Na PENDO FUNDISHA, MBEYA
MFANYABIASHARA maarufu jijini Mbeya, Steven Samweli maarufu kwa jina la Maranatha, ametiwa nguvuni akituhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Kutiwa nguvuni kwa mfanyabiashara huyo ni mwendelezo wa nia ya Serikali ya kupambana na biashara ya dawa hizo nchini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, aliwaambia waandishi juzi kwamba, Maranatha alikamatwa juzi usiku akiwa katika moja ya maduka yake ya dawa baridi.
“Baada ya polisi kupata taarifa za mfanyabiashara huyo kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya, tuliweka mtego na hatimaye kufanikiwa kumtia nguvuni.
“Kwa sasa tunamshikilia kwa mahojiano na baada ya uchunguzi kukamilika, atafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Kidavashari.
Pamoja na hayo, kamanda huyo wa polisi alisema kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kunafikisha idadi ya watu wanane waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya mkoani Mbeya.
“Miongoni mwa hawa tunaowashikilia, baadhi yao walikutwa na vielelezo, hivyo watafikishwa mahakamani wakati wowote wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
“Kwa hiyo, nawaomba wananchi mkoani hapa, waachane kabisa na biashara ya dawa hizo kwa sababu wakikutwa nazo, watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola,” alisema Kamanda Kidavashari.