NA RAMADHAN LIBENANGA, MVOMERO
KIKUNDI cha ulinzi kiitwacho Mwano kimevamia nyumbani kwa mfugaji mmoja, Christina Nuru wilayani Mvomero na kuua idadi kubwa ya ngombe na mbuzi.
Tukio hilo lilitokea jana mchana katika Kijiji cha Kambala na inasemekana mifugo 80 walijeruhiwa na wana kikundi hao walipokuwa wakitekeleza unyama huo.
Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mwiguru Nchemba, aliagiza wafuasi wa kikundi hicho wakamatwe ili wachukuliwe hatua za sheria.
Akizungumza katika Kijiji cha Dihombo, Kata ya Embeti, Nchemba alisema kitendo kilichofanywa na wafuasi wa kikundi hicho ni cha kinyama na hakiwezi kuvumiliwa kwa namna yoyote.
“Nimesikitishwa na kitendo hiki, yaani mbuzi wanakatwakatwa mapanga wakati hawajaingia shambani kwa mkulima!
“Hili siyo jambo la kuvumilia, kwa hiyo, naagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya iwakamate waliohusika hata kama ni viongozi wa Serikali.
“Hakuna asiyetambua umuhimu wa kulima ama wa kufuga lakini kitendo cha kuchukua sheria mkononi hakiwezi kuvumiliwa.
“Tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi imekuwa ya kawaida sana katika wilaya hii, nashangaa kwa nini viongozi wa wilaya hii mnashindwa kukabiliana na changamoto hizi?” alihoji Nchemba.
Hata hivyo, waziri aliwataka wafugaji wasilipize kisasi kwa kitendo kilichofanywa na wakulima kwa kuwa kunaweza kuchafua hali ya hewa.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa, alisema migogoro ya ardhi ni mingi wilayani humo na imekuwa ikichochewa na wanasiasa.
Naye Mbunge wa Mvomero, Sadick Murad (CCM), alisema Mvomero imekuwa na sura mbaya kwa muda mrefu kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji isiyokwisha.
Diwani wa Kata ya Embeti, Peter Mdidi, alisema migogoro inasababishwa na viongozi wa wilaya kwa kuwa wanashindwa kuchukua hatua wanapotakiwa kufanya hivyo.