28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Mfalme wa Saudi Arabia afariki dunia

RIYADH, Saudi Arabia
MFALME wa Saudi Arabia, Abdullah bin Abdul-Aziz Al Saud (90), amefariki dunia jana na cheo chake kurithiwa mara moja na mdogo wake, Salman (79).
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la DW, Ofisi ya Kifalme haijataja sababu ya kifo cha Mfalme Abdullah, lakini habari zaidi zinadai kuwa kiongozi huyo alilazwa hospitali tangu Desemba mwaka jana kutokana na kusumbuliwa na homa ya mapafu ambapo kwa muda wote tangu akiwa hospitali alipumua kwa msaada wa mashine.
Mfalme Abdullah bin Abdul-Aziz Al Saud ameitawala nchi hiyo tangu mwaka 2005, ambapo chini ya utawala wake nchi hiyo imekuwa mshirika muhimu wa utawala wa Serikali ya Marekani katika ukanda wa nchi za Kiarabu.
Viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani wametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mfalme Abdullah. Kiongozi huyo alitazamwa kama mwanamageuzi mwenye tahadhari, aliyeliongoza taifa hilo la kifalme katika kipindi cha machafuko yaliyotikisa Mashariki ya Kati.
Rais wa Marekani, Barack Obama amemuelezea hayati Abdullah kama mshirika anayethaminiwa, viongozi wa Japan, India, Ufilipino, Pakistani na Ufaransa pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon nao walituma salamu za rambirambi nchini humo.
Katika hatua isiyo ya kawaida, baada ya kifo cha Mfalme Abdullah, bei ya mafuta ilipanda huku wasiwasi ukitanda kuwa huenda mfalme mpya wa nchi hiyo, Salman bin Abdul- Azizi akaendelea na sera hiyo.
Ikumbukwe kuwa nchi hiyo inaongoza kwa uzalishaji mafuta duniani na imechangia kwa kiasi kikubwa kusimamia uamuzi wa OPEC wa kukataa kupunguza uzalishaji wa nishati hiyo, hivyo kusababisha kushuka kwa bei ya mafuta duniani kwa asilimia 50.
Hata hivyo, katika hotuba aliyoitoa mapema jana kwa njia ya televisheni, mfalme mpya wa nchi hiyo ameahidi kuendeleza sera za watangulizi wake.
“Tutaendelea kuziheshimu sera sahihi ambazo Saudi Arabia imezifuata tangu kuasisiwa kwake,” alisema mfalme huyo.
Hayati Mfalme Abdullah, alifanya mageuzi ya tahadhari wakati akiwa madarakani, akiwapinga wahafidhina kwa hatua kama za kuwajumlisha wanawake katika baraza la ushauri la Shura.
Pia aliongoza maendeleo ya kiuchumi ya falme hiyo na alisimamia mchakato wa nchi kujiunga na shirika la biashara duniani (WTO), akitumia fedha za mafuta kujenga miji mipya ya kiuchumi, vyuo vikuu na njia za reli.
Pamoja na jitihada zake za kuimarisha uchumi, Saudi Arabia bado inakosolewa kwa rekodi yake ya haki za binadamu, ikiwemo kufungwa kwa wapinzani pamoja na kuzuia wanawake kuendesha magari.
Tayari mfalme mpya amemteua mwanaye, Mohammed Bin Salman kuwa waziri wa ulinzi na mkuu wa ofisi ya Kifalme, huku mawaziri wengine wakibakia katika nyadhifa zao, pia amemtangaza mjukuu wa mwasisi wa taifa hilo, Mohammed bin Nayef kuwa naibu mrithi wa kiti cha ufalme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles