25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

CCM WAMEBADILI MUUNDO, HAWAJABADILIKA

NA MARKUS MPANGALA,

MUUNDO wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi-CCM umetangazwa hivi karibuni mjini Dodoma. Naweza kusema mabadiliko ya kuwa na wajumbe wachache ni kama yale yaliyowahi kufanywa na Chama cha Chinese Communist Party (CCP).

Chama hicho cha nchini China kina wajumbe 10 tu wa Kamati Kuu chini ya Katibu Mkuu, Xi Jinping, ambaye ndiye Rais wa China. Pengine si ajabu sana CCM kujirudisha kwa CCP ya China, lakini mabadiliko hayo yanatupatia tafakari jadidi.

Kulingana na mabadiliko hayo, Kamati Kuu ya CCM itaundwa na wajumbe 24, ambao ni; Mwenyekiti wa CCM-Taifa, Makamu Mwenyekiti CCM-Bara, Makamu Mwenyekiti CCM-Zanzibar, Katibu Mkuu-Taifa, Naibu Katibu Mkuu CCM-Bara, Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Spika wa Bunge, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti wa UWT-Taifa  na Mwenyekiti wa UVCCM-Taifa.

Wengine ni Mwenyekiti wa Wazazi-Taifa, Katibu wa Halmashauri Kuu Oganaizesheni, Katibu Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi, Katibu Halmashauri Kuu Uchumi na Fedha, Katibu Halmashauri Kuu Uhusiano wa Kimataifa, wajumbe watatu wa kuchaguliwa na Halmashauri Kuu ya CCM-Bara na wajumbe watatu wa kuchaguliwa kutoka Halmashauri Kuu ya CCM-Zanzibar.

Katika mabadiliko hayo kuna vipengele viwili vimepitishwa vinaisumbua akili yangu, vipengele hivyo vinabainisha kuwa, mabadiliko ya Kamati Kuu ni kutoka wajumbe 34 hadi 24 kwa sasa. Katika mabadiliko ya wajumbe hao, CCM wamekubaliana kwa kauli moja kuwa, miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Spika wa Baraza la Wawakilishi-Zanzibar.

Hii ina maana wabunge wao ambao watachaguliwa kuwa maspika wa Bunge wataingia moja kwa moja Kamati Kuu kwa kigezo hicho. Ninaweza kusema hilo ni pendekezo zuri kulingana na walivyoliona pamoja na hali ya sasa ambayo CCM ndiyo wameunda Serikali baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Spika wa Bunge ni Job Ndugai na Naibu wake Tulia Ackson. Spika wa Bunge la Wawakilishi ni Zubeir Ali Maulid na Naibu wake ni Mgeni Hassan Juma.

Katika vipengele hivyo nimebaki na maswali, mathalani iwapo CCM kikipoteza kiti cha uspika wa Bunge na Baraza la Wawakilishi, je, nafasi ya kuwa wajumbe wa Kamati Kuu itawakilishwa vipi? Wale watakaoshindwa uchaguzi wa Spika na Baraza la Wawakilishi wataendelea kuwa wajumbe ‘wawakilishi’ wa Kamati Kuu kwa kigezo hicho hicho kilichopendekezwa?

Ama CCM wanadhania kuwa hakutakuwa na uwezekano wa wao kushindwa kuliongoza Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi, huku wakijionea nafasi zao katika majimbo zinazidi kushuka?

Kwa mfano, mgombea wa uspika na mwakilishi ni wabunge wa kawaida. Chukulia uchaguzi umefanyika halafu CCM wameangushwa, ikiwa na maana amechaguliwa mbunge wa kambi ya upinzani kuwa Spika wa Bunge.

Swali linarudi kuwa je, mbunge na mwakilishi huyo ambao hawatakuwa maspika wataingizwa kwenye Kamati Kuu kama wajumbe? Na kama hawataingizwa, ina maana CCM kitakuwa kimeweka kipengele ambacho hakina umuhimu wowote wala uhalisia wa demokrasia?

Naweza kukiri kuwa, Spika wa Bunge na Baraza la Wawakilishi wanaingizwa kwenye Kamati Kuu kama njia ya mkakati wa chama kujiimarisha zaidi bungeni na Baraza la Wawakilishi.

Kwamba Maspika hao watakuwa wanaingia moja kwa moja kwenye mikakati ya chama, hivyo kuwa sehemu ya kufanikisha, kulinda, kutekeleza na kuhakikisha maslahi ya chama yanalindwa.

Si vibaya kulinda maslahi ya chama, tatizo linakuja ni mtu wa aina ipi anayeingia kwenye Kamati Kuu ikiwa watakosa nafasi ya uspika?

Ndiyo kusema kuwa, mhimili wa Bunge utakuwa ‘umetekwa nyara’ rasmi kwakuwa wasimamizi wakuu watakuwa wameingizwa Kamati Kuu ya chama kwa maslahi ya chama ndani ya mhimili wa Bunge.

Nadhani CCM wanatakiwa kuelewa kuwa, nyakati zimebadilika, na uwezekano wa kuongezeka wabunge kutoka upinzani ni mkubwa.

Taratibu wananchi wanaelewa majukumu ya wapinzani. CCM wanaweza kubeza hilo, lakini wanatakiwa kuangalia idadi ya wabunge wa upinzani walioingia mwaka 2015, ikiwa na maana wananchi wanawapa nafasi wabunge hao kama sehemu ya demokrasia.

Hivyo, kusema hilo nina maana ya kuwauliza wana CCM kwamba kupendekeza Spika wa Bunge la Muungano na Bunge la Wawakilishi waingie Kamati Kuu wanadhani utawala wa chama hicho utakuwa wa kudumu (milele) pasipo kubadilishwa au kushindwa bungeni? Wanaweza kuona ni wazo zuri, lakini nyakati zijazo watalazimika kufumua tena muundo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles