29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Mafanikio sekta ya mazingira, Muungano ndani ya miaka minne

MWANDISHI WETU

KATIKA kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, yapo mafanikio lukuki ya kujivunia yaliyopatikana kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo yamekuwa chachu kwa maendeleo katika kuhakikisha tunafikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Muungano wetu ni imara

Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuhakikisha kwamba, nchi yetu inaendelea kuwa yenye umoja, amani na usalama na Muungano wetu unaendelea kulindwa, kudumishwa, kuendelezwa na kuimarishwa. Kimsingi, yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano yaliyosaidia kuimarisha na kudumisha amani na utulivu wa Tanzania ambayo ni tunu muhimu na fahari ya nchi yetu. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:

Utatuzi wa changamoto za Muungano

Ofisi imendelea kuratibu utatuzi wa changamoto za Muungano ikiwa ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa maagizo na uamuzi wa Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano.

Katika kipindi hiki, vimefanyika vikao vya kujadili masuala ya Muungano katika ngazi ya Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mawaziri wa SMT na SMZ na kikao cha kamati ya pamoja ya SMT na SMZ.

Katika vikao hivyo, changamoto mbalimbali zilijadiliwa na kupatiwa ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili; VAT kwenye umeme unaouzwa na TANESCO kwa ZECO, changamoto za kibiashara ikiwamo gharama za kushusha mizigo (Landing Fees), uteuzi wa mjumbe wa Deposit Insurance Board (DIB), uteuzi wa mwenyekiti wa Tanzania Revenue Appeal Tribunal (TRAT), mwongozo wa ushirikishwaji wa SMZ katika masuala ya kimataifa na kikanda.

Hoja zingine ni upatikanaji wa fursa za ushiriki katika miradi ya maendeleo ya viwango na ubora wa bidhaa na maendeleo ya wajasiriamali. Aidha, changamoto zilizopo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi ni masuala ya fedha, uchukuzi, biashara na usajili wa vyombo vya moto.

Kuratibu masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa

Serikali ya Muungano inashirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Miradi na programu zinazotekelezwa pande zote za Muungano ni pamoja na  Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA), Mfuko Maendeleo ya Jamii (TASAF III), Uongezaji Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF) na Mradi wa Usimamizi wa Uvuvi Kanda ya Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) .

TASAF III imenufaisha wananchi wa pande mbili za Muungano ambapo ruzuku zinazotolewa kwa walengwa zimewasaidia kupata mahitaji ya msingi yakiwamo ya chakula, mahitaji ya shule kwa watoto na miradi midogomidogo ya kujiongezea kipato.

Aidha, MIVARF imeongeza thamani ya mazao yao, kuwajengea uwezo na kuwaunganisha na masoko, imewezesha upatikanaji wa huduma za fedha vijijini na uratibu wa programu na kwa maeneo yanayopitiwa na barabara zilizojengwa na programu hii, shughuli za kiuchumi zimeongezeka na hivyo kuongeza kipato kwa jamii inayozunguka eneo hilo.

Pia MKURABITA imeendelea kuandaa, kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mfumo wa kitaifa wa umiliki rasilimali na uendeshaji biashara utakaoboresha sheria, kanuni na taratibu za kijamii.

Mpango huu umekuwa na faida kwa wananchi kwani wameweza kurasimisha rasilimali na biashara wanazomiliki na kuzitumia kupata mitaji, mikopo na hatimaye kuongeza kipato.

Kupitia mradi wa SWIOFish umeandaliwa mwongozo wa kitaifa wa usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi kwa lengo la kuimarisha usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi pande mbili za Muungano.

 Ofisi ya Makamu wa Rais, inarataibu miradi mbalimbali ukiwamo wa kujenga uwezo wa jamii za pwani za kuhimili mabadiliko ya tabianchi ambao unajumuisha ujenzi wa ukuta eneo la Kilimani.

Pamoja na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji ya mvua katika Uwanja wa Mnazi Mmoja, eneo lililoathirika na tatizo la kudidimia kwa ardhi, Jang’ombe; Jimbo la Dimani (Kichaka Punda na Kibondeni); na mradi wa ujenzi wa ukuta na upandaji wa mikoko – Kisiwa Panza.

Kuimarika kwa ushirikiano

Ushirikiano wa Serikali hizi mbili kwa masuala yasiyo ya Muungano umeimarika kwani zimeweka utaratibu wa vikao vya kisekta kwa wizara, idara na taasisi zisizo za Muungano ambavyo vinajadili masuala ya kisekta ikiwamo kubadilishana ujuzi, utaalamu na uzoefu kupitia mafunzo, masuala ya sera na ushiriki katika masuala ya kimataifa ili kuleta ufanisi na uwiano wa maendeleo kwa pande mbili.

Katika kipindi cha Novemba, 2015 hadi Septemba, 2019, sekta zilizokutana ni nishati, maji, madini, uchukuzi, utumishi na utawala bora, viwanda na biashara, maliasili na utalii, afya, kilimo, habari, utamaduni, sanaa na michezo. Ardhi, fedha na mipango, mazingira na tawala za mikoa na serikali za mitaa.

Elimu ya muungano

Ofisi imeendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu na faida zinazotokana na Muungano kupitia redio, televisheni, magazeti na maonesho. Pamoja na elimu iliyotolewa kwa njia ya vyombo vya habari, ofisi pia iliandaa kongamano la vijana kuhusu fursa zilizopo katika Muungano ambalo lilifanyika Zanzibar, warsha ya wanafunzi wa shule za msingi zilizopo na kongamano la vyuo vya elimu ya juu zilizofanyika Dodoma.

Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano, kumekuwapo mafanikio makubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa pande zote mbili za Muungano. Dhamira ya Serikali zetu mbili ni kuuimarisha Muungano ili uendelee kudumu kwa faida yetu na vizazi vijavyo. Aidha, Serikali  zetu zitaendelea kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na umoja, amani, utulivu na usalama.

Hifadhi na usimamizi wa mazingira

Katika sekta ya mazingira likiwamo katazo la mifuko ya plastiki, ujenzi wa miundombinu muhimu kwa ajili ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali, usimamizi na uzingatiaji wa sheria ya mazingira na kuridhia kwa mikataba ya kimataifa kuhusu mazingira.

Katazo mifuko ya plastiki

Aprili 9, 2019, Serikali ilitangaza kupiga marufuku uingizaji, uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini ifikapo Juni mosi, 2019, ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa kanuni za kupiga marufuku mifuko ya plastiki za mwaka 2019, ili kuhakikisha kunakuwa na nguvu ya kisheria.

Aidha, iliunda kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu usimamizi wa katazo hilo, Aprili mwaka huu, ambacho kinajumuisha wajumbe zaidi ya 30 kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.

Katazo limepokewa vizuri na tathmini inaonesha kaguzi zilizofanywa katika maeneo mengi zimebaini kutokuwapo kwa uzalishaji, uuzaji wala matumizi ya mifuko ya plastiki na wananchi wameanza kutumia mifuko mbadala ikiwamo ya karatasi, vikapu, vitambaa na non-woven.

Katazo la mifuko ya plastiki limeleta fursa kwa kuwezesha wananchi kupata ajira kwa kushiriki kuzalisha mifuko mbadala hivyo, kujitengenezea kipato na kukuza uchumi kwa ujumla.

Kuridhiwa kwa mikataba na itifaki

Kutokana na umuhimu wa hifadhi ya mazingira, ofisi ya Makamu wa Rais imewasilisha azimio la kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu kemikali ya Zebaki na Mkataba wa ziada ya Nagoya – Kuala Lumpar.

Faida za kuridhia mkataba huu ni kulinda afya ya binadamu dhidi ya madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na Zebaki pamoja kuhakikisha taka za Zebaki zinasimamiwa kikamilifu kwa kuzingatia miongozo chini ya Mkataba wa Basel unaodhibiti usafirishaji na utupaji wa taka hatarishi baina ya nchi.

Kwa upande wa Itifaki ya Nagoya itasaidia juhudi za kuhifadhi mazingira na matumizi endelevu ya bioanuai kwa kutambua madhara yanayoweza kutokea katika afya ya binadamu, mazao au bidhaa zilizofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki kwa njia ya bioteknolojia ya kisasa.

Faida za kuridhia itifaki ya ziada ni kurahisisha uwajibishaji kisheria na upatikanaji wa fidia kutoka kwa kampuni au wafanyabiashara wa nchi nyingine au wanachama wake ambao wameingiza mazao au bidhaa zilizofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki, endapo matumizi yake yataleta madhara kwa afya ya binadamu na mazingira hapa nchini.

Miradi ya usimamizi kemikali na kanuni za taka hatarishi

Ofisi ilitekeleza mradi wa kujenga uwezo wa kitaasisi katika usimamizi wa kemikali na taka nchini wenye thamani ya Dola za Marekani 235,000 kwa ufadhili wa Mfuko wa Dhamana ya Mazingira Duniani (GEP) kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Ilitoa mafunzo kwa mamlaka za udhibiti katika sekta ya mafuta na gesi kwa maafisa 105 kuhusu usimamizi wa kemikali pamoja na kuandaa kanuni za udhibiti na usimamizi wa zebaki. Jumla ya maafisa 282 kutoka mamlaka za udhibiti, sekta ya kilimo na serikali za mitaa wamepatiwa mafunzo hayo.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa kanuni mpya za usimamizi wa taka hatarishi za mwaka 2019 kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira zilizotangazwa katika gazeti la Serikali na kupewa G.N 676.

Kanuni hizi mpya za mwaka 2019 zimeweka adhabu kali zaidi ukilinganisha na Kanuni za mwaka 2009 kwa makosa ya kutokuwa na kibali cha kusimamia taka hatarishi nchini. Adhabu hizo ni faini kuanzia milioni tano hadi bilioni kumi au kifungo kisichozidi miaka kumi na mbili au vyote kwa pamoja.

Miradi iliyopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi, ofisi inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ukiwamo wa kuhimili athari ya mabadiliko ya tabianchi kupitia mifumo ya ikolojia lengo likiwa ni kuongeza uvumilivu wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii za vijijini.

Wilaya zilizonufaika ni Mvomero (Morogoro), Simanjiro (Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpwapwa (Dodoma) na Kaskazini A, (Unguja) na thamani ya mradi ni Sh 936,235,700.00. Wananchi katika maeneo ya mradi wanajifunza njia mbalimbali (mfano: kilimo rafiki kwa mazingira za kujipatia mahitaji katika hali inayobadilika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, mradi wa kusaidia kujenga uwezo wa taasisi na jamii kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo ya kaskazini mwa nchi, unalenga kujenga uwezo wa jamii kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo kame ya Wilaya za Same na Mwanga (Kilimanjaro). Mradi huu unajenga vituo viwili vya hali ya hewa kwa wilaya za Same na Mwanga, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Jipe na Makuyuni katika Wilaya ya Mwanga. Ukarabati wa mita 1,800 za mfereji wa asili wa umwagiliaji katika Kijiji cha Mabilioni, Wilaya ya Mwanga.

Mradi wa kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame Tanzania, unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, yaani 2017 hadi 2022, lengo likiwa ni kuboresha mifumo ya ikolojia ya kilimo ambayo itawezesha kuongeza uzalishaji wa chakula na kuchangia moja kwa moja kuboresha mazingira.

Kupitia mradi huu, mpango wa matumizi bora ya ardhi ya vijiji 17 Tanzania Bara katika wilaya za Magu, Mkalama, Nzega na Kondoa umeandaliwa na kwa upande wa Zanzibar Shehia nane zilizopo Wilaya ya Micheweni, Pemba zipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji. Kukuza uelewa katika upangaji na usimamizi wa matumizi bora ya ardhi.

Mradi mwingine unaosimamiwa na ofisi ya makamu wa rais ni mradi wa usimamizi endelevu wa ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa unaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu yaani 2018-2021. Lengo likiwa ni kukuza uwezo wa usimamizi na matumizi endelevu wa ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa.

Mradi huu umesaidia kukuza uelewa kwa madiwani na maafisa ardhi wa vijiji husika juu ya matumizi endelevu ya ardhi na maliasili kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo husika, kukuza uelewa juu ya mpango wa matumizi ya ardhi, hifadhi ya mazingira na maliasili kwa wanavijiji.       

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles