NA ALOYCE NDELEIO,
JUMAPILI ijayo Februari 5, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977 ikiwa ni kipindi cha miongo minne ambayo kinaweza kuwa na mambo ya kujivunia lakini pia yakiwapo ambayo kimeyaondoa katika mstari wake.
Mambo ambayo kinaweza kujivunia ni pamoja na kwamba muda wote kimekuwa kikipata ushindi katika chaguzi za kisiasa ambazo kilisimama bila kuwa na kasha kasi ya upinzani.
Katika chaguzi za awali kabla ya kuundwa kwa CCM vyama mama vya TANU na Afro Shiraz (ASP) kila kimoja kwa upande wake kilikuwa kinapata ushindi na hali hiyo ikaendelea baada ya kuungana kwa vyama hiyo katika mwaka 1980, 1985 na 1990.
Hali hiyo kutokana na mtazamo wa kisiasa ni kwamba katika kipindi hicho mambo yalienda sawa kwa kile ambacho kinaweza kuelezwa kuwa chama kilikuwa kimeshika hatamu.
Hali kadhalika ni katika kipindi hicho kwamba chama kinapofanya uamuzi hakuna wa kuyapinga. Mara nyingine wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa uamuzi uliokuwa unafanyika ndani ya kipindi hicho upo uliowafurahisha watu na kuwahuzunisha wengine.
Wengine wanaona kuwa katika kipindi hicho chama kilikuwa na nguvu na mamlaka yalikuwa ndani ya chama na Serikali na si nje ya chama na Serikali. Kwa maana hiyo kuupinga uamuzi uliokuwa unafanywa na chama ilikuwa ni kupinga uamuzi uliopangwa na Serikali ambapo kwa lugha nyingine ni ‘totalitarianism’.
Pamoja na hali hiyo chaguzi ambazo TANU, ASP na baadaye CCM ilikuwa inashinda zilikuwa zinajulikana kuwa zinafanyika ndani ya demokrasia ya chama kimoja.
Baadaye mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi vya siasa ulirejeshwa nchini na hapo ndipo CCM ilianza kupambana na vyama vingine ambavyo baadhi ya viongozi wake walikuwa ni watumishi wa umma waliokuwa wameitumikia Serikali na chama katika mfumo wa chama kimoja cha siasa ambao waliamua kuunda vyama vya siasa ili kuleta ushindani.
Hata hivyo lengo la vyama hivyo vya siasa ilikuwa ni kuiondoa CCM madarakani kwamba malengo ya vyama vya siasa ni kutaka kushika dola. Hata hivyo katika chaguzi zilizofanyika mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 imeshuhudiwa CCM ikiwa inashinda lakini si kwa njia rahisi kama ilivyokuwa hapo awali chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa.
Ukweli unabakia kuwa CCM si malaika kwamba pamoja na ushindi huo yapo baadhi ya mambo kiliyoyachanganya hivyo kuifanya taswira yake ya mwanzo kuonekana kuwa si yenyewe.CCM ilijipambanua tangu mwanzo kuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi. Hilo lilikuwa ni vema na haki.
Hata hivyo taswira hiyo ilipakwa mkorogo kwani baadaye haikuwa rahisi tena kwa mfanyakazi au mkulima mdogo asiye na pesa za kukirimu watu aliyeweza kugombea nafasi yoyote ya uongozi na kuipata.
Hatua hiyo ikaifanya CCM kuonekana kuwa viongozi wanaotokana na CCM hawatoki katika kundi au jamii pana za wafanyakazi na wakulima bali kundi dogo sana la wafanyabiashara hasa matajiri. Tafsiri nyingine iliyotokeza hapa ikiwa ni kwamba CCM ni chama kinachowakumbatia wavuna jasho na kwamba kimewaweka wavuja jasho kando.
Ukweli unabakia kuwa CCM kiliasili mambo mengi mazuri yaliyokuwa yameasisiwa na waasisi wa vyama vilivyoungana ikiwa ni pamoja na kanuni, ahadi muhimu za MwanaCCM ambazo kwa uhalisia zililenga kujenga taifa lililo na usawa miongoni mwa wananchi.
Lakini leo hii ukianza kunyambua ahadi moja baada ya nyingine zote zimewekwa mkorogo na si asilia kama ilivyokuwa lakini bado wapo wanaodai na kujinasibu na ahadi hizo bila kujua kuwa kumekuwapo na ukengeukwaji katika kuzisimamia.
Kipindi cha miongo minne ya uwepo wake unaweza kubainisha kuwa kinatakiwa kusimamia uasilia wake kwa kufanya rejea misingi kanuni za wazazi wake TANU na ASP.