30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Miji ya pwani hatarini kutoweka mwaka 2050

NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

RIPOTI ya wanasayansi wa Marekani imeonya kuwa kuongezeka kwa joto duniani kutasababisha kuinua kwa usawa wa bahari, na ifikapo mwaka 2050 kuna uwezekano wa kutokea kwa mafuriko makubwa yanayoweza kuifuta miji hiyo katika ramani ya dunia.

Katika kipindi cha miaka ya karibuni, kumekuwapo mafuriko makubwa katika miji ya pwani, mengi yakisababishwa na vimbunga na kwa wastani ukubwa wa mafuriko hutokea kila baada ya miaka 50, ambao unatarajiwa kuongezeka zaidi.

Wanasayansi hao wa jopo la watafiti kutoka tawi la Chicago la Chuo Kikuu cha Illinois nchini Marekani, walitoa makadirio hayo katika gazeti la Scientific Reports la Uingereza.

Ni baada ya kuchambua athari ya mambo mbalimbali yakiwamo mabadiliko ya hali ya hewa, mawimbi, dhoruba na shinikizo dogo la hewa.

Wanasayansi hao wanaona kuwa kuongezeka kwa joto duniani kutasababisha barafu kuyeyuka na usawa wa bahari duniani utainuka kwa sentimita 10 hadi 20 katika makumi ya miaka ijayo.

Kiongozi wa timu hiyo ya tafiti, Profesa Sean Vitousek, anasema usawa wa bahari ukiinuka kwa sentimita tano, miji ya Mumbai na Gorge nchini India na Abidjan nchini Ivory Coast itakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya mafuriko. Hali kadhalika wanasema usawa huo wa bahari ukiinuka kwa sentimita 10, miji ya Shanghai, London na New York pia itaathiriwa na mafuriko.

Profesa Vitousek anasema hatua za kukabiliana na mafuriko ni pamoja na kuhamisha miji ya pwani na kutenga fedha nyingi katika ujenzi wa miradi ya kukinga mafuriko pwani.

“Utafiti huu unaonesha hata mabadiliko kidogo ya kiwango cha usawa wa bahari kinaweza kuongeza ukubwa wa mawimbi,” anasema Thomas Wahl, Profesa wa Masuala ya Hatari za Fukwe wa Chuo Kikuu cha Central Florida, ambaye hata hivyo hakuwa sehemu ya timu ya utafiti huo.

“Kwa jamii za pwani, inamaanisha kwamba wanahitaji kubadilika ili kuzuia matukio ya mafuriko yasitokee mara kwa mara. Mwishowe kunahitaji la washika dau kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa kuzuia hali hii isilete majanga makubwa zaidi,” anasema Wahl.

Tafiti za nyuma zilikadiria kuwa hasara kutokana na mafuriko katika miji ya pwani itapaa kufikia dola trilioni moja kwa mwaka ifikapo 2050.

Vitousek anasema: “Tunatakiwa kupunguza kiwango cha hewa chafu inayosababisha hali hii. Tunataka kuona Greenland na Antarctica zinabakia barafu kwa kipindi cha miaka mingi ijayo kwa kadiri iwezekanavyo.

“Mita moja ya ongezeko la usawa wa bahari itabadilisha kila kitu katika ukanda wa pwani na kuiweka miji yetu katika hatihati,” anaonya.

Ripoti hiyo inaoana na ile iliyotolewa miaka michache iliyopita na timu ya wanasayansi wa mazingira wa Climate Central pia ya nchini Marekani.

Timu hiyo ilitoa  matokeo ya utafiti wao wa kisayansi unaoonesha namna ulimwengu utakavyokuwa iwapo mwenendo wa sasa wa ongezeko la joto hautabadilika.

Kwa taarifa, Climate Central ni taasisi isiyolenga faida ya habari ambayo inachambua na kuripoti masuala ya sayansi ya tabianchi, ikiundwa na wanasayansi mahiri na waandishi wa habari za sayansi, kwa ajili ya kuendesha tafiti za kisayansi za tabianchi na masuala ya nishati.

Iliweka pamoja mlolongo wa picha za kidijitali zilizobadilishwa kuonesha baadhi ya majiji ya pwani maarufu zaidi duniani na namna yatakavyoonekana ifikapo mwaka 2100 iwapo hakutakuwa na juhudi za kuzuia ongezeko la joto.

Katika kila picha, Climate Central ilionesha nini kitatokea kwa majiji hayo iwapo dunia itaondoa kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafu ya kaboni na kuweka ukomo wa ongezeko la joto duniani kufikia nyuzi mbili (2C) au 3F, na hatari ambayo itatokea iwapo dunia itaendelea katika kasi ya sasa ya ongezeko hilo.

Iwapo hakuna mabadiliko, watafiti hao wa sayansi ya mazingira wanaamini halijoto itaongezeka kufikia nyuzi joto nne (7F) miongo ijayo na kumaanisha vina vya bahari vitapanda kufikia hadi futi 36 na kutishia makazi milioni 760 katika mabara sita.

Majiji makubwa kama vile New York nchini Marekani, London nchini Uingereza, Sydney nchini Australia na Shanghai nchini China yanaweza jikuta yakipotelea majini pamoja na majiji mengine 17 makubwa sambamba na miji 1800 duniani.

Kwa mujibu wa tafiti nyingine, baadhi ya majiji hayo kama vile Bangkok, Thailand ni kama vile yamekata tamaa kupata njia ya kukabiliana na tishio hilo la kuzama miongo michache ijayo.

Kwa mujibu wa wanasayansi hao, utoaji wa hewa ya kaboni kama zile zinazozalishwa na magari au umeme kwa kutumia nishati inayotokana na mabaki ya ardhini (fossil fuels) kama vile gesi na makaa kutayafanya kubakia katika angahewa kwa muda mrefu na kusababisha ongezeko la joto hata miaka mingi baada ya kusitisha matumizi yake.

Hilo linamaanisha dunia tayari ‘imefungwa’ katika kiwango fulani cha kupanda kwa kina cha bahari, hata kama tutaweza kupunguza utegemezi wa nishati inayotokana na mabaki ya ardhini.

Hata hivyo, kwa kufanya upunguzaji mkubwa na wa haraka wa kaboni kipindi cha miaka ijayo, kuna uwezekano wa kupunguza hasara itakayokumba majiji makubwa duniani. 

Taarifa hiyo ilikuja siku chache kabla ya wakuu wa nchi karibu 200 duniani kukutana mjini Paris, Ufaransa kujadili kuhusu mabadiliko ya tabianchi, ukiwa umeandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN).

MIAMI, FL – JUNE 03: Waterfront condo buildings are seen June 3, 2014 in Miami, Florida. According to numerous scientists, south Florida could be flooded by the end of the century as global warming continues to melt the Arctic ice, in turn causing oceans to rise. U.S. President Barack Obama and the Environmental Protection Agency yesterday announced a rule that would reduce the nation’s biggest source of pollution, carbon emissions from power plants, 30% by 2030 compared to the 2005 levels. It is widely believed that these emissions are a main cause of global warming. (Photo by Joe Raedle/Getty Images)

Kwa sababu hiyo, kundi hilo lilitaka uamuzi utakaofikiwa uangalie kwa uzito taswira mbili za ulimwengu wa wakati ujao.

Mkutano wa mjini Paris unazingatiwa kuwa fursa ya mwisho kwa binadamu ya kuweza kuepusha madhara makubwa kabisa yanayotokana na kuongezeka kwa joto duniani.

Hakuna anayebisha kwamba hali hizo zinazosababisha ukame, mafuriko, dhoruba na kupanda kwa vina vya bahari kunatishia kuvimeza visiwa na maeneo ya pwani yanayokaliwa na watu wengi.

UN inazitaka serikali za mataifa mbalimbali kuanzisha kile inachokieleza kuwa mapinduzi ya nishati ili kudhibiti utoaji wa gesi zinazobeba joto zinazoharibu mazingira na kuepusha ongezeko la ujoto duniani.

Mawaziri waliopewa jukumu la kupatikana mkataba wa kihistoria kuiokoa dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi wamekuwa wakijaribu kutatua maeneo yanayosababisha mivutano katika ulimwengu huu wa kibiashara.

Bahati mbaya, mataifa yameonekana bado yanatofautiana kuhusu namna ya kuzisaidia nchi zinazoendelea kiuchumi kukabiliana na gharama za ongezeko la joto duniani.

Aidha, bado zinatofautiana juu ya ukomo unaostahili kuwekwa wa kiwango cha joto duniani, pamoja na namna ya kugawana mzigo baina ya mataifa tajiri na maskini na namna ya kutathmini hatua zilizopigwa katika kupunguza gesi zinazochafua mazingira.

Kutofautiana huko kunatokana na ukweli kwamba ni mataifa makubwa ndiyo yanayochangia ongezeko la joto duniani kutokana na utitiri wa viwanda vyao yanatakiwa kuyasaidia mataifa masikini ambayo ni waathirika wakuu kutokana na kukosa uwezo wa kuyakabili.

Lakini mataifa hayo tajiri yanaonekana kutoyaamini yale masikini katika matumizi ya fedha huku pia yakitegemeana yenyewe kwa yenyewe katika kiwango cha kupunguza joto kutokana na eneo hilo kugusa uhai wa viwanda na chumi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles