Beatrice Kaiza
KAMA upo karibu nna mitandao ya kijamii bila shaka utakuwa umewahi kukutana na picha za watu mbalimbali waliopiga na mtu mwenye urefu wa kustaajabisha.
Anaitwa Julius Charles, anayeishi Dar es Salaam ambaye mastaa kama Stamina, Dogo Janja, Bright na wengineo wamewahi kupiga naye picha huku akitajwa ni mtu wa pili kwa urefu unaokimbizana na mchezaji wa mpira wa kikapu wa Kimataifa, Hasheem Thabeet.
Njemba huyo ameweka wazi kupitia wakati mgumu nyakati za usiku kwa kukimbiwa na watu mbalimbali anapokutana nao njiani wakidhani ni jinamizi.
Julius mwenye urefu wa futi 7.2 amepiga stori na ripota wa Swaggaz alipotembelea ofisi za gazeti hili, hivi karibuni ambapo amezungumza mengi kuhusu maisha yake hasa harakati za kusaka nafasi za kucheza mpira wa kikapu kwenye anga za Kimataifa,karibu.
Swaggaz: Julius ni nani?
Julius: Mimi ni mzaliwa wa Mwanza, ni mtoto wapili kati ya watoto saba kwenye familia yetu na mpaka sasa nina miaka 25.
Swaggaz: Ulianza lini kujiona upo tofauti na wenzako?
Julius: Nilianza kujiona tofauti nikiwa shule ya msingi sababu nilikuwa najigonga mara kwa mara mlangoni na watu wakaanza kushangazwa na aina ya ukuaji wangu maka kuna kipindi nikawa kivutio cha kushangaza kwa wanafunzi wenzangu.
Swaggaz: Kuna faida yoyote umeipata kwa kuwa mrefu?
Julius: Nimepata faida nyingi hasa kujulikana na watu wengi pia nimepata marafiki na wengine wanatamani kuwa kama mimi.
Swaggaz: Tunajua unacheza mpira wa kikapu, je unakutana na changamoto gani?
Julius: Kwa hapa Tanzania mchezo wa kikapu umekosa wadhamini hata watu wamekuwa hawachukulii kwa uzito mkubwa mchezo huu. Watu ambao wanacheza ni kwa ajili ya afya na kijiburudisha tu siyo mchezo ambao unatumika kwa ajili ya ajira.
Swaggaz: Una ukaribu gani na Hasheem Thabeet?
Julius: Hasheem Thabeet ni kama kaka yangu ni mtu ambaye ananifariji sana tunafahamiana tangu nikiwa shule.
Swaggaz: Umejaribu kuongea na Hasheem kuhusu kujaribu kucheza kipapu Marekani?
Julius: Nimeongea na Hasheem mambo mengi tu na amenipa ushauri wa mambo mbalimbali hadi safari yangu ya kwenda Marekani niliyofanya mwaka jana yeye ndiyo alinisaidia.
Swaggaz: Safari yako ya Marekani ilizaa matunda?
Julius: Bado ipo lakini kwasasa kuna mambo nayaweka sawa kama kukusanya nauli na njia ambayo natumia ni kuomba watu mbalimbali kuchangisha wadau ili kufanikisha nauli na kuweza kwenda tena.
Swaggaz: Watu wanachukuliaje urefu wako wa maeneo unayopita na kuishi?
Julius: Hapo zamani ndiyo watu walikuwa wananishangaa ila kwasasa imekuwa kawaida na kila ambapo napita nimekuwa najipatia marafiki mbalimbali.
Swaggaz:Ni kitu gani ambacho huwezi kukisahau katika maisha yako?
Julius:Kifo cha baba yangu, nilimwona akiwa anataka roho hadi kufikia umauti wake.
Swaggaz: Ni kitu gani unawaambia wadau wa mchezo wa kikapu?
Julius: Ombi langu ni wadau wa michezo kuuangalia mchezo huu na kuutengenezea mazingira ili uwe ajira.
Swaggaz: Karibu sana na asante kwa ushirikiano wako.
Julius: Nashukuru sana, asante pia.