30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mgumba: Tunakabiliana na uhaba wa magunia

RAMADHAN HASSAN, DODOMA

NAIBU Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba amekiri kuwepo kwa changamoto ya magunia ya kuwekea kahawa na kusema Serikali inaendelea kukabiliana nayo.

Mgumba alieleza hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), ambaye alidai kwamba kumekuwa na changamoto ya upatikanaji magunia kuwekea kahawa.

Nape alitaka kujua kuhusu msimamo wa Serikali, kuwa inasemaje kuhusiana na jambo hilo.

Akijibu, Mgumba alikiri kuna changamoto ya magunia ya kuwekea kahawa na alidai kwamba jukumu la kuagiza magunia ni la vyama vya ushirika.

Alisema mara baada ya kuona zoezi hilo linasuasua, Serikali imeingilia kati na kwa sasa yapo magunia milioni 2.4 bandarini ambayo yanatarajiwa kupakiwa na kupelekwa kwa wakulima.

“Magunia milioni 2.4 yapo bandarini, jana (juzi) wamepakia 278,000, leo (jana) tunapakia 255,000,” alisema Mgumba.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate (CCM) alitaka kujua nini mkakati wa Serikali kuhakikisha zao la kahawa linaongeza pato la taifa kwa ujumla.

Akijibu, Mgumba alisema Serikali ina mikakati mbalimbali ya kuhakikisha zao la kahawa linapata soko la uhakika na lenye tija kwa wakulima.

“Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi bora ya pembejeo, kuongeza uzalishaji kwa upanuzi wa mashamba ya wakulima kuzalisha miche bora ya kahawa yenye kuhimili ukame,” alisema.

Mgumba alisema sambamba na mikakati hiyo, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya masoko ya mazao ya kilimo, ikiwemo kahawa kwa kufanya utafiti wa mahitaji ya soko, kuimarisha vyama vya ushirika na kusimamia mikataba baina ya wanunuzi na wakulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles