Na Mulusale Maziku,
JIJI la Dar es Salaam bado linakabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri wa umma. Ukipita eneo la Gerezani, Karikaoo nyakati za jioni utaona umati wa watu katika kituo cha daladala za Mbagala na Temeke.
Umati huu unatoa taswira ya changamoto ya usafiri wa umma Dar es Salaam. Daladala zinapofika abiria hukimbilia na kurukia gari huku wengine wakipitia madirishani.
Lakini upande wa pili wa eneo hilo, kipo kituo cha mabasi ya UDART yanayotoa huduma za usafiri wa haraka katika mfumo maalumu lakini hawakusukumani na kugombana kama wale wa upande wa pili.
Abiria wanaotumia usafiri wa mabasi ya mwendo kasi wana uhakika wa kufika mwisho wa safari yao kwa dakika 40 na pengine chini ya hapo tofauti na wenzao wa njia ya Mbagala ambao hawana muda maalumu wanaotumia njiani.
Hata hivyo, wapo baadhi ya abiria wanaotumia usafiri wa mabadi ya mwendo kasi wanaotamani kurudi kwenye dala dala.
Na huu ndiyo msingi wa kuandika makala haya. Ninayajua mateso ya usafiri wa umma ndani ya nje ya nchi. Nchi chache zenye miradi ya usafiri wa umma wa uhakika ndizo ambazo raia wake wana uhakika wa kusafiri wakati wowote bila ya kukutana na changamoto za hapa na pale.
Mimi ni mmoja wa watumiaji wa usafiri wa mabasi yaendayo kasi na yapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya abiria kuwa watoa huduma hii wameshindwa.
Nimefanya uchunguzi kidogo na kugundua kuwa mradi huu, mfumo wake wa utoaji huduma ni wa mpito na siyo huduma kamili, kwa hiyo viko vitu vingi ambavyo vinaweza kuwa na upungufu lakini kiuhalisia ni uhitaji wa masharti ya huduma ya mpito.
Moja kubwa ni muda wa watu kukaa sana vituoni, mwanzoni kulikuwa na malalmiko kwamba mabasi yanafungiwa Jangwani na abiria wanateseka hili lilinishangaza, nikafikiri hawa wanaotoa huduma wanaweza kuwa na aina fulani ya uendawazimu, kama abiria wao wanapata shida halafu wao, wanapaki mabasi Jangwani, waliyaleta ya nini basi!
Nimefanya uchunguzi na kugundua kuwa watoa huduma wa mradi huu yaani UDART, wanafanya juhudi kubwa mpaka kutoa huduma bora kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Nimeambiwa kuwa mradi huu unahitaji mabasi 305, ambayo yatahudumia njia zinazotumiwa sasa na mwendokasi, (yaliyopo sasa ni 140) lakini pia kutakuwa na ongezeko la idadi ya njia za mlisho (feeder) zaidi ya sita, pale huduma kamili (Full Service Provision) itakapoanza mapema mwakani.
Katika idadi hiyo ya mabasi, mabasi yanayotakiwa kufanya kazi kwenye trunk, ni zaidi ya mabasi 180, na kwa sasa kama kukiwa na mabasi mengi sana kwenye trunk, hayazidi 120, hii ndiyo kusema watoa huduma wa sasa wanatoa huduma wakiwa na upungufu wa mabasi 60 kwenye trunk, na nikaambiwa suala la kuamua kuleta mabasi haliko mikononi mwa UDART, liko kwa Serikali kupitia wakala wake DART, watakapomtunuku tenda atakayeshinda zabuni ya kutoa huduma kamili.
Changamoto kama za mtandao, ni jambo ambalo lazima Serikali ihakikishe kuwa inakuwa na mfumo mzuri na wa uhakika wa mtandao kupitia kampuni yake TTCL, kwa kuwa sasa maisha yetu yanakwenda kimtandao tu, itafika mahali maisha yetu hayatawezekana bila kuwa na mtandao imara na wa kutegemewa, changamoto ya mtandao inayotokea kwa mifumo ya UDART na wakala wake Maxicom, ituamshe tujua umuhimu wa kuwa na mtandao imara.
Zama za daladala zimepita
Zipo kampeni za baadhi ya watu kupinga mfumo wa usafiri wa mwendo kasi kwa sababu dala dala na wamiliki wake wanaathirika kiuchumi na kwamba wana mikopo benki ambayo sasa hailipiki.
Mfumo wa usafiri wa umma unaotumia mabasi makubwa na barabara maalumu ulianza kutumika kwa mara ya kwanza duniani mwaka 1974 katika mji wa Curitiba, ulioko Brazil.
Huduma hii sasa imekuwa ni mfumo muhimu wa kusafirisha abiria mijini kwa wepesi sehemu nyingi duniani. Miradi mingi na mikubwa imeanzishwa Afrika, Australia, China, Indonesia, Iran, Mexico, Uturuki na katika majiji mengi tu barani Ulaya na Amerika.
Msingi wa mfumo huu ni kuhakikisha abiria wanasafirishwa kwa haraka katika namna ambayo haina madhara makubwa kwa mazingira, lakini pia kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu mijini kwa sababu kuendelea na usafiri ambao hapa kwetu unajulikana kama dala dala hakuwezi kuhimili mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu mijini.