NA KOKU DAVID-DAR ES SALAAM
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea na mikakati yake ya kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wote wa ndani na nje ili waweze kufanya biashara bila usumbufu ili kulipa kodi stahiki kwa hiari kwa mujibu wa sheria.
Moja ya mkakati wake ni kuanzisha mfumo wa Kielektroniki wa Dirisha Moja la Huduma (Electonic Single Window System) ambao utamuepusha na usumbufu wa kutumia muda mwingi katika kufuatilia vibali vya mzigo na badala yake huduma zote atazipata katika sehemu moja.
Katika kuhakikisha mpango wa uanzishwaji wa mfumo huo unafanikiwa, hivi karibuni TRA ilikutana na wadau mbalimbali kutoka taasisi za Serikali zinazotoa vibali na binafsi ili kupokea maoni yao ambayo yatafanikisha uanzishwaji wake.
Matumizi ya Dirisha Moja la Huduma yanatarajiwa kuboresha huduma kwa wafanyabiashara, ikiwa ni pamoja na kuwaondolea changamoto waliyokuwa wakikutana nayo ya mizigo kukaa muda mrefu bila kushughulikiwa kutokana na kukosa vibali.
Mfumo huo unaotarajiwa kuanza kutumika mwaka 2018, pia utapunguza changamoto ambazo zinaukabili mfumo wa sasa wa Uingizaji na Uondoshwaji wa Mizigo katika vituo vya forodha (TANCIS) ambao unashindwa kufanya kazi kwa haraka, hali inayosababisha mizigo kuchelewa kutolewa kutokana na muda mwingi unaotumiwa na wamiliki kufuatilia vibali.
Kupitia mfumo huo, wafanyabiashara hawatakuwa wakienda kwenye idara na taasisi za Serikali na badala yake wakiwa kwenye ofisi zao wataweza kuomba na kupata vibali, ikiwa ni pamoja na kupata bili za malipo ambazo watatakiwa kwenda kuzilipia benki kutokana na kuwa mfumo utakuwa ukifanya kazi na benki.
Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kutumia mfumo huo ambao unatumiwa na mataifa mbalimbali kwa lengo la kurahisisha huduma kutolewa kwa haraka hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa dunia imekuwa ikienda na teknolojia ya kisasa.
Mfumo unaotumika sasa, ili mtu aweze kupata kibali atalazimika kutembelea taasisi husika zaidi ya mara 10 kutokana na kuwa  baadhi ya ofisi hutaka vibali zaidi ya kimoja, lakini kwa kutumia mfumo huo muda utapungua.
Kwa sasa taasisi za Serikali zinazotoa vibali zipo 47 lakini mfumo wa dirisha moja la huduma utakuwa na taasisi 32 ambazo kwa pamoja zitakuwa zikitoa vibali 106.
Kabla ya mfumo huo, mifumo iliyoanzishwa katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2015 ili kutekeleza jukumu la kufanya maboresho na kurahisisha taratibu za uingizaji na utoaji mizigo ndani na nje ya nchi pamoja na upitishaji mizigo kwenda nchi jirani, ni Electronic Cargo Tracking System (ECTS) ambao uliundwa ili kufuatilia mizigo ipitayo katika Bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi jirani na ulisaidia kuondoa tatizo la ukwepaji wa kodi kwa mizigo iliyokusudiwa kupelekwa nchi jirani.
Mfumo mwingine ni ule wa Kielektroniki wa ulipaji Kodi (Revenue Gateway System) ambao ulianzishwa mwaka 2013 ambao unawasiliana na Benki Kuu pamoja na benki za kibiashara na kumwezesha mlipakodi kufanya malipo ya kodi mbalimbali kupitia benki au kwa kutumia simu ya kiganjani akiwa mahali popote na hivyo kumuondolea usumbufu, pia mfumo huu unawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za mapato ya Serikali kwa wakati.
Kwa upande wa mfumo wa kielektroniki wa Forodha (TANCIS) ambao ulianzishwa mwaka 2014, unatumika kuthaminisha mizigo na kukadiria kodi ili kodi sitahiki ilipwe pamoja na kuratibu shughuli za uondoshwaji mizigo maeneo ya forodha.
Mifumo hiyo imewezesha kuongeza mapato ya Idara ya Forodha kutoka wastani wa Sh trilioni 3.4 mwaka 2013/14 hadi Sh trilioni 5.2 kwa mwaka 2015/16.