiria kutumia Sh trilioni 11.94.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh trilioni 11.21 ni kwa ajili matumizi ya kawaida na Sh bilioni 730.58 ni matumizi ya maendeleo.

Alisema matumizi ya kawaida yanajumuisha Sh bilioni 608.37 kwa ajili ya mishahara na Sh trilioni 10.60 kwa ajili ya matumizi mengineyo na matumizi ya maendeleo Sh bilioni 77.

Akichambua baadhi ya mafungu yanayoombewa fedha hizo, Dk. Mpango alisema Wizara ya Fedha na Mipango inaomba kuidhinishiwa Sh bilioni 65.71, kati yake Sh bilioni 37.92 ni mishahara na matumizi mengineyo ni Sh bilioni 27.79, miradi ya maendeleo Sh bilioni 34.76

Alisema fungu 21 Hazina, linaomba Sh trilioni 1.27, mishahara ikiwa Sh bilioni 536.52 na matumizi mengineyo Sh bilioni 736.28.

Katika fungu 22 –  deni la taifa, aliomba Sh trilioni 9.73, kati yake mishahara Sh bilioni 8.88 na matumizi mengineyo Sh trilioni 9.72 huku fungu 23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, ikiomba fedha za matumizi ya kawaida Sh bilioni 44.07 mishahara ikiwa Sh bilioni 7.03 na matumizi mengineyo Sh bilioni 37.04.

WAOKOA SH BILIONI 10

Dk. Mpango alisema kiasi cha Sh bilioni 10 kimeokolewa kutokana na uhakiki wa madai ya fedha za fidia za miradi ya Serikali, ikiwamo ya maendeleo ya miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam (DMDP), ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa na ujenzi wa kituo cha Jeshi la Majini.

Pia alisema walibaini baadhi ya halmashauri kutozingatia mwongozo na utaratibu unaotakiwa katika utekelezaji wa programu ya uboreshaji mazinigra ya miji na manispaa.

MIRADI YA KIMKAKATI

Dk. Mpango alisema kwa mwaka wa fedha 2018/2019 wizara imefanya uchambuzi wa miradi ya kimkakati 111 yenye thmani ya Sh bilioni 749.63 kutoka katika halmashauri 67 kwa ajili ya kuzingatiwa kwenye bajeti ya mwaka 2019/20.

Alisema matokeo ya uchambuzi huo ni kuwa miradi 15 ya Sh bilioni 137.38  kutoka kwenye halmashauri 12 ilikidhi vigezo na mikataba kusainiwa.


UTAKATISHAJI FEDHA 

Dk. Mpango alisema katika mwaka 2018/19 wizara kupitia Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu (FIU), imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ya udhibiti wa fedha haramu kwa kutekeleza majukumu mbalimbali.

Alitaja majukumu hayo kuwa ni pamoja na kupokea taarifa 1,305 za miamala kutoka kwa watoa taarifa na kuwasilisha taarifa za fiche 32 kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria kwa ajili ya uchunguzi.

Aidha, kupokea taarifa 5,536 zinazohusu usafirishaji fedha taslimu na hati za malipo mipakani, kuratibu na kusimamia zoezi linaloendeshwa na ESAAMLG na tathimini ya mifumo ya udhibiti wa fedha haramu (AML/CFT) kwa kuimarisha ushirikiano na FIU za nchi za Djibouti, Sudan, Ethiopia, Somalia, China (Taiwan) na Mauritius.

MISAADA NA MIKOPO

Dk. Mpango alisema katika mwaka huu wa fedha, wizara ilipanga kuratibu upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu ya Sh trilioni 2.67 kutoka kwa washirika wa maendeleo kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema hadi kufikia Aprili, misaada na mikopo ilifikia Sh trilioni 1.7, sawa na asilimia 86 ya lengo la kipindi hicho.

Dk. Mpango alisema katika mwaka huu wa fedha, wizara hiyo pia imeratibu upatikanaji wa mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara ya Sh trilioni 8.9, kati yake, Sh trilioni 3.11 ni mikopo ya nje, Sh trilioni 1.19 mikopo ya ndani na Sh trilioni 4.6 mikopo ya ndani ya kulipia hatifungani zilizoiva.

Alibainisha kuwa hadi kufikia Aprili, Sh bilioni 692.3 zilikopwa kutoka nje, Sh trilioni 3.3 zilikopwa kutoka soko la ndani zikijumuisha malipo ya dhamana za Serikali zilizoiva.

KAMATI

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mashimba Ndaki, alisema wanaipongeza Serikali katika jitihada za kusimamia biashara ya ubadilishaji fedha nchini.
Ndaki ambaye ni Mbunge wa Maswa Magharibi (CCM), alisema hatua hiyo itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama na kukabiliana na mianya ya ubadilishaji wa fedha haramu.

“Hata hivyo, endapo Serikali haitaimarisha mifumo yake, itatoa mianya ya kuwepo kwa maduka ya ubadilishaji fedha yasiyo rasmi – ‘black market’,” alisema.

MAONI YA WABUNGE

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) aliomba Spika Job Ndugai kuunda timu ambayo itafanya kazi ya ukaguzi wa deni la taifa akidai takwimu zinazotolewa si sahihi.

Zitto alisema usimamizi wa deni la taifa ni tatizo na amewataka wabunge kutazama ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka miwili.

Alisema kuna upotoshaji kuhusu taarifa za deni la taifa kwa sababu ya mfumo wa malipo na wa utunzaji wa kumbukumbu za deni la taifa havisomani.

Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema) alisema haridhishwi na jinsi Wizara ya Fedha na Mipango inavyofanya kazi kwa propaganda.

“Mioyoni mwetu haturidhiki jinsi Wizara ya fedha inavyofanya kazi, uchumi hauendeshwi kwa propaganda, nasema hivi Dk. Mpango yule wa Tume ya Mipango na huyu ni tofauti kabisa, pia Wizara ya Fedha inafanya mambo bila ya ruhusa ya Bunge,” alisema.

Mbunge wa Tanga Mjini, Musa Mbarouk (CUF) aliomba wafanyabiashara wasaidiwe katika biashara zao, huku akidai kwa sasa mfumuko wa bei upo juu, hivyo Wizara ya Fedha na Mipango inatakiwa iliangalie jambo hilo.

“Tuwasaidie wafanyabiashara, mfumuko wa bei upo juu, mwaka jana tambi ilikuwa Sh 1,800 leo ipo juu Sh 2,000. Mwananchi wa kawaida unapomwambia mfumo wa bei umepungua hakuelewi, tunasema uchumi umekua, hapana.

“Ukimwangalia mwananchi wa chini amechoka, yupo hohehae. Hebu tuwaeleze ukweli na tuwawekee mazingira rafiki,” alisema.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alihoji sababu za wezi kuingiza sukari kwa njia ya panya na  haiwakamati. 

 “Kuna watu wanaingiza sukari za viwandani kwa njia ya panya kuziingiza sokoni, kwanini hawa watu wezi watatu tu wanaojulikana hawakamatwi? Tunaenda kuharibu soko lote la sukari, hili swali nimeliuliza kwa miaka miwili katika Kamati ya Bajeti, lakini huwa sipati jibu.

“Tuanzishe kodi za kwenda kuua viwanda vyetu, sio ‘fair’, Waziri Mpango tunakubebesha dhambi nyingi, una mambo mengi, kwa sababu ni mmoja ‘be bold’, walazimishe polisi, walazimishe  Mambo ya Ndani wachukue hatua, sekta nzima inateketea.

“Hivi kweli Waziri Mpango Coca Cola ataingiza Industrial Sugar aipeleke Kariakoo akauze?” alihoji Bashe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles