33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tunasikitishwa  RC Mghwira, ma-dc kutoleewana

MKUU  wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na wakuu wake wa wilaya zote hawana maeelewano mazuri, jambo ambalo kwa namna moja au nyingine linaathiri  utendaji kazi  za Serikali kwa kiasi kikubwa.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya shughuli nyeti kutokwenda  kwa wakati kutokana na mkwaruzano uliopo baina ya viongozi ambao ni nguzo kuu ya kuwatumia wananchi wao.

Siri hiyo ilifichuliwa  na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofungua kikao cha kazi kwa wakuu wa mikoa na wilaya   Dodoma juzi.

Alisema anasikitishwa na kukerwa kutokuwapo mfumo mzuri wa uelewano kati ya viongozi hao ambao ni wateule wa Rais Dk. John Magufuli, ambao wakati wanateuliwa kushika nyadhifa hizo walikula kiapo cha kuwatumikia wananchi kwa gharama yoyote.

Akionekana kukerwa zaidi, Majaliwa anasema imefikia hata wameshindwa  kuheshimiana, tena kibaya zaidi wakienda kinyume cha itifaki.

Vilevile,  viongozi hao wamekuwa wakitunishiana misuli, kila mmoja akijigamba kuwa ni mteule wa Rais hivyo ana haki ya kufanya  jambo lake anavyojisikia. Huo ni utoto uliopitiliza.

Haiwezekani na haingii akilini hata kidogo  mkuu wa wilaya ashindwe kumheshimu mkuu wa mkoa kama kiongozi wake wa kazi ambaye anaripoti kwake kila siku. Huo ni uelevi wa madaraka ambao umepita kipimo.

Lakini hata mkuu wa mkoa  mwenyewe kama msimamizi mkuu wa shughuli zote za mkoa wake, inakuwaje anashindwa kuwakalisha wakuu wa wilaya kwenye vikao vyao halali wakazungumza na kuondoa kasoro za aina hiyo?

Aibu hiyo ndiyo chanzo cha kushindwa kwa mkoa mzima kusimamia majukumu yao ya kila siku, huku wakibaki wanaviziana kwenye korido na kurushiana vijembe visivyokuwa na tija   kwa maendeleo ya wananchi masikini wa mkoa huo.

Tunatambua   kwamba kiitifaki mkuu wa mkoa yuko juu ya wakuu wa wilaya, inakuwaje wanafikia hatua hiyo ambayo ni kiwango kibovu cha utawala?  Rais anayo mamlaka ya kuteua wote kwa mujibu wa kada, itifaki ya kada na kazi.

Ugomvi huo umefika pabaya kwa sababu unaonyesha sasa mkuu wa wilaya anamwandikia Rais barua  moja kwa moja, hiyo si itifaki. Mwenye jukumu la kumwandikia barua ya aina hiyo ni mkuu wa mkoa.

Kauli ya Majaliwa ifunguwe milango  kwa uongozi wa  Mkoa wa Kilimanjaro kujitafakari kama upo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wake au kuendeleza malumbano ambayo hayana tija kwao huku wakishindwa kutumia muda mwingi kutatua kero za wananchi wao.

Tunamkumbusha Mghwira   kiapo chake  Ikulu, Dar es Salaam siku anaapishwa mbele ya Rais Dk. John Magufuli na maelekezo aliyopewa ya kwenda kuwatumia wananchi masikini.

Lakini pia wakuu wa wilaya  nao wakumbuke viapo vyao; walipoapishwa na Mghwira waliahidi kuchapa kazi na kuwaletea maendeleo wananchi kwa ujumla. Sasa inakuwake wote   wamesahau   viapo vyao?

Tunamshauri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Kapteni George Mkuchika kukutana na viongozi hao haraka   kurejesha umoja, amani na utulivu kwao ili wasimamie majukumu ya Serikali vizuri.

Tunasema hivyo kwa sababu Mkuchika ni waziri ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana ya kusimamia utawala bora, lakini pia ni waziri ambaye amekuwa serikalini katika awamu tano za urais wa nchi anaweza kuwa msaada mkubwa wa kumaliza ugomvi huo haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles