27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 60 ya Uhuru; Umaskini wapungua Tanzania

*Corona yaleta athari chanya kwa Tanzania

*Huduma jumhishi za kifedha, mapato vyaongezeka

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba amesema ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kiwango cha umaskini kimepungua kutokana na jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za msingi za jamii ikiwemo upatikanaji wa maji, umeme, huduma za afya, utoaji wa elimu msingi bila malipo.

Amesema kiwango cha umaskini na mahitaji ya msingi kimepungua hadi asilimia 25.7 mwaka 2020 kutoka asilimia 38.6 mwaka 1992.

Pia amesema takwimu zinaonesha kuwa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka 60  ya uhuru ulikuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali lakini haujawahi kufikia ukuaji hasi huku akidai  Nchi inajivunia kuingia uchumi wa kati.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Novemba 11,2021,kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara,Waziri Nchemba amesema Tangu uhuru, uchumi wa Tanzania umepitia katika nyakati mbalimbali za mafanikio ya kiuchumi pamoja na changamoto kadhaa.

Ameziataja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukame katika miaka ya mwanzoni mwa 1970 na 2012, mdororo wa uchumi wa mwaka 2008, vita vya Kagera mwaka 1978 pamoja na ugonjwa wa UVIKO mwaka 2020.

Hata hivyo, Serikali kupitia mikakati mbalimbali iliweza kujikwamua kutokana na magumu hayo iliyopitia na hii iliwezesha katika historia ya Tanzania kutokuwa na ukuaji hasi wa uchumi  tangu uhuru.

Sehemu ya Waandishi wa Habari.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka sitini ya uhuru ulikuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali lakini haujawahi kufikia ukuaji hasi.

Amesema wastani wa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha Serikali ya awamu ya kwanza (1967 – 1985) iliyoongozwa na mwasisi na Baba wa Taifa  Hayati Mwalim Juluis Kambarage Nyerere ulikuwa asilimia 3.1; Serikali ya awamu ya pili (1986 – 1995) asilimia 3.0, Serikali ya awamu ya tatu (1996 – 2005) asilimia 5.7, Serikali ya awamu ya nne (2006 – 2015) asilimia 6.3, na Serikali ya awamu ya tano (2016 – 2020) asilimia 6.5.

PATO LA TAIFA

Waziri huyo wa Fedha na Mipango amesema Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019 ambapo amedai sababu kuu ya kupungua kwa kasi ya ukuaji ni athari za hatua zilizochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani ambao ni washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania katika kukabiliana na janga la UVIKO-19.

“Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na mataifa hayo ni pamoja na kufunga mipaka, kusitisha safari za ndege za kimataifa na kusitisha baadhi ya shughuli za kiuchumi zinazohusisha mikusanyiko,”amesema waziri huyo.

Amesema hatua hizo zilisababisha uchumi wa dunia kuporomoka mwaka 2020 ambapo nchi nyingi zilikuwa na ukuaji hasi na kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni nchi 11 tu zilikuwa na ukuaji chanya kati ya nchi 45.

“Pamoja na kupungua kwa kasi ya ukuaji, Tanzania iliweza kuwa na ukuaji chanya kutokana na kutochukua hatua za kuzuia kufanyika kwa shughuli za kiuchumi isipokuwa kwa kipindi kifupi tu cha robo ya pili ya mwaka 2020 ambapo ilisitisha kwa muda baadhi ya shughuli zinazohusisha mikusanyiko ya watu kama shule, sanaa na burudani,”amesema.

UCHUMI WA KATI

Aidha,Waziri Nchemba amesema  Tanzania ilikuwa nchi ya kipato cha chini kwa miaka 59 tangu kupata uhuru hadi mwaka 2020 Benki ya Dunia ilipoitangaza kwa mara ya kwanza kuwa nchi ya Uchumi wa Kati wa Chini.

“Hii ni baada ya mageuzi makubwa ya kiuchumi yaliyofanyika ambayo yalipelekea wastani wa pato kwa mtu (Per capita GNI) kuvuka kiwango kilichowekwa na Benki ya Dunia cha dola za Marekani 1,036 kufikia dola za Marekani 1,100 mwaka 2019.

“Mwaka 2020, uchumi wa nchi nyingi duniani uliyumba lakini pamoja na kasi ya ukuaji wa Tanzania kupungua bado tulifanikiwa kubaki ndani ya kundi la nchi za kipato cha kati cha chini kwa wastani wa Pato kwa mtu la dola za Marekani 1,080.

“Tanzania iliingia katika kundi la nchi ya uchumi wa kati mapema zaidi ikilinganishwa na malengo ya Dira ya Taifa ya kufikia hadhi hiyo mwaka 2025.

“Hii ilitokana na matokeo chanya katika vigezo vya kiuchumi ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, utulivu wa thamani ya shilingi na mfumuko wa bei uliobaki katika wigo wa tarakimu moja kwa muda mrefu,”amesema.  

WASTANI WA PATO KWA MTU WAONGEZEKA  

Waziri Nchemba amesema wastani wa pato kwa mtu ulikuwa unaongezeka mwaka hadi mwaka kutoka wastani wa dola za Marekani 178.3 (1990 – 1995), wastani wa dola za Marekani 365 katika serikali ya awamu ya tatu, dola za Marekani 747 awamu ya nne, na wasatani dola za Marekani 1,010 awamu ya tano kwa kutumia kipimo cha Atlas cha Benki ya Dunia.

SEKTA YA FEDHA

Waziri Nchemba amesema hadi mwaka 2020, kulikuwa na benki na taasisi za fedha 55, kampuni za bima 32, kampuni za soko na mitaji 28 na mifuko ya hifadhi ya jamii 2.

“Kwa upande wa sekta ndogo ya fedha hadi Agusti 2021 kulikuwa na watoa huduma ndogo za fedha daraja la pili (Non deposite taking) 549, watoa ndogo za fedha daraja la tatu (SACCOSS) 460 na watoa huduma ndogo daraja la nne (Vikundi vya kijamii vya huduma dogo za fedha) 11,149.

 Jitihada hizo zimewezesha kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha kutoka asilimia 56 mwaka 2013 hadi asilimia 65 mwaka 2017 na inatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 75 mwaka 2022.

“Hii inaenda sambamba na mageuzi ya kiteknolojia yaliyowezesha kutumia mitandao ya simu za mkononi kuanzia miaka ya 2000 mwanzoni kufikisha huduma za fedha maeneo mengi nchini yakiwemo yale ambayo hayana matawi ya benki,”amesema.  

MWENENDO WA MAPATO YA NDANI

Amesema kulikuwa hakuna utaratibu wala mifumo madhubuti ya ukusanyaji wa mapato, katika serikali ya awamu ya kwanza iliweza kukusanya mapato ya ndani ya jumla ya shilingi milioni 5,557.3 kati ya mwaka 1966 – 1985.

Amesema  kiasi hicho kilichokusanywa katika kipindi hicho kilikuwa cha wastani wa asilimia 18.3 ya Pato la Taifa.

Amesema jitihada mbalimbali ziliendelea kuchukuliwa na serikali ili kuimarisha usimamizi wa mapato ikiwemo kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania mwaka 1997 na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

“Jitihada hizo zilizaa matunda ambapo mapato ya ndani yaliongezeka kufikia wastani wa shilingi milioni 130,853 katika kipindi cha awamu ya pili, wastani wa shilingi milioni 954,339 katika kipindi cha awamu ya tatu, wastani wa shilingi milioni 6,403,888 katika kipindi cha awamu ya nne, na wastani wa shilingi milioni 18,957,084 katika kipindi cha awamu ya tano,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles