25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Michomoko kurudishwa stendi mpya (Somanda)

Na Derick Milton, Bariadi

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila ametoa siku saba kwa mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange kufanya tathimini ya uamuzi uliofanyika wa kuhamisha magari madogo (Mchomoko) kutoka stendi ya mpya ya Somanda kwenda standi ya zamani kama umeathiri ukusanyaji wa mapato yatokanayo na mradi huo.

Kafulila ametoa tamko hilo jana alipotembelea standi hiyo kujionea hali halisi na kumtaka mkuu wa wilaya na wataalam wake kufanya tathimini ya kina ambayo itaonesha kama makusanyo yamepungua au yameongezeka.

Alisema serikali ya awamu ya sita haikusanyi hela kwa utaratibu ambao sio afya kwa raia na ndo msingi wa uamuzi wa awali wa kuhamisha magari madogo na kuyapeleka standi ya zamani .

Mkuu huyo alisema maamuzi yaliyofanyika yalifanywa kwa lengo la kuondoa usumbufu kwa wananchi ambao walikuwa wakisumbuli pindi walipokuwa wakienda kupata huduma hiyo.

“Mkuu wa wilaya na wataalam wako nendeni mkafanye tathimini…na kama itaonekana uamuzi uliofanywa haukuwa sahihi ubadilishwe,na mpaka sasa kwa haraka haraka mapato yameshuka hivyo mje na majibu na ushawishi wa kutosha kwangu jumatatu wiki ijayo ambao utanifanya nibadilishe uhamuzi au ubaki pale pale,” amesema Kafulila.

Amesema wakati maamuzi yanafanyika kuhamisha magari hayo, mkuu wa wilaya na wamiliki wa magari walinihakikishia kuwa mapato ya Halmashauri hayataathirika jambo ambalo limeonekana kuwa sio kweli na kwamba uhalisia unaonesha mapato yameshuka kwa kiwango kikubwa.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Bariadi, Maganiko Msabi amesema baada ya magari kuhamishwa makusanyo yamepungua kwani kabla ya uamuzi halmashauri ilikusanya asilimia 75 ya lengo ndani ya standi hiyo.

“Kwa mwaka wa fedha 2020/ 2021 tulikusanya Sh milioni 224.2 sawa na asilimia 75 hapo ni kabla ya magari madogo kuhamishwa lakini kwa mwaka wa fedha 2021/2022 toka Julai 2021 hadi Machi 30, mwaka huu tumekusanya Sh milioni 112.2 sawa na asilimia 37 ya lengo,” amesema.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange akitetea uamuzi wa awali alisema kuwa kilichosababisha kushuka kwa mapato sio uamuzi huo bali kuna mianya ya upotevu wa mapato.

Amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakihujumu standi hiyo na kusababisha kupungua kwa mapato kwani kuna baadhi ya mabasi makubwa yamekuwa yakipakia abiria nje ya standi tofauti na utaratibu na hayachukuliwi hatua.

Baadhi ya mawakala wamempongeza mkuu wa mkoa kwa kutembelea standi hiyo na kumueleza kuwa uamuzi uliofanyika haukuwa sahihi kwani ndio chanzo cha kupungua mapato na ni vema magari madogo yarudishwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles