29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MIFUGO ILIYOKAMATWA IAACHIWE – DC

Na SAMWEL MWANGA – MASWA

MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk. Seif Shekalaghe, ameagiza kuachiwa mara moja kwa mifugo iliyokamatwa ikilishwa katika chanzo cha maji cha bwawa la Nyanguganwa lililoko mjini hapa kwa kuwa wafugaji hawajapewa elimu juu ya utunzaji wa mazingira kwenye eneo hilo.

Mifugo iliyokuwa inashikiliwa ni ng’ombe 70 waliokamatwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa) ambao ni wamiliki wa bwawa hilo baada ya kukutwa ikilishwa ndani ya eneo la hifadhi ya chanzo hicho cha maji.

Dk. Shekalaghe alitoa uamuzi huo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari za mazingira waliotembelea vyanzo vya maji katika wilaya hiyo na kujionea jinsi baadhi ya watu wanavyofanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivyo na kusababisha kukauka.

“Wananchi hawa walikuwa hawajapewa elimu vizuri, na Mauwasa walikuwa hawajaweka matangazo yoyote ya kuzuia mifugo hiyo kuchungwa wala kunyeshwa maji katika bwawa hilo na ukizingatia ni muda mrefu wafugaji walikuwa wakilitumia eneo, hivyo kwa kuzingatia hali hiyo kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tuliona ni busara kuiachia mifugo hiyo,” alisema.

Alisema kwa sasa wananchi hao watapewa elimu ya kutoingiza mifugo yao katika vyanzo vya maji sambamba na kutofanyika shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya bwawa hilo kwani Mauwasa inatarajia kulitumia kama chanzo kingine cha maji.

“Natumia fursa hii kutoa elimu na kuwaelimisha wananchi kuwa hii ni mara ya mwisho kufanya shughuli za kibinadamu katika bwawa la Nyanguganwa kwa sababu Mauwasa wanajiandaa kufanya majaribio ya kusukuma maji ili kiwe chanzo kingine cha maji katika mji wa Maswa ambao una chanzo kikuu cha maji cha bwawa la New Sola lililoko katika Kijiji cha Zanzui,” alisema Dk. Shekalaghe.

Mmoja wa wafugaji ambaye mifugo yake iliachiwa, Stanley John, alipongeza uamuzi huo na kusema kuwa kwa sasa watakuwa walimu wazuri kwa wafugaji wenzao juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji.

“Tunamshukuru sana Mkuu wa Wilaya kwa kutumia busara na kuachia mifugo yetu na tumepatiwa elimu juu ya athari za uharibifu wa vyanzo vya maji, tutakuwa mabalozi wazuri kwa wenzetu na sasa Serikali ichukue hatua kali za kisheria kwa watu wote watakaofanya shughuli za kibinadamu katika hifadhi ya vyanzo vya maji wilayani Maswa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles