29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

MFAHAMU RAFIKI WA MTOTO WAKO

NA AZIZA MASOUD,

TATIZO la mmomonyoko wa maadili katika familia  na jamii kwa ujumla limekuwa likilalamikiwa  na wazazi wengi. Watoto wanaoishi katika maadili mabovu mara nyingi wanakuwa na tabia chafu baadaye kwa sababu  ya kukosa mwongozo katika malezi.

Malezi ya mtoto hayaishii tu nyumbani kwa mama au mlezi, ni vema pia kama mzazi ukawa na utaratibu wa kumwangalia mtoto na watu anaofuatana nao anapokuwa nje ya nyumba.

Mtoto anapaswa kulelewa katika mazingira na misingi mizuri ili asijiingize katika masuala mbalimbali ya kidunia, ikiwamo unywaji wa pombe, vitendo vya ngono, uhusiano wa jinsia moja, matumizi ya madawa ya kulevya, lugha chafu n.k.

Kitu muhimu unachopaswa kufanya ni kufuatilia rafiki au marafiki wa mtoto wako wa nyumbani na shuleni.

Unapaswa kumfahamu rafiki wa mtoto wako na anapoishi, unaweza ukaenda mbali zaidi  na kutengeneza mazingira ya kuhakikisha unakutana na wazazi wake ili ujue analelewa na watu wa aina gani.

Mbali na hilo, unapaswa kuchunguza pia sababu zilizomuunganisha mwanao na kijana huyo. Je, ni masuala ya kimasomo, michezo tu ya kawaida ya shuleni au kuna sababu nyingine?

Umeshawahi kufuatilia na kugundua tabia nzuri ama mbaya alizonazo chanzo chake si marafiki, ni vyema kufahamu mambo haya muhimu, kwani ndiyo msingi wa malezi kwa watoto.

Inawezekana kabisa mtoto wako ana rafiki lakini rafiki huyo ni mtukutu, ujue kabisa na mwanao atajifunza utukutu tu na si vinginevyo.

Pia inawezekana kabisa busara alizokuwa nazo mtoto wako amejifunza kutoka kwa rafiki yake, lakini kwasababu wewe hujui huwezi kuelewa.

Zipo faida nyingi utazipata ukifahamu mtoto wako yuko karibu na nani na anaongozana na nani, ni muhimu kwasababu hata ikitokea dharura mwanao haonekani nyumbani unaweza ukapata mwanga wa kumtafuta kupitia rafiki yake.

Ni vizuri kumkaribisha rafiki wa mtoto wako nyumbani kwako, zungumza naye kufahamu mawazo yake, weka mada zenye changamoto za kielimu na kijamii, kuna vitu utavifahamu.

Ikishindikana kumwalika nyumbani waweza andaa safari ya kutoka nje ya maeneo mnayoishi ukiwa nao, unapaswa kuwaacha wacheze wenyewe, huku wewe ukifuatilia mienendo yao na baadaye kuzungumza nao.

Lakini unaweza pia kutembelea shule wanayosoma na kudadisi kwa walimu juu ya uhusiano wa mtoto wako na rafiki yake, kwa kufanya hivyo utajua kama urafiki wao uendelee au la, utafahamu ni urafiki wenye faida au ni wa kufundishana mambo maovu.

Hata kama wazazi/walezi tuko ‘busy’ kupita kiasi, ni vyema kufuatilia vitu vidogo vidogo vya mtoto wako, vinaweza kuwa na faida kubwa kwako na kwa maisha yake ya baadaye.

Kwa leo tuishie hapa, tukutane tena wiki ijayo, kwa maoni, ushauri andika kwa barua pepe

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles