Na MWANDISHI WETU- TABORA
MWENYEKITI wa taasisi inayojishughulisha na utawala bora ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja, amesema kauli ya Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Abdallah Bulembo, kwamba alipewa Sh milioni 40 na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ili amsaidie kupata ushindi katika jumuiya ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi mwaka 2014, haina ukweli wowote.
Mgeja alitoa kauli hiyo mjini hapa jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari akiwa njiani kuelekea mkoani Kigoma.
“Kauli ya Bulembo ni ya kumdhihirishia Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, kwamba rushwa ndani ya CCM imeota mizizi na haiepukiki katika uchaguzi ndani ya chama hicho.
“Kauli ya Bulembo inaonyesha kwamba, hata yeye alipopata nafasi ya uenyekiti wa wazazi Taifa, alitumia mamilioni ya fedha mwaka 2014.
“Kwa mtu aliye makini, hawezi kuamini kwamba Lowassa alimpa fedha ili zimsaidie kwenye kampeni bali Bulembo anachofanya sasa ni propaganda ya mwendelezo wake wa kila siku wa kumdhalilisha, kumdhihaki, kumtukana na kumkejeli Lowassa.
“Lakini kama anaamini Lowassa alimpa fedha hizo, basi awataje majina watu wengine waliompa msaada wa mamilioni ya fedha kwa ajili ya uchaguzi huo.
“Nasema hivyo kwa sababu tatizo la rushwa ndani ya CCM siku zote limekuwa donda ndugu na limeisababisha CCM kupoteza mvuto wake wa asili kwa wananchi.
“Nasema hivyo kwa sababu ile falsafa ya CCM ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi haipo na ilishatoweka siku nyingi na kinachoangaliwa sasa ni kwa mwenye fedha kuchukua madaraka na si vinginevyo,” alisema Mgeja.