-Na FARAJA MASINDE
UKUBWA wa Mifuko ya Uwekezaji umeongezeka kutoka Sh bilioni 290.7 Juni 30, mwaka jana hadi kufikia Sh bilioni 412.8, Juni, mwaka huu.
Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya UTT AMIS, Casmir Kyuki wakati akiwasilisha taarifa yake kwenye Mkutano Mkuu wa wawekezaji wa Mfuko wa Umoja uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.
Kyuki alisema ongezeko hilo la Sh bilioni 122.1 ni sawa na asilimia 42 ukilinganisha na pungufu ya Sh bilioni 4.4 sawa na asilimia hasi 1.5 kwa mwaka uliopita.
“Kiwango hiki cha ukuaji wa mfuko ndani ya mwaka mmoja kimefikiwa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mifuko ya uwekeji wa pamoja na kampuni ya uwekezaji ya UTT AMIS pamoja na taasisi zilizotangulia.
“Ukuaji wa mifuko pia unadhihirishwa na ongezeko la idadi ya wawekezaji 13,671 sawa na asilimia 9.4 ukilinganisha na ongezeko la wawekezaji 5,169 sawa na asilimia 3.7 mwaka uliopita.
“Kwa mwaka huu wa fedha pato la wawekezaji wa mifuko ni zuri kwa upande wa Mfuko wa Umoja ambapo pato la wawekezaji ni asilimia 10.3,” alisema Kyuki.
Kyuki alisema pamoja na changamoto nyingi zilizojitokeza ndani yam waka wa fedha uliopita bado mfuko huo umeendelea kufanya vizuri ikilinganisha na mifuko mingine ya uwekezaji.
“Hatua hii imechangiwa na kuongezeka kwa wawekezaji weno kutokana na kuongezeka kwa Imani ya wawekezaji kwenye mfuko.
“Ukuaji wa mfuko pia umechangiwa na elimu inayotolewa na meneja wa mfuko kuhusu faida za uwekezaji wa pamoja, pia matumizi ya mitandao ya simu katika kufanya miamala yauwekezaji nayo yamerahisisha namna ya kufanya uwekezaji kwenye mifuko, hivyo wawekezaji wamehamasika kujiunga na mifuko toka huduma hii ilipozinduliwa Novemba, mwaka jana,” alisema Kyuki.
Alisema pamoja na changamoto za ugonjwa wa corona na mabadiliko ya sera za uwekezaji katika nchi zinazoshirikiana na Tanzania, utendaji wa soko bado umeendelea kuwa wa kuvutia na kuridhisha mazingira imara ya udhibithi pamoja na jinsi serikali ilivyo zifanyia kazi changamoto hizo ndiyo msingi wa kuwa na madhara madogo kwenye utendaji wa soko.
“Aidha, kutokana na uzinduzi wa huduma kwa wateja kwa njia ya mitandao ya simu Novemba mwaka jana, miamala ya uwekezaji kwa njia ya mitandao imekuwa ikiongezeka na kufikia wastani wa Sh milioni 300 kwa mwezi, hili ni ongezeko zuri. hata hivyo kampuni itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma kwa njia ya mitandao ya simu kwa kuwa tunaamini kuwa bado kuna fursa ya kuongeza miamala zaidi ya hapo tulipofikia,” alisema Kyuki.