LIRA, UGANDA
ALIYEKUWA mtumishi wa umma nchini hapa Charles Obong amezikwa na zaidi ya Sh milioni 200 za Uganda ambazo ni sawa na Sh milioni 120 za Tanzania, ili akamhonge Mungu asipewe hukumu kali atakapokutana naye.
Obong mwenye umri wa miaka 52 aliyefanya kazi katika Wizara ya Utumishi wa Umma tangu mwaka 2006 hadi 2016, alichanga fedha hizo na kuzihifadhi kwa lengo hilo wakati akiwa hai.
Alifariki dunia Desemba 17 mwaka jana baada ya kuugua kwa muda mrefu na kuzikwa bomani kwake katika Kijiji cha Adag-ani, kaunti ndogo ya Aromo iliyo Wilayani Lira wakati wa mkesha wa Krismasi.
Alizikwa kwa jeneza la chuma linalokadiriwa kugharimu Sh milioni 20Â za Uganda sawa na Sh milioni 12 za Tanzania.
Shemeji yake, David Elic alisema marehemu aliacha wosia kuwa atakapofariki dunia, mke wake Margaret Obong aweke kiasi kikubwa cha fedha ndani ya jeneza lake.
Alipanga kupeleka fedha hizo kwa Mungu ili amsamehe dhambi zake na kumwepusha na adhabu ya jehanamu bali apate uzima wa milele.
Inadaiwa alimwambia kaka yake, Justin Ngole na dada yake Hellen Aber wawe mashahidi kuhakikisha mke wake anatimiza agizo lake hilo kikamilifu.
Wizara alimofanya kazi ni miongoni mwa zile zinazokumbwa na kashfa kubwa za ufisadi nchini hapa na mabilioni ya fedha yamewahi kupotelea mifukoni mwa watumishi wa umma.
Hata hivyo wiki iliyopita, Mzee wa Ukoo wa Okabo, Mike Gulu aliagiza mwili wake ufukuliwe na fedha hizo zikatolewa na kuhifadhiwa kwingine kwa sababu anaamini ni mwiko kuzika watu na fedha.