27.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

MFUNGWA ALIYESAMEHEWA NA RAIS AKOSA MAKAZI

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA


MFUNGWA aliyepata msamaha wa Rais John Magufuli, Jimson Fungo, amekosa makazi ya kuishi kwa kushindwa kuwapata ndugu zake baada ya kutolewa gerezani.

Fungo mwenye umri wa miaka (48), mzaliwa wa Makete mkoani Njombe, alikuwa akiishi katika eneo la Isanga jijini Mbeya, akiwa na familia yake akiwamo mama mzazi na watoto wake wawili hadi mwaka 1995 alipohukumiwa kifungo cha miaka 30 na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, baada ya kukutwa na kosa la kuua bila kukusudia.

Desemba 22, mwaka jana, alitolewa gerezani kupitia msamaha huo wa rais, lakini baada ya kufika kwenye makazi yake ya awali huko Isanga, hakuwapata ndugu zake wala kuiona nyumba aliyokuwa akiishi.

Hata hivyo, ilibainika baadaye kwamba nyumba zilizokuwa katika eneo hilo zilibomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara miaka kadhaa iliyopita.

Fungo amekaa gerezani kwa miaka 22 na alianzia kifungo chake kwenye gereza la Ruanda jijini Mbeya kabla ya kuhamishiwa gereza la Mlowo mkoani Songwe, baada ya mahakama kumkuta na kosa la kuua bila kukusudia.

 

Katika mahojiano na gazeti hili, Fungo anaonyesha kujutia na kusikitishwa na hukumu hiyo ambapo alisema kuwa kilichomtokea ni bahati mbaya baada ya kupigana na rafiki yake ambaye hakumtaja jina na kusababisha kifo chake.

Kutokana na kushindwa kuwapata ndugu zake hasa ikizingatiwa kuwa hana mawasiliano yoyote na familia yake, Fungo kwa sasa analazimika kulala kituo kikuu cha mabasi ya mikoani jijini Mbeya na kunapokucha huanza kuzurura mitaani kuomba msaada wa chakula kwa wahisani.

Fungo ni miongoni mwa wafungwa waliopata msamaha wa rais hivi karibuni kutokana na kukidhi vigezo vya kisheria vya kupewa msamaha huo kwa sababu afya  yake ilidhoofika sana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles