25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

MIILI YA WANAJESHI WALIOUAWA CONGO YAWASILI NCHINI

Miili 14 ya wanajeshi waliokuwa wakilinda amani nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) imewasili nchini na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo, jijini Dar es Salaam.

Miili ya wanajeshi hao wanaosadikiwa kushambuliwa na Kikundi cha waasi cha ADF nchini humo, imepokelewa katika Uwanja wa Jeshi ulioko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JNIA), saa 11 jioni leo na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Luteni Jenerali Venance Mabeyo.

Akizungumza baada ya kupokelewa kwa miili hiyo, Dk. Mwinyi amesema vyombo vya ulinzi nchini vimesikitishwa na tukio hilo ambalo limetokea wiki iliyopita.

“Miili ya wanajeshi wetu itaagwa Alhamisi wiki hii pale pale katika Hospitali ya Lugalo, na kwa kweli tumesikitishwa na tukio hilo kwani wanajeshi wetu walikuwa wakilinda amani lakini ikatokea bahati mbaya wameuawa, hatuna jinsi zaidi tutajipanga upya,” amesema.

Kwa upande wake Luteni Jenerali Mabeyo, amesema tukio kubwa kama hilo lilitukia miaka mitano iliyopita na kuahidi kujiimarisha lakini pamoja na hayo hakuna hofu iliyotanda ambapo jeshi linajipanga kutazama wapi lilipokosea ili lijisahihishe.

“Kikundi cha waasi wa ADF si kikubwa sana lakini ni mbinu tu mapambano na kwamba jeshi la Tanzania liko kwa ajili ya kulinda amani na si kwa ajili ya kupigana. Ni bahati mbaya zaidi wenzetu wameshtukiza ndiyo maana yametukia haya,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, amesema wanajeshi waliojeruhiwa wanaendelea vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles