CHRISTINA GAULUHANGA – DAR ES SALAAM
MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob ameagiza Wakala wa Majengo Tanzania(TBA) kujipima kabla ya kuanza ujenzi wa jengo jipya la utawala la halmashauri hiyo.
Alisema  kama hawawezi kutekeleza kwa viwango vinavyotakiwa ni vema wakaachia ngazi mapema.
Akizungumza wakati wa kutia saini ujenzi wa jengo hilo la utawala Dar es Salaam jana, Jacob alisema kamwe hatafumbia macho na atakuwa wa kwanza kupiga kelele endapo mradi huo utaenda kinyume na mkataba uliosainiwa,
Alisema Serikali kuu ilitoa mwongozo wa kuwatumia TBA katika mradi huo lakini angekuwa yeye binafsi angependekeza kushindanisha wakandarasi kadhaa wakiwamo Suma JKT Â kupata mkandarasi bora.
“Naomba nitoe tahadhali kwa TBA mkajipime kabla hamjaanza ujenzi huu kwa sababu  mkionyesha kusuasua mimi ndiyo nitakuwa wa kwanza kulalama kwa vile wadau wetu wa pili wa mradi huu ambao ni Serikali wamewateua nyie mjitahidi msiwaangushe,” alisema Jacob.
Alisisitiza hilo akigusia historia fupi ya TBA kwenye baadhi ya mikoa ambako imeshindwa kutekeleza mikataba na kusababisha mingine kunyang’anywa.
“Tunasikia huko mikoani baadhi ya miradi mliporwa kwa sababu ya uzembe wa watendaji wenu wa huko lakini kwa hapa Dar ea Salaam hamjapata kashfa hiyo, hivyo naomba mjipange vema katika mradi.huu,” alisema Jacob.
Meya huyo alisema mradi huo    hadi ukamilike utatumia Sh bilioni 6.2 ambako Serikali kuu itatoa Sh bilioni 4.3 na halmashauri   itachangia Sh bilioni 1.9.
“Katika miaka hii miwili tayari tumepoteza zaidi ya Sh milioni 300 kwa ajili ya kupanga jengo jambo ambalo limesababisha fedha nyingi za halmashauri ambazo zingetumika katika huduma za jamii kupotea,” alisema Jacob.
Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam, Edwin Godfrey alisema amepokea salaam za watendaji wa halmashauri hiyo na kujionea mazingira halisi ya kazi.
“Tumepokea maagizo yote tunachoahidi ni iwe mvua, jua, usiku, sikukuu tutafanya kazi  saa zote kwa kiwango kinachohitajika ambacho kipo kwenye mikataba yetu,”alisema Godfrey.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Beatrice Kwai alisema atasimamia mkataba   utekelezwe kwa viwango vinavyotakiwa.