27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA NANE YA TRUMP MWIMBA KWA WAAFRIKA


Na Hafidh Kido

ANGA za kimataifa zimeanza upande wa Afrika zimeanza vibaya mwaka huu kufuatia matamshi mabaya yaliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Trump ametamka kuwa mataifa yanayoingia katika ulimwengu wa tatu yanapatikana katika shimo la choo: ‘Shithole Countries.’

Baada ya kauli hiyo baadhi ya wanasiasa na waandishi wa habari nchini wametoa matamko yao kulaani na wengine kuunga mkono.

Baadhi ya waandishi nguli nchini wameieleza kauli hiyo ya kifedhuli kuwa imetolewa katika eneo sahihi.

Kwa muktadha huo nadhani miongoni mwetu  Waafrika wapo wasiojitambua.

Tafsiri ya haya nitakayoyasema haitokani na chochote zaidi ya kujivunia uafrika wangu, nieleweke kuwa sijivunii mabaya yanayotokea Afrika kama ambavyo hao wanaojiita wanahabari nguli walikubaliana kuwa sisi ‘Waafrika’ jina la ‘Shithole Countries’ linatustahili kwa sababu tuna viongozi wa hovyo wanaoendekeza rushwa na kujilimbikizia mali.

Hivi karibuni nilisoma habari mtandaoni juu ya raia wa Mexico aliyetimuliwa nchini Marekani baada ya kuishi katika ardhi hiyo kwa miaka 30 tangu akiwa na umri wa miaka tisa.

Jorge Garcia (39), anaonekana katika picha akiwa ameikumbatia familia yake yaaani  mke na watoto wawili katika uwanja wa ndege nchini humo, amelazimika kuiacha familia yake na kurejea kwao Mexico kuanza maisha mapya.

Garcia anasema anatamani Rais Trump, angekuwa hakimu wa kesi hizi za uhamiaji kwa sababu watu aliowapa mamlaka wanafanya makosa makubwa bila kujitambua. Garcia ameshindwa kuelewa kuwa agizo la kuwaondoa wahamiaji wote nchini humo zimesemwa katika kipindi cha kampeni ya urais, hivyo kufukuzwa kwake ni kutekeleza ilani ya chama cha Republican kilichompa dhamana Trump kuongoza nchi.

Nikirejea katika kauli ya Trump ya Januari 18, 2018 msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Sanders, alitoa taarifa ya kumtetea bosi wake kuhusiana na matamshi hayo ya kibaguzi yenye mlengo wa kidhalimu.

Utetezi aliotoa ni kusisitiza kuwa hakumshuhudia Trump akitamka maneno hayo bali huenda yametengenezwa na wabaya wao.

Sarah anasema Trump si roboti ya maandishi alitumia neno ‘Scripted robot’ akimaanisha katika hotuba zake huwa hasomi moja kwa moja kila kilichoandikwa huwa na maneno mengine magumu kuyapokea. Akaweka wazi kuwa maneno hayo magumu ndiyo yaliyomsaidia kupata urais.

Kauli hii ni ya kweli, kwa sababu Trump akiwa mgombea alikuwa maarufu kwa kauli za hovyo juu ya Waislamu, wahamiaji na watu weusi. Aliwatusi kwa kadiri alivyoweza na aliahidi akipata ridhaa ya Wamarekani kuongoza nchi atawafukuza wote.

Katika hali inayoonyesha Sarah haoni uzito wa kauli ya bosi wake, alipoulizwa na wanahabari anaizungumziaje kauli hiyo alisema: “Hakuna mtu hapa atakayejifanya hajui Rais Trump hayuko sahihi kisiasa. Si mwanasiasa na nadhani hiyo ndiyo sababu raia wa Marekani wanampenda.

“Miongoni mwa sababu zilizomfanya akashinda urais na sasa anakaa katika ofisi ya Oval ni kwa sababu si roboti wa maandishi. Ni mtu anayeeleza kila kitu kama kilivyo, hajui kufunika maneno wala kuyapaka rangi, mara nyingine anatumia lugha za kuudhi.”

Unaweza kujiuliza mjadala huu unatokea wapi hasa. Ni hivi: Rais Trump alikuwa katika moja ya vikao vyake vya kazi kujadili hali ya wahamiaji nchini humo akawauliza wasaidizi wake wakiwemo maseneta kuwa hadi lini Marekani itaendelea kupokea wahamiaji kutoka Haiti na ‘shithole’ mataifa ya Kiafrika?

Seneta wa chama cha Democratic, Dick Durbin na baadhi ya maseneta wenzake walisema wamemsikia akisema neno hilo, baadhi ya maseneta na wasaidizi wa Trump wamedai kutomsikia huku wakibainisha kauli yake imetafsiriwa vibaya.

Katu hatutakuwa tayari kuonekana tunajisafisha bali huo ndio ukweli kuwa Afrika hatustahili kutukanwa na mtu asiye msafi.

Ingrid Rojas, mwenye asili ya Colombia ambaye siku Rais Trump anatoa kauli ya kuwatukana watu wa dunia ya tatu alikula kiapo kuwa raia wa Marekani ameandika makala yenye kichwa cha habari: ‘I became an American the day Trump made his ‘Shithole Countries’ comment.’

Anaandika Rojas: “Saa ya kwanza nikiwa raia wa Marekani nimezitumia wakati rais akiita Haiti, El Salvador na nchi za Kiafrika ni mataifa yaliyo katika shimo la choo. Hali yoyote ya mapokezi tuliyopewa na rais wa nchi kwa raia wapya 1,123 tulijihisi siku hiyo ya kwanza kabisa.

“Lakini maneno yake (Trump) si kuwa hayana maana. Akiwa amiri jeshi mkuu maneno yake yanatengeneza sera na mwongozo wa taifa.”

Siku ambayo Trump anatoa matamshi haya mabaya ndani ya taifa hilo hilo kwenye ukumbi wa Paramount Theater katika Mji wa Oakland jimboni California wahamiaji kutoka mataifa 88 walikuwa wamesimama wanakula kiapo cha utii huku wameinua mikono yao juu ya kuume wakisema: 

“I hereby declare, on oath, that I absolutely and entirely renounce and abjure all allegiance and fidelity to any foreign prince, potentate, state, or sovereignty…”

Tafsiri isiyo ya moja kwa moja raia hawa wapya zaidi ya 1,000 walikula kiapo wakisema wanaapa kwamba wanapinga na kuachana kuwa watiifu wa utawala au kiongozi mwingine yeyote ama taifa jingine lolote lisilokuwa Marekani.

Maana yake ni kuwa raia hawa wapya tangu siku hiyo ni Wamarekani na chochote kwao ni kuiona Marekani njema, kuiunga mkono rohoni ingawa midomoni wataisema kama ambavyo wapo raia weupe wa taifa hilo wanainua midomo kumsema kila kiongozi anayekosea.

Ninachotaka kukiweka hapa au ujumbe ninaotuma katika makala haya ni kuwa viongozi wa mataifa yaliyotukanwa na Trump yakiwemo yale ya Ulaya Mashariki, Latin America na sehemu ya mataifa ya Asia lazima waionyeshe jamii kuwa wamekerwa, na dhamira yao iwe hivyo kuwa wamekerwa.

Kama hiyo haitoshi, mbali ya Umoja wa Afrika (AU) kutoa kauli ya pamoja kupinga matamshi ya Trump lakini zichukuliwe hatua za pamoja kuangalia namna ya kujisimamia kwenye suala la uchumi kwa sababu rais huyo wa Marekani anakuwa na jeuri kwa sababu ya nchi yake kuwa na uchumi mkubwa.

Afrika na mataifa mengine ya dunia ya tatu ndio wanayotegemewa na mataifa ya dunia ya kwanza katika nishati na madini.

Asilimia kubwa ya mafuta na gesi ya kuendesha mitambo inatoka katika ukanda huu, vito vya thamani vinavyovaliwa katika masikio na shingo za matajiri wa Marekani na Ulaya vinatoka katika ukanda huu wa ‘Shithole Countries.’

Tuchukue hatua, kwa sababu haisaidii kuwa na kauli za kupinga matamshi ya Trump ambaye tayari msemaji wa Ikulu ya White House, Sarah anadai yeye si roboti wa maandishi  ‘Scripted robot’ maana yake tujiandae kwa matusi kwa miaka minane ya utawala wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles