Lilian Justice, Morogoro
MGOGORO wa kugombania ardhi umeibuka katika Kijiji cha Kongwa Kata ya Mvuha, wilayani Morogoro huku watu kadhaa wakijeruhiwa kwa mapanga.
Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa, umekuwa ukichukua sura mpya kila kukicha ambapo jana yaliibuka mapigano ya kugombania mpaka kati ya wananchi wa vijiji vya Kongwa na Dala.
Katika ugomvi huo watu zaidi ya 10 wamejeruhiwa na kukimbizwa katika Kituo cha Afya cha Duthumi, huku wengine wakihofiwa kupoteza maisha.
Wakizungumza na MTANZANIA baadhi ya wananchi ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini, walisema mgogoro huo umesababisha wananchi wa Kongwa kuingia katika mashamba ya Kijiji cha Dala kwa ajili ya shughuli za kilimo, huku wenzao wakipinga hatua hiyo.
Waliojeruhiwa kwenye mapigano hayo wametajwa kuwa ni Hamis Lukambala, Mohamed Kibali, Omary Lugeni na Adam Lugeni ambao walikatwa mapanga katika sehemu za kichwani, mabegani na mikononi na wote wanadaiwa kuwa na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi.
Akizungumzia hali hiyo Mwenyekiti wa muda wa Kijiji cha Kongwa, Hassan Semndili, alikiri kutokea kwa mapigano hayo jana asubuhi.
“Ni kweli kuna mapigano ambayo yamesababisha watu kuumia sana, yametokea leo (jana) saa 5 asubuhi baada ya wananchi wa kijiji changu cha Kongwa wakiwa wanaendelea na shughuli zao za kilimo kwenye mashamba yao ghafla lilitokea kundi la watu kutoka Kijiji cha Dala na kuanza kuwajeruhi kwa mapanga na fimbo.
“Wakati haya yakiendelea hata wale waliovamiwa wasingeumia lakini lile kundi la wananchi wa Dala walikuwa wakishinikizwa na mwenyekiti wao wa kijiji kuwa wafanye unyama huu jambo ambalo sisi kama viongozi tunatakiwa kuleta amani na si kuleta mgogoro kama hivi. Leo wananchi wangu wanne hali zao ni mbaya sana,” alisema Semndili.
Mwenyekiti huyo alimwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kufika kijijini hapo ili aweze kumaliza mgogoro huo ambao umekuwa ukisababisha ulemavu kwa watu.
“Huu mgogoro ulianza tangu mwaka 2010 na ilipofika mwaka 2013 wananchi wa vijiji vyote viwili tulikubaliana kufuata sheria ya kuheshimu mpaka wa kila eneo lakini bado wenzetu inaonekana hawako tayari na kila mara tumekuwa tukishuhudia hali kama hii,” alisema
Hata hivyo alisema tatizo hilo liliendelea kukua baada ya uongozi wa Kijiji cha Dala kuendelea kugawa ardhi kwa wawekezaji wakubwa wakiwamo viongozi wa serikali bila kufuata utaratibu.
‘’Baada ya Kijiji cha Dala kugawa eneo kubwa kwa mwakezaji bila ya makubaliano kati ya vijiji hivyo viwili ndipo mgogoro ulipozidi kukua,’’ alisema Semndili.
Alisema baada ya kuona mgogoro huo unazidi kushamiri ilipelekea kufanyika kikao cha Baraza la Maendeleo la Kata, na kuitisha mkutano mwaka 2017 kwa kushirikisha Serikali za vijiji vyote viwili.
“Maamuzi yaliyotolewa ni pamoja na vijiji vyote kuachana na makubaliano na kufuata sheria ili kuweza kutatua tatizo la mpaka sambamba na uongozi wa kata kwenda Wizara ya Ardhi ili kuchukua ramani na maofisa Ardhi kupima upya eneo hili kisheria,” alisema mweyekiti huyo.
Alisema baada ya makubaliano hayo na upimaji kufanyika kuliweza kuwekwa jiwe la mpaka kati ya Kijiji cha Dala, Kongwa na Lukulungu liliopo eneo la Kwamnyone lenye nambari BAH 975 mnamo mwaka 2017 lakini bado kumekuwepo na mgogoro mkubwa wa kugombani mpaka unaofanywa na wananchi wa Dala ambao bado wamekuwa wakigawa ardh kiholela.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Dala, Boi Lubegete, alikanusha kuhusika katika mgogoro huo na kueleza kuwa yeye hajahusika kushinikiza mapagano hayo kama inavyodaiwa.
“Mimi sijahusika kwa namna yotote ile kushirikiana na wananchi wangu, ama kushinikiza wananchi wa Kongwa kupigwa bali kila mara huwa nasisistiza amani na sio vinginevyo,’’ alisema Lubegete.
Alisema kilichosababisha mgogoro huo uliosababisha watu kuumizana ni baada ya wananchi wa Kijiji cha Kongwa kuingiza matrekta shambani katika kijiji cha Dala na hivyo wananchi wakashindwa kuvumilia.
KAULI YA MKUU WA MKOA
MTANZANIA ilipomtafuta Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk, Kebwe Steven, alikiri kutokea kwa mapigano hayo na kusema hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha.
“Hakuna mauaji yoyote yaliyotokea bali taarifa nilizopokea ni kwamba watu wawili wamejeruhiwa kutokana na mgogoro wa kugombani mpaka katika Kijiji cha Kongwa na Dala wilayani Morogoro,” alisema.
Dk. Kebwe alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imeanza kufanyia kazi mgogoro huo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuanza uchunguzi na tayari ameagiza Diwani wa Kata ya Mvua, Mfaume Chanzi (CCM), kufika haraka ofisini kwake ili kueleza mgogoro huo.
Alisema mkutano huo utawahusisha maofisa ardhi na wananchi wa vijiji vyote viwili ikiwezekana vijiji hivyo viweze kupimwa upya jambo ambalo litawasaidia kujua mwisho wa mpaka husika kama njia ya kukomesha kutokea mapigano ya mara kwa mara kwa ajili ya mpaka wa vijiji hivyo.
“Mkulima wa Kijiji cha Kongwa hazuiliwi kulima shamba Dala kama ana eneo lake kule lakini kinachotakiwa kufanyika ni mkulima kufuata utaratibu wa kijiji husika anakofanyia shughuli za kilimo na hiyo itaondoa migogoro isiyo ya lazima,’’ alisema.