25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

MIGOGORO YA WAFUGAJI YAKERA WABUNGE

Na MAREGESI PAUL -DODOMA


MIGOGORO ya wakulima na wafugaji imeonekana kuwakera wabunge wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita na Waziri Dk. Charles Tizeba.

Aliyekuwa wa kwanza kuonyesha jinsi asivyoridhishwa na uwepo wa migogoro hiyo, ni Mbunge wa Hanang, Dk. Mary Nagu.

Katika mchango wake, Dk. Nagu alisema zitatakiwa jitihada za haraka ili kukabiliana na migogoro hiyo kwa kuwa inarudisha nyuma sekta ya kilimo.

“Mifugo ni mali ya mtu mmoja mmoja, lakini ni rasilimali ya taifa kwa kuwa inachangia kukuza pato la taifa.

“Lakini pia, sekta ya kilimo ni muhimu katika nchi yetu, japokuwa inaonekana imesahaulika sana. Kwa mfano, mwaka 2011 sekta hiyo ilichangia katika pato la taifa kwa asilimia 3.5 na mwaka 2016 ilishuka hadi kufikia asilimia 1.7.

“Kwa hiyo, lazima tuwekeze katika kilimo, ikiwa ni pamoja na kuweka njia sahihi za kukabiliana na migogoro ya wakulima na wafugaji,” alisema Dk. Nagu. 

Naye Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Abdallah Bulembo (CCM), aliitaka Serikali ieleze ni lini itakuwa na sheria ya kuwabana wauzaji wa nyavu haramu kama inavyowachukulia hatua wavuvi wanaozitumia.

Kwa mujibu wa Bulembo, kitendo cha Serikali kutowachukulia hatua wauzaji hao, hakiwatendei haki wavuvi kwa kuwa wanalazimika kununua nyavu hizo kwa vile zinapatikana madukani.

Akizungumzia migogoro ya wakulima na wafugaji, alisema lazima Serikali ichukue hatua imara za kukabiliana nayo kwa kuwa imekuwa ikisababisha vifo vya watu na mifugo bila sababu za msingi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), alisema kama hakutakuwa na mipango mizuri ya ardhi, migogoro itazidi kutokea katika maeneo ya wakulima na wafugaji.

“Ili kilimo kiweze kuwa na faida nchini, lazima sasa ramani ya ardhi ichorwe upya kwani migogoro inayotokea inatokana na kutokuwapo kwa ramani hiyo.

“Jambo jingine ninalotaka kusema ni kwamba hakuna maendeleo katika viwanda kama kilimo hakijaimarishwa.

“Lazima tuwe na mikakati ya kuhifadhi maji ya mvua zinazonyesha kwa sababu hapa kwetu mvua zikinyesha, maji yanapotea na mvua zikikata, tunaanza kuathiriwa na ukame,” alisema Mapunda.

 Wiki iliyopita, Mbunge wa Viti Maalumu, Aza Hamad (CCM), naye alilalamikia migogoro hiyo na kusema chanzo chake ni malisho na maji kukosekana katika maeneo ya wafugaji.

Ili kukabiliana na hali hiyo, alisema kuna haja Serikali iwahamasishe wafugaji kupanda nyasi kwa mifugo yao.

Naye Mbunge wa Malindi, Ally Salehe (CUF), alisema zinahitajika mbinu mbadala kuiimarisha sekta ya kilimo nchini kwa kuwa wataalamu walioko serikalini wameshindwa kutimiza wajibu wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles