AMON MTEGA-SONGEA
MKAZI A wa Mtaa wa Kibulang’oma Manispaa ya Songea, Mwajuma Mfaume (23), ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kumsaidia kupatiwa matibu ya maradhi ya kuugua mgongo ambao unakidonda kikubwa miaka miwili sasa.
Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, alisema maradhi hayo yalimkuta Septemba, 2017 saa 8 usiku akiwa amelala chumbani kwake.
Alisema akiwa amelala, alijisikia mgongo unawaka moto na alipoamka na kuugusa alikuta ngozi yote imenyofoka, huku akisikia maumivu makali.
Alisema baada ya tukio hilo, mama yake mzazi Fatuma Bashiru alimpeleka Hospital ya Misheni Peramiho ambako alitibiwa bila kupata mafanikio ya ugonjwa huo na hatimaye wakamrudisha nyumbani.
Alisema wakiwa nyumbani, walishauriwa na majirani waende Hospitali ya Rufaa ya ya Mkoa wa Ruvuma na walipofika walianza tena matibabu ambapo kidonda kilikuwa kikisafishwa kwa gharama ya Sh 45,000, lakini mwisho wa siku walishindwa kumudu garama hizo kutokana na kidonda hicho kutokuonyesha dalili za kupona.
“Nina maumivu makali, nalala kifudifudi muda wote, mama yangu anapata taabu namna ya kunihudumia,nimeambiwa kidonda kioshwe kwa dripu la maji ambalo hugarimu shilingi 2,500 kila baada ya siku moja,fedha hizi mama yangu hana ,maana ana mzigo mkubwa wa kuniuguza mimi,”alisema.
Mama mzazi Fatuma, alisema amehangaika na mwanaye kufanikisha matibabu kwa kuomba misaada mbalimbali, lakini hajafanikiwa .
Alisema waliwahi kupata kibali cha Ofisa Mtendaji wa Kata ya Lizaboni kilichotolewa Novemba 27, mwaka huu apite kuomba fedha kwa wafanyabiashara wa maduka jambo ambalo alishindwa kutokana na kukosa muda wa kufanya hivyo.
Katika hatua nyingine, aliwaomba a watu wenye kuguswa na hali ya mwanae basi waweze kumtafuta kwa namba ya simu ya kiganjani ,0653-543498.