26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MFANYABIASHARA JELA MIAKA 10

Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha miaka 10 jela mfanyabiashara Gairo Mtozoma (43) kwa kosa kupatikana na silaha na risasi kinyume cha taratibu.

Mshtakiwa huyo, mkazi wa Magomeni Kagera alihukumiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Hakimu Mwambapa, alisema upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi watano waliothibitisha mashtaka na mahakama ilimuona mshtakiwa ana kesi ya kujibu na kujitetea mwenyewe.

Alisema upande wa Jamhuri, umeweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka hivyo mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine.

Akijijitea kabla ya kuhukumiwa, mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.

“Katika shtaka la kwanza la kupatikana na silaha, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitano jela na katika shtaka la pili atatumikia kifungo cha miaka mitano,” alisema Hakimu Mwambapa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa anadaiwa Agosti 11, 2016 akiwa maeneo ya Magomeni Kagera wilayani Kinondoni, alikutwa na bastola moja aina ya Browing, yenye kumbukumbu namba 90002 iliyosajiliwa kwa namba TZCAR-A222683 bila kuwa na leseni.

Katika shtaka jingine, alidaiwa kuwa mnamo Agosti 11, 2016 mshtakiwa akiwa maeneo ya Magomeni Kagera wilayani Kinondoni, alikutwa na risasi sita bila kuwa na leseni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles