26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Wizara ya Kilimo, NMB zakubaliana kukuza kilimo nchini

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WIZARA ya Kilimo na Benki ya NMB, wameingia makubaliano ya kukuza sekta ya kilimo nchini ambapo benki hiyo imetenga sh bilioni 20 kwa ajili ya kutoa mikopo ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao hasa maeneo ya vijijini na Sh bilioni 100 kwa ajili ya kukuza kilimo nchini.

Waziri wa Kilimo na Chakula ,Hussein Bashe (katikati) akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari (Hawapo Pichani) wakati wa kutangaza makubaliano kati ya wizara ya kilimo na benki ya NMB kutusu kushusha riba ya mikopo kwa asilimia tisa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Kulia ni fisa Mtendaji Mkuu wa benmi ya NMB Ruth Zaipuna na Afisa Mkuu wa Wateja binafsi na Biashara Benki ya NMB ,Filbert Mponzi (Kushoto). Makubaliano hayo yalifanyika jijini Dodoma wiki hii

Akizungumza katika hafla ya makuliano hayo iliyofanyika jana katika ukumbi wa Hoteli ya Morena mjini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema kuwa wamekubali kuingia makubaliano hayo baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya Benki hiyo na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.

Alisema mikopo hiyo ya ujenzi wa maghala, itatolewa kwa riba nafuu ya asilimia 9 na mazao yanayolenga kwa kuanzia ni korosho, pamba na nafaka. 

Alisema mkopo huo ni mwendelezo wa juhudi ya NMB kuuza sekta ya kilimo nchini kwani Oktoba mwaka jana, benki hiyo ilitenga shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya kukopesha sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwa riba isiyozidi asilimia 10.

“Kwa taarifa tu, mpaka sasa zaidi ya shilingi Bilioni 80 zimeshatolewa kwenye mikopo hii. Baada ya kuona shilingi bilioni 100 zinaisha, leo tunaona tuongeze nyingine kama hizo ili kuongeza utoaji wa mikopo kwa wakulima, wavuvi, wafugaji na wajasiliamali katika sekta hizi huku tukipunguza riba ya mikopo hii mpaka asilimia 9,” alisisitiza Zaipuna.

Alisema kuwa nyongeza hiyo ya shilingi bilioni 100 kwenye mikopo na shilingi Bilioni 20 kwenye ujenzi wa maghala, kunafanya kiasi ambacho tayari kimetengwa na NMB kwa ajili ya mikopo nafuu ya kilimo kufikia shilingi Bilioni 220.

“Leo tupo hapa na waziri wa kilimo Mh Hussein Bashe ili kuwatangazia makubaliano tuliyofikia kati ya wizara ya kilimo na benki ya NMB yanayolenga kuendeleza juhudi za kukuza kilimo nchini.

Tumekuwa na mazungumzo kadha na Mh Waziri toka alipoteuliwa kuwa waziri wa kilimo. Kwetu kama Benki ilikuwa ni muhimu sana kuonana na kuelewa maono ama vision aliyonayo waziri kwenye sekta ya kilimo kama waziri mwenye dhamana ili sisi tuweze kuona ni jinsi gani tutaingia kusaidia kutekeleza maono hayo,” alisema Zaipuna 

Alisema moja ya changamoto kubwa waliyoongea na Waziri Bashe inayowakabili wakulima vijiini ambayo NMB wanaweza kusaidia kutatua kwa sehemu ni ukosefu wa maghala ya kuhifadhia mazao hasa maeneo ya vijijini.

 “Ni matarajio yangu kuwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wajasiliamali katika tasnia hii watumie fursa hii kuendelea kujipatia mikopo nafuu na kujiongezea kipato na kujenga nchi yetu.

Kwa mujibu wa Zaipuna, NMB  itazingatia masharti ya utoaji wa mikopo hii nafuu kwa kuzingatia taratibu za ukopeshaji ikiwemo kiwango cha juu cha mkopo cha TZS 1 Bilioni kwa mkopaji mmoja. Mkopaji huyu anaweza kuwa mtu binafsi, chama cha ushirika, kampuni au taasisi yeyote itakayokidhi masharti ya ukopeshaji.    

“Ninatoa wito kwa wanaotaka kukopa mikopo hii nafuu zaidi sokoni, kutembelea mtandao wetu wa matawi 226 yaliyo enea nchi nzima ili kuweza kupata huduma za mikopo hii ya riba nafuu,”  alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Bashe aliipongeza NMB kwa juhudi zake za kukuza sekta ya kilimo nchini.

Alisema moja ya changamoto wanayokabiliana nayo wakulima vijijini ni mazao yao kupoteza ubora kabla ya kufika sokoni kutokana na mazingira mabaya ya kuhifadhi mazao yao.

“Kule vijijini ukiona magunia mengi ya mazao yamewekwa kwenye eneo la mashine za kusaga, usifikiri kuwa ni mali ya mwenye mashine hiyo. Magunia hayo ni mali ya wakulima yamehifadhiwa hapo baada ya kukosa ghala la kuhifadhia na yanapofika sokoni, yanakuwa yamepoteza ubora na thamani yake,” alisema Bashe.

Waziri Bashe alisema wizara yake inatambua matatizo na changamoto za wakulima na imejipanga kukabiliana nayo kwa kushirikiana na wadau kama Benki ya NMB.

Alisema maghala hayo yatajengwa kupitia vyama vya ushirika na Wizara ya kilimo itasimamia kuhakikisha dhamila ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kukuza sekta ya kilimo, inatimia.

Alisema maghala yatakayojengwa, yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 100, 200 hadi 300 ili wakulima waweze kutunza mazao yao na yabaki kwenye ubora kabla ya kufika sokoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles