Na MWANDISHI WETU-ARUSHA
MHADHIRI Msaidizi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, Haliye Mabakwe (32),amepandishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na kusomewa mashtaka mawili, likiwemo la kuomba rushwa ya Sh 450,000 kwa wanafunzi ili awafaulishe katika mitihani ya marudio.
Jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Martha Mahumbuga,Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU),Richard Jacopiyo, alidai kosa la kwanza, ni mshtakiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa kati ya Septemba 9 na 15, mwaka huu, akiwa eneo la Tengeru chuoni hapo.
“Mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa chuo, aliomba rushwa ya shilingi 450,000 kutoka kwa mwanafunzi Joyce Deogratias ambaye alikuwa akikusanya na za wanafunzi wenzake wane wanaosoma chuoni hapo ili awasaidie kufaulu mitihani yao (Supplementary Exams),”alidai
Alidai shtakala la pili ni kujihusisha na vitendo vya rushwa, ambapo kati ya Septemba 9 hadi 15, mwaka huu alipokea rushwa ya Sh 449,000 kutoka kwa Joyce za wanafunzi wanne kwa lengo la kuwafaulisha kwenye masomo yao waliyofeli.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo, huku Wakili Jacopiyo akiomba mahakama kuahirisha shauri hilo kutokana na upelelezi wake kutokamilika.
Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana na Hakimu Mahumbuga kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 8, 2020, itakapotajwa tena.
Awali taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Takukuru mkoani hapa,Frida Wikesi ilidai mshtakiwa alikuwa akiwashawishi wanafunzi wake wa astashahada mwaka wa mwisho kumpatia rushwa ya fedha ili awafaulishe katika somo la Participatory Research Methods,ambalo yeye hufundisha.
“Uchunguzi wa Takukuru, umebaini mtuhumiwa alikuwa akiwaomba shilingi 50,000 kila mwanafunzi ambaye hakufaulu katika mitihani ya somo hilo,ushawishi aliokuwa akiufanya kupitia mwanafunzi huyo ambaye alikuwa akipokea fedha hizo kwa wanafunzi wenzake na kuzituma kwa mwalimu huyo kwa miamala ya simu na benki,”ilidai taarifa hiyo