29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

RC APIGA MARUFUKU KUPIGA YOWE

Na BENJAMIN MASESE – MARA

MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amepiga marufuku utaratibu wa wananchi wa vijiji vitatu vya Remng’orori, Mikomarilo na Sirorisimba vilivyoko katika wilaya za Bunda, Serengeti na Butiama vinavyogambania mipaka ya wilaya zao, kupiga yowe pale inapotokea kuwapo na jambo la hatari.

Marufuku hiyo imekwenda sambamba na katazo la kuzuia shughuli zozote zikiwamo za kilimo eneo linalogombaniwa, kutotumiwa na pande zote hadi hapo Serikali itakapoamua vinginevyo, ikiwa ni njia pekee ya kuzuia athari zitakazoweza kutokea.

Malima amewataka wananchi wa vijiji hivyo kutoa taarifa Jeshi la Polisi pale linapotokea jambo la kiuhalifu au linalohatarisha usalama wao, kuliko kujichukulia sheria mkononi na kusababisha uvunjifu wa amani.

Kauli hiyo aliitoa juzi wakati akizungumza na timu ya waandishi wa habari kutoka Mwanza, waliokwenda mkoani Mara katika vijiji vya Remng’orori kilichopo wilayani Serengeti, Sirorisimba (Butiama) na Mikomarilo (Bunda) kufuatilia mvutano wa mipaka uliodumu zaidi ya miaka 40.

Malima alisema amelazimika kuzuia yowe katika vijiji hivyo kwa sababu amebaini ilikuwa ikitumika vibaya kwa kukusanya watu kwa hisia zisizo za kweli,  huku baadhi ya wananchi wakitumia nafasi hiyo kufanya uchochezi dhidi ya upande mwingine.

“Kwanza nimezuia eneo lile linalogombaniwa maarufu ‘Sambusa’ lisitumiwe na pande zote, pia utaratibu wa kupiga yowe nimezuia kabisa hata kama kuna jambo lolote la hatari, wanachotakiwa kufanya ni kutoa taarifa polisi kwani wao ndio waliopewa jukumu la kulinda raia na mali zao.

“Nimefanya hivyo kwa sababu tangu kutokea tukio la uvamizi lililosababisha watu wawili kuuawa, sasa kila mtu akiona wakiwa wawili au watatu anaanza kuwa na hofu na kupiga yowe, ikiashiria kuomba msaada upande wa kijiji chake na watu kujikusanya, hapo ndipo uchochezi unapotokea kwa sababu ya hisia za mtu,” alisema.

Malima alisema wapo baadhi ya viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wamefikia hatua ya kutoa taarifa potofu katika mamlaka za juu kwa lengo la kumharibia, lakini ameahidi kusimamia ukweli kwa lengo la kuhakikisha anamaliza tatizo hilo.

Alisema kitendo kilichofanywa na wananchi kutoka Mikomarilo kwenda kuwafuata wananchi wa Remng’orori wakiwa mashambani na kuwaua huku wakisingizia kwamba wameporwa ng’ombe zao, ni ujambazi uliokamaa.

“Kama kila pande haitakuwa tayari kutafuta suluhu ama kukubaliana na mapendekezo yatakayofikiwa, basi Serikali italichukua eneo hilo na kuwakabidhi Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na magereza ili litumike kwa kuzalisha chakula, kwa bahati nzuri eneo lile ni zuri sana kwa kila zao,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles