Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
IKIWA ni miaka mitatu na miezi 11 tangu Rais Dk. John Magufuli kuingia madarakani, tayari amewafuta kazi mawaziri na manaibu waziri 11 kwa sababu mbalimbali.
Idadi hiyo ilifikiwa jana baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Dk. Susan Kolimba aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli amemteua Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro (CCM) kuchukua nafasi ya Dk. Kolimba.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza sababu ya Dk. Kolimba kuondolewa kwenye nafasi yake ambayo ameitumikia tangu Desemba mwaka 2015 Rais Magufuli alipotangaza baraza lake la kwanza la mawaziri.
Taarifa ya Ikulu ya jana, ilisema pia Rais Magufuli amemteua Dk. Faraji Mnyepe kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akichukua nafasi ya Profesa Adolf Mkenda, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Profesa Mkenda anachukua nafasi ya Meja Jenerali mstaafu Gaudence Milanzi ambaye amestaafu.
Baada ya kuingia madarakani Oktoba mwaka 2015, Rais Magufuli aliteuwa baraza lake la kwanza la mawaziri Desemba 10 mwaka huo likiwa na wizara 19.
Oktoba 7 mwaka jana, alifanya mabadiliko katika baraza hilo yaliyoliongeza ukubwa na kuwa na wizara 21.
KAULI YA NDUMBARO
Dk. Ndumbaro akizungumza na MTANZANIA alisema amepokea uteuzi huo kwa mikono miwili na anajiandaa kwenda kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema ni heshima kubwa sana kwani Rais kumwamini kwa muda mfupi aliokaa bungeni si kitu kidogo.
“Uteuzi ni heshima. Ni heshima kwangu, nimeupokea kwa mikono miwili na najipanga kutekeleza ilani ya CCM,” alisema.
Aidha, alisema taarifa ya kwanza kuhusu uteuzi wake aliipata kutoka kwa mke wake aliyempigia simu akiwa jimboni katika kikao cha kamati ya siasa.
“Mtu wa kwanza kunipigia alikuwa mke wangu akaniuliza umeona? Nikamwambia sijaona chochote na kweli nilikuwa sijaona kwa wakati huo, akasema umeteuliwa na Rais kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, basi nikatoka hapo nikarudi kuendelea na kikao na nilikuwa ‘very busy’.
“Baada ya uteuzi huo, imebidi nirudi sasa leo kwani katika ratiba zangu za kawaida ilikuwa nirudi Jumatatu, nilikuwa jimboni natumikia wananchi,” alisema Dk. Ndumbaro.
MAWAZIRI WALIOTUMBULIWA
Miongoni mwa mawaziri ambao uteuzi wao ulitenguliwa ni pamoja na Charles Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Machi 20 mwaka juzi Kitwanga aliingia bungeni na kujibu swali linalohusu wizara yake akiwa amelewa, kisha baadaye uteuzi wake kutenguliwa.
Mwingine ni Nape Nnauye (Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) aliyetumbuliwa siku moja baada ya kupokea ripoti kutoka kwa kamati aliyokuwa ameiunda kuchunguza sakata la kuvamiwa kwa Ofisi za Clouds Media Group.
Mei 24 mwaka jana, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi Profesa Sospeter Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Ingawa sababu haikuelezwa, lakini wakati akipokea ripoti ya makinikia, Rais Magufuli alimtaka Profesa Muhongo ajiuzulu kwa kushindwa kusimamia suala la mchanga wa dhahabu unaosafirishwa kwenye makontena.
Pamoja na hilo, Profesa Muhongo naye aliandika barua kwenda kwa Rais Magufuli akieleza kwamba amejiuzulu nafasi yake ya uwaziri kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyofanya uchunguzi wa makinikia.
Januari 19 mwaka jana, uteuzi wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu aliyekuwa akishughulikia walemavu, Dk. Abdallah Possi, ulitenguliwa na kuteuliwa kuwa balozi.
Septemba 7 mwaka jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya kutajwa katika ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na almasi iliyoonyesha namna Serikali ilivyopoteza matrilioni ya fedha kutokana na sababu mbalimbali.
Hatua hiyo ya kujiuzulu Simbachawene, ilikuja muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuwataka viongozi wote aliowateua ambao wametajwa katika ripoti hiyo wakae pembeni kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.
Kama ilivyokuwa kwa Simbachawene, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani naye alijiuzulu baada ya kutuhumiwa kutotekeleza majukumu yake kikamilifu alipokuwa akifanya kazi Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lenye dhamana ya kusimamia madini.
Pia Oktoba 7 mwaka jana, wakati alipofanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza idadi ya wizara, alitengua uteuzi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla.
Katika mabadiliko hayo, Mhandisi Ramol Makani naye aliachwa na nafasi yake ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ilichukuliwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga.
Mwingine aliyeacha ni Anastazia Wambura aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Juliana Shonza.
Julai mwaka huu, Rais Magufuli alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, na alimtupa nje aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola.
Akitaja sababu za kutengua uteuzi wa Mwigulu, Rais Magufuli alisema ni jinsi alivyoshindwa kushughulikia azimio la Bunge kuhusu suala la kufunga mashine za alama za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole (AFIS) katika vituo 108 vya polisi, mradi uliofanywa na Kampuni ya Lugumi kwa gharama ya Sh bilioni 37.
MAKATIBU WAKUU WALIOTUMBULIWA
Mbali na mawaziri, Rais Magufuli pia amekuwa akiwaacha baadhi ya makatibu wakuu wa wizara huku wengine akiwahamishia katika wizara mbalimbali.
Makatibu hao ni pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Jumanne Sagini na aliyekuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donald Mmbando.
Machi mwaka jana, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa siku chache baada ya kufanya ziara ya kushtukiza bandarini.
Mei mwaka jana, Rais Magufuli alitaja sababu za kumfuta kiongozi huyo kazi kuwa ni kutokana na kuieleza Kamati ya Bunge kiasi kilichokuwa katika makontena ya dhahabu ambacho hakikuwa sawa.