Upendo Mosha – Siha
MAHAKAMA ya Wilaya ya Siha imemuhukumu kwenda jela kwa miaka 60, mkazi wa Kijijij cha Karansi wilayani humo, Abrahamu Kaaya(23), baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Karansi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Jasmine Abdul, alitoa hukumu hiyo jana baada ya kuridhika na ushahidi ulitolewa na mashahidi watano.
“Mahakama hii imemtia hatiani mshitakiwa Abrahamu Kaaya (23) kutokana na kupatikana na makosa mawili, la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 na ataenda kutumiki kifungo cha miaka 60 jela,”alieleza.
Alisema katika kosa la kwanza la ubakaji, mtuhumiwa amehukumia kifungo cha miaka 30 na kosa la pili la kumpa ujauzito mwanafunzi, amehukumia kifungo cha miaka 30 na vifungo vyote vitaenda kwa pamoja.
Alisema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo haukuwa na shaka yeyote.
Hakimu alisema alitoa hukumu hiyo ili iwefundisho kwa watu wengi ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo kama hivyo.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Simoni Feo, alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Octobar 11 mwaka 2017 katika Kijijiji cha Karansi.
Kabla ya kutolewa hukumu, mwendesha mashitaka aliomba mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshitakiwa kutokana na kukithiri vitendo hivyo iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hiyo.