Na FREDERICK KATULANDA-GEITA
SERIKALI imeufunga Mgodi wa RZ Union uliopo mkoani Geita kwa siku tano ili kupisha ukaguzi maalumu wa timu ya watalaamu, nayoongozwa na Kamishna wa Madini, Alli Samaje.
Agizo hilo, limetolea na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, juzi wakati akizungumza na wananchi, baada ya wachimbaji 15 kuokolewa kutoka shimoni wakiwa hai.
Alisema baada ya kutokea ajali hiyo, mlango wa mgodi huo ulifukuliwa na kuharibu sura yake ya awali, hivyo lazima mgodi huo ufanyiwe ukaguzi kabla ya kuruhusiwa kuendelea.
“Siku tano (kuanzia jana), Kamishna wa Madini na watalaamu wengine wahamie hapa kwa ajili ya ukaguzi wa kina kuhusu usalama kabla ya kuendelea na shughuli zao ili kujiridhisha kama utakuwa salama,” alisema.
Naibu waziri huyo aliagiza ukaguzi wa awali ufanyike, iwapo aliyeukagua alishauri vyema na ikibainika kama hakutimiza wajibu wake, hatua zichukuliwe dhidi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji wa mgodi huo, Francis Kiganga alisema wamesitisha uzalishaji wao kupisha ukaguzi na wako tayari kupokea maelekezo ya Serikali.
“Kamishna wa Madini, ataanza ukaguzi nadhani akikamilisha ukaguzi wake tutapewa maelekezo hivyo tunangoja katika kipindi hicho cha ukaguzi kupokea maelekezo hayo na kutekeleza,” alisema.
Ukaguzi waanza
Katika kutekeleza agizo hilo, Kamishna Samaje jana aliwasili mgodini hapo saa 7 mchana kwa ajili ya kuanza ukaguzi wake.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Mkazi wa Madini wa Mkoa wa Geita, Ally Said alisema tayari Samaje alikuwa katika eneo la tukio.
“Nitazungumza naye baadae, sasa yupo kwenye ukaguzi na akikubali nitawafahamisha waandishi mkutane naye maana yeye ndiye anaweza kueleza suala la ukaguzi huu,” alisema.
Wachimbaji watoka Hospitali
Wakati huo huo, wachimbaji hao waliofukiwa na kifusi na kukaa siku nne wamerejea kazini kwao tayari kwa ajili ya kuanza kazi wakingoja ukaguzi wa Serikali kukamilika.
Hii ni baada ya madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Geita kuthibitisha kuwa wachimbaji hao wapo salama.
Akizungumza hospitalini baada ya kuruhusiwa, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga alisema afya za wachimbaji hao zimeimarika na wako salama na kuwataka warejee kwenye majukumu yao ya kila siku.
“Kilichowatokea ni ajali kazini, madaktari wanasema mpo salama sasa mnaruhusiwa leo kutoka hapa hospitalini na mtakwenda kuendelea na majukumu yenu hivyo niwatakie utendaji kazi mwema,” alisema.
Akizungumzia afya ya wachimbaji hao Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Brian Mawala alisema watu hao wako katika hali nzuri, baada ya kukaguliwa kitabibu kwa siku ya juzi na jana na wameridhika kuwa hawana shida nyingine yoyote, hivyo wanaweza kuendelea na kazi.
DC ataka wapewe mikataba
Kutokana na hatua hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi aliuagiza mgodi huo kuwapatia mikataba ya ajira wachimbaji hao waliofukiwa ili kuwapa uhakika wa ajira zao kutokana na kubaini kuwa wawakifanya kazi kwa mkataba wa miezi mitatu.
“Nimezungumza na wajiri wenu juu ya ajira yenu, tumekubaliana awapatie mkataba na wamekubali wote mtapata mkataba wa muda mrefu, hivyo zaidi ya hapo kuna fedha ambazo zilitolewa na wadau kwa ajili yenu sasa tutazungumza niwafahamishe ni kiasi gani na kesho nitawaletea wote kila mmoja asaini kupokea na kisha nitatangaza.
Mgodi
Katika hatua nyingine Msemaji wa Mgodi wa RZ Union, Francis Kiganga alisema mgodi huo ambao umeanzishwa Julai, 2013, ulikuwa ukichimbwa mawe kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya kuanza uzalishaji hapo Juni mwaka huu.
Alisema walikuwa katika hatua za ukamilishaji wa ujengaji wa kinu cha kusagia mawe, ikiwa ni pamoja na mtambo wa kuzalisha dhahabu (CP) ambao ulikuwa ukiendelea kujengwa.