32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Meya Tabora aagiza kuchunguzwa mradi wa Afya Tumbi

Na Allan Vicent, Tabora

Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora, Ramadhani Kapela, ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani hapa kuchunguza mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Tumbi kilichoko katika manispaa hiyo baada ya kutoridhishwa na gharama zilizotumika kutekeleza mradi huo.

Ametoa agizo hilo leo Machi 9, katika kikao cha robo ya pili ya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa manispaa.

 Amesema kuwa ujenzi wa miundombinu ya mradi huo ikiwemo vyoo umetekelezwa chini ya kiwango jambo ambalo hawakubaliani nalo, hivyo akaomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwenda kufanya uchunguzi wa kina.

 Amefafanua kuwa serikali iliwapatia kiasi cha sh mil 200 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la kuhudumia wagonjwa na vyoo lakini kazi iliyofanyika haina ubora unaotakiwa na haiendani ya thamani ya fedha iliyotolewa.

Mstahiki Meya alibainisha kuwa mradi huo ambao ujenzi wake umekamilika, utekelezaji wake haukufuata maelekezo yaliyobainishwa katika BOQ kwani fedha iliyotakiwa kutumika ni mil 200 lakini imeshaisha na wanataka sh mil 14 zaidi.

Amesisitiza kuwa hata Wajumbe wa Kamati ya Fedha waliotembelea mradi huo hivi karibuni hawakuridhishwa na utekelezaji wake, kwani jengo lililojengwa ni dogo na vyoo haviko sawa na hata viongozi wa kata waliotembelea mradi huo na kujaribu kuhoji hawakupewa ushirikiano wowote.

“Namshukuru sana Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kutuletea sh mil 200 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho ili kuwarahishia wakazi wa kata hiyo kupata huduma bora za afya.

“Hatuwezi kukubali fedha za serikali zichezewe, naomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na vyombo vingine vya dola kuchunguza suala hili ili ukweli ujulikane,” amesema.

Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo (MDO) Baraka Msumi alisema kuwa atawapa ushirikiano wa kutosha Maofisa wa TAKUKURU na vyombo vingine vya dola vitakapokuja kufanya uchunguzi katika mradi huo.  

 Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Ellis Lucas Ndelemba alisema mradi huo ulianza kutekelezwa na halmashauri hiyo mwezi Machi 2020 kwa kutumia fosi akaunti (force account) na ulitarajiwa kuanza kutumika mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles