27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Hekta 469,420 za misitu uharibiwa kila mwaka

ALLAN VICENT-Tabora

SERIKALI mkoani Tabora imesema hekta 469,420 za misitu uharibiwa kila mwaka nchini kutokana na shughuli za kibinadamu, hivyo hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa kupunguza kasi ya uharibifu huo.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Msalika Makungu, wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau wa mradi wa usimamizi shirikishi wa misitu ya miombo ya nyandakame Tanzania kutoka mikoa minne.

Alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wengine, kiwango cha uharibifu wa misitu ikiwemo ile ya miombo bado kiko juu, hivyo kusababisha kuwepo kwa tishio la kupotea kwa uoto wa asili.

Makungu alisema uharibifu wa misitu usipodhibitwa sasa, Serikali italazimika kutumia gharama kubwa kuurejesha na matokeo yake ni kizazi kijacho kushindwa kupata matunda ya asili kutokaa na uharibifu huo.

Alisema mradi huo umekuja wakati mwafaka ambapo wadau wanatakiwa kujiwekea malengo ya pamoja ili kutekeleza mkakati wa kuondoa uharibifu wa mazingira na kukabiliana  na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira unasababishwa na shughuli za kibinadamu zisizofuata utaratibu, ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, hivyo kila mdau anapaswa kusimamia ipasavyo misitu iliyopo katika eneo lake,” alisema.

Mwakilishi Mkazi wa Shirikika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) nchini, Jonathan Sawaya alisema mradi huo ni shirikishi, ambao utawasaidia wakulima maeneo ya vijijini ili watumie maeneo madogo kwa kuzalisha mazao mengi zaidi.

Alisema pia mradi huo utawawezesha wafugaji kuzingatia mbinu bora za ufugaji ambazo zitawawezesha kupata mifugo na mazao yake yenye ubora na ushindani katika masoko ya nyama, ngozi, maziwa, kwato na kadhalika.

Sawaya alisema matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya vijijini ni miongoni mwa mbinu shirikishi zitakazohusishwa katika mradi huo mikoa ya Tabora, Katavi, Songwe na Rukwa.

Mratibu wa mradi huo, Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Zainabu Bungwa alisema warsha hiyo ni muhimu sana kwani itachochea uhifadhi wa rasilimali misitu zilizopo hapa nchini.

Alibainisha kuwa wameshirikisha wadau kutoka mikoa yote ya nyanda kame, wakiwemo wakulima, wafugaji, maofisa wa Serikali, asasi za kiraia na wahifadhi wa mazingira wa mikoa hiyo ili kuibua shughuli zitakazowezesha uhifadhi endelevu wa miti ya miombo katika maeneo yao.

Zainabu alisema kuwa mradi huo utagharimu kiasi cha dola za Marekani bilioni 7.25 sawa na Sh bilioni 14 na kwa kuanzia wataanza kutekeleza mradi huo katika wilaya mbili za Kaliua mkoani Tabora na Mlele katika Mkoa wa Katavi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles