25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Bilionea aiibia TRA mil. 7/- kila dakika

RAIS Dk. John Magufuli
RAIS Dk. John Magufuli

*Rais Magufuli asema ameshughulikiwa yupo sehemu salama

*Awapa rungu ma-DC wapya, wakorofi kushughulikiwa

NA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amemtumbua mfanyabiashara mmoja maarufu Dar es Salaam, aliyebainika kufanya miamala ya fedha ya Sh milioni saba hadi nane kwa kila baada ya dakika moja.

Kutokana na hesabu ya Sh milioni saba anayoingiza kwa dakika moja, mfanyabiashara huyo hutengeneza Sh milioni 420 kwa kila saa moja, sawa na Sh bilioni 5.2 kwa saa 12 na Sh trilioni 16 kwa mwezi ambazo halipi Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Rais Magufuli amesema mfanyabiashara huyo aliyebainika kuwa na makampuni mengi, alikuwa akishirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana, baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa mikoa watatu katika hafla iliyohudhuriwa pia na wakuu wa wilaya wateule.

Alisema waligundua jipu hilo baada ya kufuatilia kwenye mapato.

“Tulikuwa tunafuatilia kwenye ‘revenue’ (mapato), kwenye zile VAT ambazo zinatumika ‘ku-collect revenue’ (kukusanya mapato), yupo mtu mmoja ambaye alikuwa ametengeneza kampuni zake nyingi, alikuwa anafanya ‘transaction’ (miamala) ya fedha kila dakika moja kati ya Sh milioni saba na nane.

“Na hizo risiti alikuwa anaziuza kwa wafanyabiashara wengine, kwenye VAT anatakiwa kulipia kwa asilimia 18. Wafanyabiashara wengine hao walikuwa wanauziwa kwa asilimia tano na wakishauza bidhaa wanakwenda kuomba TRA iwarudishie hiyo asilimia 18, kwa hiyo Serikali imekuwa ikipoteza asilimia 18.5, ni matrilioni na matrilioni ‘of money’ (ya fedha).

“Bahati nzuri huyo mtu yuko kwenye mikono salama, tunafuatilia namna tutakavyorudisha hizo fedha, na huyo mtu alikuwa ana-connection kati ya watu wa BRELA na TRA… hiyo ndiyo Tanzania.

“Najaribu tu kutoa mfano ili katika maeneo yenu mkasimamie mapato ya Serikali, kwa sababu tumepoteza mapato mengi kuliko tunavyofikiria, huku Watanzania wakiteseka sana, na mambo yanayofanyika ni ya ajabu,” alisema Rais Magufuli akiwaambia wakuu hao wa mikoa na wilaya.

 

MA-DC 101 NA VIGEZO

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema mchakato wa kupata wakuu wapya wa wilaya ulikuwa mgumu, na kwamba amewaacha wengi wa zamani kwa kuwa hawakutimiza vigezo alivyovitaka.

“Mchakato wa kupata ma-DC ulikuwa mgumu kwa sababu ilibidi tuangalie historia ya kila mmoja. Tuliangalia mambo mengi sana, lakini pia tuliangalia kwa ku-preview atatimiza haya tunayotaka kuyafanya kwa miaka mitano?

“Na ndiyo maana mnavyoona ma-DC wa zamani waliorudi ni 39, kwa hiyo wale 101 wote hawakurudi… niseme tu ukweli kwamba hawakufikia vigezo tulivyokuwa tunavitaka,” alisema Rais Magufuli.

UTEUZI WA WAKURUGENZI

Alisema katika uteuzi huo, alichukua wakurugenzi kwa kuwa walifanya vizuri katika maeneo yao waliyokuwa wakiyaongoza.

“Tulichukua wakurugenzi walio-perform vizuri katika maeneo yao. Wapya wako takribani 100 na waliobaki ni hao kati ya 38 na 39. Ni matumaini yangu kwamba mtakwenda kufanya kazi na kutimiza wajibu wenu.

“DC ni nafasi kubwa ya uongozi katika Serikali na ndiyo maana mfano mkubwa wa DC mstaafu ni Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), ni kwa sababu alitimiza wajibu wake na leo yuko hapa,” alisema.

MIKAKATI  YA KAZI

Mkuu huyo wa nchi aliwapa mikakati ya kufanya kazi wakuu hao wa wilaya kwa kutimiza dhana ya kuchapa kazi kwa niaba ya Serikali.

“Nina matumaini makubwa mtakwenda kutimiza dhana ya kuchapa kazi kwa niaba ya Serikali, ninyi ndio wawakilishi wetu na ndio mnawakilisha wananchi wa maisha yote.

“Watanzania wana matatizo na changamoto kubwa. Ni matumaini yangu kwamba hamtaniangusha na hamtaiangusha Serikali. Nina imani mtakwenda kutatua matatizo ya wananchi, hasa walio masikini, sitegemei wala sifikirii kwamba mkawe chanzo cha kutengeneza matatizo,” alisema Rais Magufuli.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wasimamie haki, huku wakimtanguliza Mungu katika kufanya kazi, kusimamia maadili, kutenda haki, kutojihusisha na rushwa, kuwatumikia Watanzania bila kubagua dini, kabila wala vyama vyao.

“Kikubwa mkasimamie yale tuliyoyaahidi sisi wanaCCM, kwa sababu wakati tunazunguka tukiomba kura, yapo tuliyoyaahidi, hayo mkayatekeleze kwa nguvu zote.

“Na wala asitokee mtu yeyote wa kuwakwamisha kutekeleza hayo, ninyi ndio wakuu wa wilaya na ninyi watatu ndio wakuu wa mikoa. Mna mamlaka makubwa ya kuweka mahabusu mtu masaa 48 halafu kesho yake ukamwachia. Ila msiende kuonea watu, mkachape kazi.

“Imani tuliyoionyesha kwenu sisi viongozi wenu mkaionyeshe kwa Watanzania mnaowaongoza, mkashirikiane na viongozi mtakaowaongoza, wanasema umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

“Nina uhakika mkisimama vizuri  kwa kuzingatia maadili mliyonayo, na bahati nzuri wengi mna uzoefu katika maeneo yenu. Mkawahamasishe Watanzania katika wilaya na mikoa yenu kufanya kazi. Watanzania wengi tumezoea kulalamika, tunataka tupewe, lakini hatufanyi kazi. Tukawasimamie kuchapa kazi,” alisema.

Aliwataka wakuu hao wa wilaya ambao pia ni wenyeviti wa kamati ya ulinzi na usalama, kukemea rushwa katika maeneo yao na kusimamia mapato ya Serikali.

“Huwa inatokea saa nyingine wakurugenzi kwa sababu kuna fedha nyingi tunapelekaga kule, wanadhani ni zao wakati ni za Serikali, mkawasimamie bila woga.

“Kupitia halmashauri zenu, mkahakikishe fedha hizo zinatumika kulingana na matakwa ya kanuni na sheria za nchi,” alisema Rais Magufuli.

AWAPA RUNGU

Aidha aliwaagiza wakuu hao wa wilaya kutumia madaraka yao kwa wale ambao watawachezea katika kutimiza majukumu yao.

“Atakayewachezea mkatumie madaraka yenu ili msiwe wanyonge, ninyi ndio wawakilishi wangu huko, tunawa-support kwa nguvu zote. Mkafanye kazi bila woga wowote, mkatembee na vifua mbele, ikiwezekana na hata vichwa mbele kwa sababu tumewaamini.

“Ukifanya kitu kizuri kwa dhamira na nia njema kitafanikiwa, ukifanya kitu kwa unafiki hakitafanikiwa, ndiyo maana nawaambia mfanye kazi kwa kumtanguliza Mungu na kuwatanguliza Watanzania. Kazi iliyo njema itazaa matunda mazuri.

“Kazi ya kiongozi ni kuongoza na uwezo huo mnao, na nina uhakika dhamira hiyo pia mnayo. Mmechaguliwa miongoni mwa Watanzania milioni 50, mnaweza mkafikiri tumewachagua sisi, lakini inawezekana Mungu ametutumia sisi kuwachagua,” alisema.

AMFAGILIA DC KASESELA

Rais Magufuli alisema pamoja na kwamba Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, alisemwa sana, lakini aliamua kumrudisha katika nafasi hiyo kwa kuwa ni mchapakazi.

“Namwona DC wa Iringa alivyokuwa anabeba watoto… wakamsema weee na mimi nikasema huyu huyu abaki hapa. Katika kazi hizi utasemwa sana, wapo watakaowakejeli, wapo watakaowadhihaki, mkamuweke Mungu mbele mkafanye kazi kadiri Mungu atakavyowaongoza,” alisema.

HASIMU WA NDUGAI

“Katika uteuzi wangu nimefanya ‘combination’ nzuri sana, wataalamu wamo, vijana… ningeweza kuwataja kwa majina wote, naona hata yule Joseph Chilongani (DC wa Meatu) aliyepigwa fimbo na mtani wangu naye yuko hapa,” alisema.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Job Ndugai ambaye ni Spika wa Bunge, alimpiga kwa fimbo DC Chilongani, wakati wa mchakato wa ndani wa kura za maoni kupitia CCM.

MAJALIWA

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwaambia viongozi hao kuwa kazi waliyopewa ni kubwa hivyo wakatimize majukumu yao kwa kuwatumikia Watanzania.

Alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kwa yeyote anayeshindwa kutekeleza majukumu yake.

“Mkakati wa kuwatumikia Watanzania uko kule mnakokwenda, mtumie busara, hekima, kuwaheshimu wasadizi wenu wa kazi, kujua wananchi wanapata matatizo gani na mhakikishe migogoro ya wakulima na wafugaji inakwisha,” alisema Majaliwa.

SAMIA

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wakuu hao wa wilaya kusoma alama za nyakati wanapofanya kazi.

“Msome alama za nyakati mliobakia ni kwa sababu mlifanya kazi na wapya someni kwa wale waliobaki, tuyaache yale tuliyoyazoea huko nyuma, naomba angalieni kwa sasa ni kitu gani kinatakiwa,” alisema Samia.

Wakuu wa mikoa walioapishwa ni Zainab Telack (Shinyanga) ambaye amejaza nafasi ya Anne Kilango, Dk. Binilith Mahenge (Ruvuma) anayejaza nafasi ya Said Mwambungu aliyehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Dk. Charles Mlingwa (Mara), anayejaza nafasi ya Magesa Mulongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles